Prime
Ruben Amorim aiba kitabu cha Arteta
Muktasari:
- Man United, ambayo kwa sasa ipo nafasi ya 13 katika msimamo wa Ligi Kuu England pengine itahitaji kufanya kwa ubora zaidi kuliko wapinzani wao wa Anfield na Emirates wakati zilipokuwa katika kipindi cha mabadiliko.
MANCHESTER, ENGLAND.
PRESHA ipo juu kwa kocha Ruben Amorim baada ya dirisha la usajili la majira ya baridi huko Ulaya kufungwa, huku chama lake la Manchester United likishindwa kunasa mastaa wa maana wa kuja kuongeza nguvu kikosini.
Ni ngumu kuamini kwamba Amorim alichohitaji ni kumsajili beki wa kushoto tu na yule beki kinda wa kutoka Arsenal - hata kama alifurahia kwa kitendo cha kuwaondoa Marcus Rashford na Antony kwenye kikosi chake.
Pesa inaonekana kuwa kikwazo kikubwa kwa Man United kushindwa kuwa na nguvu kwenye soko la usajili katika dirisha la Januari huku ikifahamika wazi kikosi hicho kina shida nyingi zinazohitaji kurekebishwa kwa kile kilichotokea hadi sasa msimu ulipofikia.
Mashabiki wengi wa Man United walimtaka Amorim na mabosi wake, akiwamo bilionea Sir Jim Ratcliffe kufanya usajili kwenye dirisha dogo. Hata hivyo, pamoja na ishu ya kifedha, pengine Amorim na Man United wameamua kupita njia ambazo Liverpool na Arsenal zimepita hadi kufikia ubora wao sasa, zikitajwa kama timu bora kwenye Ligi Kuu England na kufukuzia ubingwa wa ligi hiyo msimu huu.
Mabadiliko yanahitaji muda. Ni suala la kuhitaji usahihi na sio kufanya tu ilimradi, kila kitu kizuri kinahitaji muda.
Man United, ambayo kwa sasa ipo nafasi ya 13 katika msimamo wa Ligi Kuu England pengine itahitaji kufanya kwa ubora zaidi kuliko wapinzani wao wa Anfield na Emirates wakati zilipokuwa katika kipindi cha mabadiliko.
Makocha Jurgen Klopp na Mikel Arteta, walifanya kazi kubwa kufanya mabadiliko kwenye timu za Liverpool na Arsenal walipoingia kwa mara ya kwanza na hicho ndizo kitu Amorim anataka kukifanya Man United. Klopp alitua Anfield, alirithi kikosi cha Brendan Rodgers kilichokuwa na shida nyingi.
Mechi yake ya kwanza alitoka sare ya bila kufungana dhidi ya Tottenham Hotspur, huku timu yake ilikuwa na wachezaji kama Martin Skrtel, Mamadou Sakha na Alberto Moreno kwenye beki, Emre Can na Lucas Leiva kwenye kiungo na benchi alikuwa na wachezaji Jordan Ibe, Jerome Sinclair na Kolo Toure. Hakikuwa kikosi cha kupambania mataji na kushinda.
Kitu cha kwanza kufanya Klopp, alianza kubadili akili za wachezaji aliowakuta kwanza kwenye kikosi kabla ya kuanza kuwafungulia mlango wa kutokea mmoja baada ya mwingine ambao aliona watakuwa mzigo kwake.
Na dirisha lake la kwanza la usajili, Klopp akiwa Liverpool, Januari 2006, alimnasa kiungo Marko Grujic na ikamtoa kwa mkopo Red Star Belgrade.
Ilipofika dirisha kubwa, wachezaji 16 - ikiwamo wasiopungua sita ambao walicheza mechi ile ya Spurs, walifunguliwa mlango wa kutokea na hapo wakaletwa Joel Matip, Sadio Mane na Georginio Wijnaldum, wakiwa miongoni mwa nguvu mpya zilizoongezwa kwenye timu.
Jambo hilo lilikwenda sambamba na kuwajenga wachezaji utimamu wao wa mambo ya nje ya uwanja, mazoezini na kwenye vyumba vya kubadilishia. Baada ya hapo Klopp alijifunza kutambua majina ya wafanyakazi wote 80 wa Liverpool waliopo kwenye uwanja wa mazoezi huko Melwood na kisha kuwatambulisha kwa wachezaji. Hiyo ilileta mshikamano na kuibuka na kaulimbinu ya 'One club. One goal'.
Kwamba umoja wao unaanzia kwa mfanyakazi wa kawaida wa kutunza nyasi za uwanjani hadi kwa straika wa timu hiyo ambaye ni staa. Ukapatikana mshikamano. Huko Arsenal, Arteta, aliteuliwa kabla ya Krismasi 2019, dirisha lake la kwanza la usajili aliishia kunasa mchezaji wa mkopo.
Kisha alinasa mastaa watatu, huku Emile Smith Rowe na beki Mavropanos wakaondoka kwa muda. Mabadiliko makubwa ya klabu yalikuja baada ya hapo. Januari waliwasili Pablo Mari na Cedric Soares ambao dili zao za mkopo zikafanywa za jumla, huku beki wa Kibrazili Gabriel, kiungo Thomas Partey na winga Willian waliongezwa kikosini.
