Ronaldo aonyesha ubora: ‘Bicycle Kick’ yaleta ushindi wa 4–1 kwa Al-Nassr
Muktasari:
- Al-Nassr ilianza mchezo kwa kasi, ambapo João Félix alifungua ukurasa wa mabao kabla ya Wesley kuongeza la pili. Al-Khaleej walipata bao lao la kufutia machozi mapema kipindi cha pili kupitia Murad Al-Hawsawi, lakini Sadio Mané aliirejesha Al-Nassr kwenye uongozi mnono kwa kufunga bao la tatu.
Mshambuliaji mkongwe Cristiano Ronaldo ameendelea kudhihirisha kuwa bado ana ubora wa hali ya juu baada ya kufunga bao maridadi la ‘Bicycle Kick’ katika ushindi wa 4–1 wa Al-Nassr dhidi ya Al-Khaleej kwenye Ligi Kuu ya Saudi.
Al-Nassr ilianza mchezo kwa kasi, ambapo João Félix alifungua ukurasa wa mabao kabla ya Wesley kuongeza la pili. Al-Khaleej walipata bao lao la kufutia machozi mapema kipindi cha pili kupitia Murad Al-Hawsawi, lakini Sadio Mané aliirejesha Al-Nassr kwenye uongozi mnono kwa kufunga bao la tatu.
Dakika za nyongeza, Ronaldo aliwapa mashabiki kilio cha furaha baada ya kufunga bao la kuvutia kwa kuruka na kupiga ‘Bicycle Kick’ akitumia krosi ya Nawaf Boushal. Bao hilo liliimarisha ushindi wa Al Nassr na kuwa moja ya mabao bora msimu huu.
Ushindi huo uliifanya Al-Nassr kuendeleza rekodi yao ya kushinda mechi tisa mfululizo kwenye ligi, huku Ronaldo akifikisha bao lake la 954 katika maisha yake ya soka.