Ronaldo ataka kocha mpya Ureno
Muktasari:
- Ronaldo mwenye umri wa miaka 41 ameamua kufunga ukurasa wa kuitumikia timu ya taifa ya Ureno baada ya kipindi kirefu kilichojaa mafanikio, rekodi na makombe mbalimbali.
LISBON, URENO: SUPASTAA wa soka duniani, Cristiano Ronaldo, anatarajiwa kuwa na kocha mpya katika mchezo wake wa mwisho wa kuiwakilisha timu ya taifa ya Ureno, huku aliyekuwa kocha wake wa zamani, Luiz Felipe Scolari, akitajwa kuwa mmoja wa wanaoweza kupewa jukumu hilo.
Ronaldo mwenye umri wa miaka 41 ameamua kufunga ukurasa wa kuitumikia timu ya taifa ya Ureno baada ya kipindi kirefu kilichojaa mafanikio, rekodi na makombe mbalimbali.
Uamuzi huo unakuja kufuatia taarifa za kutokuelewana kwake na kocha Jorge Jesus, ambaye inadaiwa alimuacha nje ya kikosi katika mchezo dhidi ya Norway, Septemba mwaka huu.
Hatua hiyo ilimfanya nyota huyo kuondoka kambini akiwa na hasira, kabla ya kuamua kusitisha safari yake ya kuitumikia timu ya taifa.
Hata hivyo, Ronaldo hataki kuondoka kimya kimya, kwani anatarajiwa kupewa nafasi ya kucheza mchezo mmoja wa mwisho kama sehemu ya kumuaga rasmi baada ya kuitumikia Ureno kwa zaidi ya miongo miwili.
Jina la Scolari limeibuka kuwa miongoni mwa yanayozungumziwa kuiongoza timu hiyo katika mchezo huo wa kihistoria, huku Ronaldo akikataa Jesus kuwa kwenye benchi.
Scolari ndiye aliyempa Ronaldo nafasi yake ya kwanza katika timu ya taifa mwaka 2004, wakati nyota huyo akiwa anaanza safari yake ya kuwa mmoja wa wanasoka wakubwa duniani.
Uhusiano wa wawili hao ulikuwa wa karibu, huku Ronaldo akimuunga mkono kocha huyo katika kipindi kigumu cha maisha yake baada ya kumpoteza baba yake akiwa na umri wa miaka 20.
Kwa upande mwingine, aliyekuwa kocha wa Ureno, Fernando Santos, ambaye alifanya kazi na Ronaldo kati ya mwaka 2014 na 2022, hatarajiwi kupewa jukumu hilo.
Santos alifanikiwa kuiongoza Ureno kutwaa ubingwa wa Euro 2016, lakini uhusiano wake na Ronaldo uliripotiwa kuharibika baada ya kumuweka benchi nyota huyo katika Kombe la Dunia 2022.
Ronaldo mwenyewe ameeleza kuwa haikuwa rahisi kufanya uamuzi wa kuachana na timu ya taifa, akisema jezi namba saba aliyovaa kwa miaka 23 ilikuwa na maana kubwa kwake.
"Siku imefika ya mimi kuikabidhi jezi namba saba ya timu yetu ya taifa kwa kizazi kijacho. Haikuwa uamuzi rahisi, kwa sababu baadhi ya maamuzi hayafanywi kwa akili pekee, bali pia kwa moyo," amesema Ronaldo.
Ameongeza kuwa safari yake iliyoanza Agosti 2003 imebadilisha maisha yake na kumpa nafasi ya kuwakilisha mamilioni ya watu wa Ureno duniani.
"Nilipokuwa na timu ya taifa sikuona tu mechi, mabao, rekodi na mataji. Niliona watu, niliona Wareno wanaoishi nje ya nchi ambao kwa dakika 90 walijihisi kuwa karibu na nyumbani," amesema.
Kwa upande wake, Jorge Jesus ameheshimu uamuzi wa Ronaldo licha ya tofauti zilizoripotiwa kati yao.
"Cristiano ni alama kubwa duniani na mfano kwa Ureno pamoja na timu ya taifa. Nilimuomba aendelee kuwa pamoja nami kwa sababu nilihitaji uwepo wake, lakini lazima nikubali uamuzi wake," amesema Jesus.
Alisisitiza kuwa Ronaldo ataendelea kuwa na nafasi ya pekee katika mioyo ya wananchi wa Ureno na historia ya soka la taifa hilo.
Katika kipindi chake cha kimataifa, Ronaldo ameifungia Ureno mabao 146 katika mechi 234, huku akisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa wa Euro 2016.
Safari yake inapokaribia kufikia tamati, mashabiki wa soka duniani wanasubiri kwa hamu mchezo huo wa kumuaga mmoja wa wachezaji walioweka alama kubwa katika historia ya mchezo huo.