Prime
Tulitakiwa tuanze na kina Shalulile
JINA la mshambuliaji wa kimataifa wa Namibia, Peter Shalulile ndio habari ya mjini hivi sasa baada ya nyota huyo wa zamani wa Mamelodi Sundowns kusaini mkataba wa kuichezesa Yanga kuanzia msimu wa 2026-2027.
Habari hiyo inazungumzwa kwa mitazamo tofauti, ukianzia na ule unaomuona kama nyota wa kimataifa wa kiwango cha juu ambaye amekuja kuizindua Ligi Kuu Bara iliyojaa wachezaji wageni wenye viwango vya kawaida.
Lakini, upo mtazamo unaomuona mshambuliaji huyo kama mchezaji aliyechoka, mwenye umri mkubwa ambaye kwa maneno ya mitaani amekuja kuchukua pensheni yake wakati huu anapokaribia kustaafu baada ya kucheza soka la kiwango cha juu kwa muda mrefu.
Kwangu yote mawili ni sawa. Ni nyota mkubwa anayekuja kuongeza thamani kwenye ligi yetu na ni kweli kuja kwake ni sehemu ya kuhitimisha soka lake lililojaa mafanikio na asingeweza kwenda sehemu ambayo angepata fedha nzuri za kumalizia soka lake.
Kikubwa ni kwamba yote mawili yana faida, lakini kama ungeniuliza ningekwambia hilo la pili ni muhimu sana kwa soka letu la Tanzania; kupata mchezaji wa kiwango cha juu anayekuja kustaafia Tanzania.
Ndivyo soka la sasa linavyoendeshwa duniani kote. Katika kiwango chake cha juu na umri mdogo isingekuwa rahisi kwa klabu za Tanzania kunasa saini yake kutokana na uwezo wa kiuchumi.
Klabu tajiri kama za ukanda wa kaskazini, baadhi za Afrika Kusini na hata zile za Ulaya zina macho makali ya kuona vipaji katika umri mdogo na zina mabavu ya kiuchumi wa kuweza kumchukua kwa bei yoyote.
Kama Barcelona ilimuona Lionel Messi akiwa mtoto mdogo, zitakosaje kumuona mtoto mdogo wa Kiafrika anayeweza kuwa nyota wa dunia? Macho makali ya mawakala wa wachezaji huweza kutambua uwezo wa baadaye wa mchezaji katika umri mdogo na kutuma taarifa kwa klabu kubwa duniani.
Ndio maana isingekuwa rahisi kuipoka Mamelodi Sundowns kipaji cha Shalulile wakati kikiwa katika viwango vya juu. Lakini umri wake haumzuii kuendeleza makali yake na kuchangia uzoefu wake na hata kuiongezea thamani Yanga na ligi kwa ujumla.
Tumetoka kushuhudia fainali za Kombe la Dunia nchini Marekani, Canada na Mexico zilizovunja rekodi za mahudhurio. Inakadiriwa kuwa mashabiki zaidi ya milioni 6.8 waliangalia mechi za fainali hizo msimu huu na kuvunja rekodi ya mwaka 1994 wakati mashindano hayo yalipofanyika Marekani na kuangaliwa na watu zaidi ya milioni tatu.
Wamarekani wanaona kuwa hayo ni matokeo ya mkakati wa kuitangaza soka nchini Marekani baada ya kuandaa fainali hizo. Ligi Kuu ya Marekani (MLS) ikaanzishwa mwishoni mwa miaka ya tisini.
Ligi hiyo ilianzishwa kwa waandaaji kuwa na sauti katika usajili. Sera ililenga wachezaji nyota duniani waliokuwa wakielekea kustaafu ndio wasajiliwe. Nyota hao walipangwa kwenye timu zilizo katika majimbo yenye watu wenye asili inayolingana na nyota hao.
Hilo lilisaidia kuanza kushtua watu kuwa kuna mchezo wenye wachezaji wa asili yao na kuanza kwenda viwanjani. Kuanzia enzi hizo hadi hizi za sasa za akina Lionel Mesi, soka nchini Marekani limekuwa maarufu na sasa linaweza kutuma nyota wake barani Ulaya, kama akina Christian Pulisic ambaye anaichezea Roma ya Italia.
