Mashabiki Ureno waibua mjadala mzito, Ronaldo akitajwa
Muktasari:
- Hilo limeibuka na baada ya kikosi hicho kuangusha kipigo kizito kwa Armenia cha mabao 9-1 katika mchezo wa kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 uliofanyika jana Jumapili.
LISBON, URENO: MJADALA umeibuka. Mashabiki wa soka wanaamini timu ya taifa ya Ureno inakuwa bora zaidi inapocheza bila ya huduma ya supastaa Cristiano Ronaldo.
Hilo limeibuka na baada ya kikosi hicho kuangusha kipigo kizito kwa Armenia cha mabao 9-1 katika mchezo wa kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 uliofanyika jana Jumapili.
Katika mchezo huo, Ureno haikuwa na huduma ya Ronaldo baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu kutokana na kumpiga kiwiko beki wa Ireland, Dara O’Shea kwenye mchezo wa kufuzu fainali za Kombe la Dunia, Alhamisi iliyopita.
Alipoonyeshwa kadi nyekundu, Ronaldo aliwapigia makofi ya kejeli mashabiki wa Ireland uwanjani Aviva huku pia alizozana na kocha wa timu hiyo, Heimir Hallgrimsson wakati alipokuwa akitoka uwanjani.
Ronaldo, 40, yupo kwenye hatari ya kukosa mechi nyingi zaidi kutokana na kadi hiyo nyekundu kuonekana kama ilitokana na tatizo la kushambulia, hivyo anaweza kukosa mechi ya kwanza ya Ureno kwenye fainali za Kombe la Dunia 2026.
Lakini, kikosi hicho cha kocha Roberto Martinez kilishinda 9-1 bila ya huduma ya nahodha wao, jambo lililowaibua mashabiki wa soka wakihoji kama kukosekana kwa Ronaldo kuna faida kubwa kwa timu hiyo katika kushinda mechi zake bila ya kutumia nguvu nyingi.
Shabiki mmoja amesema kwenye X: “Ureno bila ya Ronaldo imekuwa timu bora zaidi…”
Mwingine alikubaliana na hilo, aliposema: “Mashabiki wa Ronaldo watachukia huu ukweli, lakini Ureno inakuwa timu bora bila ya huduma yake.”
Kiungo Bruno Fernandes alifunga hat-trick katika mechi hiyo, ikiwamo penalti mbili. Joao Neves pia alifunga mara tatu katika mechi hiyo, huku Renato Veiga, Francisco Conceicao na Gonçalo Ramos, kila mmoja alifunga mara moja, kuhitimisha ushindi huo mnono wa mabao tisa.
Shabiki mmoja aliona kiwango cha kwenye mechi hiyo kilithibitisha ubora wa kiungo wa Man United, Fernandes kuwa steringi mpya wa Ureno.
Shabiki huyo amesema: “Ni salama kusema hili hii sio Ureno ya Ronaldo. Hii ni timu ya Bruno Fernandes.”
Wakati shabiki wa nne alikubali CR7 sio shujaa tena wa taifa lake, aliposema: “Ronaldo ndiye mtu anayeifanya Ronaldo kufanya hivyo.”
Kwenye mabao yaliyofungwa katika mechi hiyo, mfano Neves, aliyefunga hat-trick, ikiwamo friikiki matata kabisa, mipira ambayo Ronaldo alikuwa akijinasibu kwamba yeye ndiye mkali wa kufanya jambo hilo uwanjani.
Ronaldo, ambaye ni straika wa Al-Nassr hakuwapo uwanjani Estadio da Dragao huko Porto kwenye mchezo huo, ambapo ushindi umeifanya Ureno kukamatia tiketi ya kwenda kucheza fainali hizo za Kombe la Dunia 2026, zitakazofanyika Marekani, Mexico na Canada.
Lakini, Ronaldo alituma ujumbe wa kuwahamasisha wenzake kufanya kweli kwenye mchezo huo kupitia ukurasa wake wa Instagram, akilenga kwenda kuvunja rekodi ya kucheza fainali za sita za Kombe la Dunia, ambapo kwa wakati huo atakuwa na umri wa miaka 41.