Na safisha safisha ilianza kueleweka kwenye dirisha lake la pili na tatu, ambapo Henrikh Mkhitarian, Mesut Ozil na mabeki Sokratis na Mustafi wote waliondoka Januari 2021 na wakafuatiwa na straika Pierre-Emerick Aubameyang.
Ilipofika Agosti 2022, chini ya miaka mitatu tangu alipotua Emirates, wachezaji watano tu ndiyo waliokuwa na uhakika wa nafasi kwenye timu yake, ambapo Bukayo Saka, Smith Rowe, Granit Xhaka, Gabriel Martinelli na Reiss Nelson - ambapo timu hiyo ilijijenga na kuwa ya kiushindani kwa sasa.
Kama ilivyokuwa kwa Klopp, hata Arteta naye alijali kwenye kuvumilia na kuijenga timu kuwa ya viwango kuliko kuhitaji mabadiliko ya haraka. Arteta aliondoa wachezaji ambao aliona kwamba hawana kitu kipya cha kumpa kwenye mipango yake. Akajenga timu mpya na sasa ni tishio.
Wakati anatimiza miaka yake mitano kwenye kikosi cha Arsenal, Desemba mwaka jana, Arteta alisema: “Kitu cha kwanza nilichofanya ni kutengeneza umoja kwenye timu kuanzia kwa wafanyakazi hadi kwa wachezaji, niliwaambia ninachofikiria na kama tutashindwa kukifanya, basi tutashindwa kufikia mafanikio.”
Hizo ndizo njia walizopita Klopp na Arteta katika kuzifanya timu zao za Liverpool na Arsenal kuwa tishio.
Walianza kwa kuwaondoa wachezaji ambao waliwakuta na kuona hawana jipya kwenye timu, kama ambavyo Amorim ameanza kukifanya huko Old Trafford, akianza na Antony na Marcus Rashford.
Arteta alianza kwa kuwaweka benchi vipenzi vya Arsenal kama Aubameyang na Ozil kabla ya kuwaondoa, kitu ambacho kimekuja kufanywa na Amorim, alipomweka benchi kipenzi cha Old Trafford, Rashford kabla ya kumwondoa kwenye kikosi chake kwa mkopo kwenda Aston Villa.
Kwa matukio yanavyoonekana kushabiana, unaweza kusema Amorim anapitia vitabu vya Arteta na Klopp kujaribu kurudisha zama bora Man United. Tofauti iliyopo ni kwamba kwa Arteta na Klopp hawakuwa na nyakati ngumu sana kama zinazomkabili Amorim kwa sasa.
Klopp alipoteza mechi moja tu kati ya 11 za kwanza, wakati Arteta alipoteza moja kati ya 14. Kwa Amorim mambo ni tofauti, amepoteza mechi sita kati ya 11 za kwanza tangu alipochukua mikoba ya kuinoa Man United kutoka kwa Mdachi Erik ten Hag.
Mambo yamekuwa magumu, kwa ujumla wake timu hiyo imeshinda mara nane katika mechi 19, imepata ushindi mara nne tu katika mechi 13 za mwisho, huku ikipoteza mara saba katika Ligi Kuu England. Kubadilibadili kikosi mara kwa mara imetajwa kuwa tatizo jingine, lakini Amorim anafanya hivyo ili kutambua uwezo wa kila mchezaji katika kumpa nafasi ili kitakapofika kipindi cha kufanya uamuzi wa nani aondoke na nani abaki, kusiwepo na malalamiko.
Amorim bado anafanya majaribio, hajajipata. Kwenye mechi dhidi ya Crystal Palace, Jumapili iliyopita aliamua kucheza na Namba 9 bandia, alipomtumia kiungo Kobbie Mainoo na kuwaacha benchi mastraika wa asili, Joshua Zirkzee na Rasmus Hojlund. Amefanya hivyo kujaribu kutafuta suluhu ya kupatikana mabao kwenye timu hiyo, jambo ambalo kwa sasa linaonekana kuwa tatizo.
Ulipofika usajili wake wa kwanza, Amorim amenasa saini ya mchezaji mmoja tu wa kikosi cha kwanza, beki wa kushoto, Patrick Dorgu. Hilo linazidi kuthibitisha namna Amorim anavyopita kwenye njia za Arteta na Klopp wakati walipokuwa wakiboresha vikosi vyao.
Rekodi zinaonyesha kwamba Klopp msimu wake wa kwanza Liverpool, timu ilimaliza nafasi ya nane, sawa na Arteta, naye timu yake ilimaliza namba nane. Amorim kwa sasa timu yake ipo kwenye nafasi ya 13 na inatazamwa hali itakavyokuwa hadi kufikisha mwisho wa msimu. Man United itamaliza nafasi gani.
Mechi ya kwanza ya Klopp (Liverpool vs Spurs): Mignolet; Clyne, Skrtel, Sakho, Moreno; Coutinho, Can, Milner, Lallana, Lucas; Origi
Mechi ya kwanza ya Arteta (Arsenal vs Everton): Leno; Chambers, Luiz, Maitland-Niles, Saka; Torreira, Smith Rowe, Xhaka; Martinelli, Aubameyang, Nelson
Mechi ya kwanza ya Amorim (Man United vs Ipswitch); Onana, Mazraoui, De Ligt, Fernandes, Rashford, Eriksen, Amad, Garnacho, Casemiro, Dalot, Evans.