Kwa hiyo akina Messi na nyota wengine kutoka klabu za barani Ulaya wamesaidia kuongeza thamani ya Ligi Kuu ya Marekani kwa kuvuta mashabiki viwanjani na katika televisheni, hivyo kuongeza uchumi wa mchezo huo katika nchi ambayo michezo ni biashara kubwa.
Kwa mfano katika mechi za Kombe la Dunia, mapumziko ya afya (hydration break) huwa hayana matangazo kwenye televisheni, lakini kwa Marekani, kituo cha Fox kiliwatoza watoa matangazo kuanzia Dola 200,000 kwa tangazo la sekunde 30 hadi Dola 750,000 wakati Marekani ikicheza.
Hapo unaweza kuona thamani iliyoongezwa na nyota hao inavyochangia katika uchumi wa mpira wa miguu. Kwa hiyo suala hapa si umri, bali ni thamani wanayotembea nayo wachezaji wanaoelekea kustaafu kwa kuwa walishajigtengenezea jina wakati wakiwa katika viwango vyao vya juu na jina hilo wanaenda nalo kwenye klabu zinazotafuta mafanikio ya uwanjani na nje ya uwanja.
China ilijaribu kutumia dhana hiyo, lakini haikuwa na mkakati mzuri wa kifedha wa kuendana na mkakati huo, ndio maana ilifikia wakati klabu iliyotwaa ubingwa ikafilisika na kushindwa kuendelea na ligi. Faida nyingine ni ukweli kwamba nyota wanaoelekea kustaafu huwa hawana gharama kubwa. Baadhi huchukuliwa kwa mkopo, wengine bure baada ya kumaliza mkataba na wengine thamani ya bei yao huwa ndogo kutokana na kubakiza muda mfupi kabla ya kumaliza mkataba.
Kitu ambacho kitasumbua ni mshahara kwa kuwa hauwezi kushushwa. Hapo ndipo klabu zinazomchukua hutakiwa kujiandaa kiuchumi kumlipa mshahara na marupurupu mengine.
Mbali na thamani hiyo ya kifedha, wachezaji nyota wanaoelekea kustaafu husaidia kuchangia maendeleo ya mpira kutokana na uzoefu wao.
Hawa husaidia kuongeza uzoefu kwa wachezaji wengine vijana, kama vile Shalulile alivyo mpiganaji kwa dakika zote tisini, au Lionel Messi anavyoamua kupambana kuibeba timu pale inapoonekana kila kitu kimeshindikana.
Mazungumzo na wachezaji wenzake na tabia binafsi huwa kitu muhimu kwenye timu na hali kadhalika mbinu binafsi na nidhamu ya mbinu za mchezo kulingana na mkakati wa kocha.
Sera kama hii ndiyo tulitakiwa tuwe nayo. Leo Bodi ya Ligi imekuja na kanuni kwamba mchezaji wa kigeni atakayesajiliwa Tanzania ni lazima awe alishachezea timu za vijana. Lakini si wachezaji wote wanaoweza kuitwa timu za taifa kutokana na sababu mbalimbali.
Hili ni ongezeko katika kanuni kwamba mchezaji wa kigeni ni lazima atoke klabu za juu kwenye nchi anakotoka. Kwa kuwa tulishazipa klabu uhuru wa kusajili, hatuwezi kuzilazimisha zisajili wachezaji nyota barani Afrika wanaoelekea kustaafu ili waje kuongeza thamani. Lakini hili lingewezekana ndio lingesaidia timu zetu ndani na nje ya uwanja kama ilivyo Marekani na hata Saudia.
Uhuru wa kusajili na kutokuwa na sera nzuri ndio uliosababisha tukawa na wachezaji kama Robert Jama Mba aliyeshindwa kabisa kuonyesha hata cheche ndogo ambazo zingethibitisha sababu za Yanga kumfuata.
Na sasa tumejaza lundo la wachezaji kutoka nje ambao wanazurura kwenye klabu zetu wakati wa usajili mkuu na usajili mdogo kana kwamba wakiondoka nchini hawataweza kupata timu tena.
Tunahitaji sera nzuri za usajili wa wachezaji wa kigeni na kwangu aina hii ya wachezaji kama Shalulile ndio ingefaa zaidi kwa kuwa ingesaidia kutuongezea thamani badala ya kuokota mabaki huko nje eti kwa sababu ni vijana.