Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ronaldo aondoka Ureno, ‘ukweli nitausema’

RONALDO Pict

Muktasari:

  • Kuondoka kwa Ronaldo kambini kumekuja siku chache baada ya Kocha Mkuu wa Ureno, Jorge Jesus, kukanusha kuwepo kwa mgogoro kati yake na nahodha huyo, kufuatia madai kwamba mshambuliaji huyo alikataa kufanya mazoezi.

LISBON, URENO: CRISTIANO Ronaldo ameondoka kwenye kambi ya timu ya Taifa ya Ureno na kusema atakuja kueleza sababu zilizomfanya kufanya hivyo “kwa wakati unaofaa”, hatua inayoongeza maswali kuhusu kinachoendelea ndani ya kikosi hicho.

Kuondoka kwa Ronaldo kambini kumekuja siku chache baada ya Kocha Mkuu wa Ureno, Jorge Jesus, kukanusha kuwepo kwa mgogoro kati yake na nahodha huyo, kufuatia madai kwamba mshambuliaji huyo alikataa kufanya mazoezi.

Ronaldo, 41, aliwahi kusema alifikiria kustaafu soka la kimataifa baada ya Kombe la Dunia, lakini akaamua kuendelea na harakati zake za kufikisha mabao 1,000 katika maisha yake ya soka.

RONAL 01

Alijumuishwa kwenye kikosi cha wachezaji 25 kilichoitwa kwa mechi za kimataifa za kipindi hiki na kuanza katika mchezo wa Ligi ya Mataifa dhidi ya Wales.

Hata hivyo, mshambuliaji huyo wa Al-Nassr hakutumia dakika yoyote katika ushindi wa Ureno wa mabao 2-1 dhidi ya Norway mjini Oslo Jumapili, huku pia akishindwa kwenda kuwasalimia mashabiki wa Ureno pamoja na wenzake baada ya mchezo kumalizika.

Badala yake, nyota huyo wa zamani wa Real Madrid na Manchester United alikwenda moja kwa moja vyumbani, hali iliyozua taarifa kwamba huenda hakufurahishwa na uamuzi wa kocha Jesus.

RONAL 02

Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya mchezo wa Ureno dhidi ya Denmark, Jesus amesisitiza kuwa hakukuwa na tukio lolote la ugomvi kati yake na Ronaldo.

“Hakukuwa na tukio lolote. Mchezaji yeyote na mimi pia nilikuwa mchezaji akikaa dakika 20 au 30 akipasha misuli na kisha asiingie uwanjani, hakuna anayefurahia hilo,” amesema Jesus.

Kocha huyo amesema alimweleza Ronaldo kabla ya mchezo kwamba hatakuwa kwenye kikosi cha kwanza, lakini angeweza kumuingiza baadaye.

“Baada ya hapo, kama kocha, niliamua kutomuingiza. Hakuna jambo la kufanya kelele kuhusu hilo,” ameongeza.

RONAL 03

Jesus pia alikanusha taarifa kwamba Ronaldo alikataa kufanya mazoezi Jumanne, akisema mchezaji huyo alipewa mazoezi binafsi kwa ajili ya kuimarisha mwili na uwezo wa kujisogeza, kabla ya kutakiwa kufanya mazoezi ya kawaida Jumatano.

Baadaye Ronaldo alitumia ukurasa wake wa Instagram kuthibitisha kuwa ameondoka kambini.

“Baada ya mkutano wa waandishi wa habari wa timu ya Taifa na kufuatia mazungumzo yangu na rais wa Shirikisho la Soka la Ureno, nimeamua kuondoka kwenye kambi ya timu ya taifa,” aliandika Ronaldo.

“Kwa wakati unaofaa, nitawaeleza Wareno wote ukweli kuhusu sababu zilizonifanya kuondoka.”

Ronaldo pia aliwatakia wenzake kila la heri katika michezo yao ijayo.

Mshambuliaji Goncalo Ramos ndiye aliyefunga bao la ushindi dhidi ya Norway, huku Jesus akisema mshambuliaji huyo wa AC Milan angeendelea kupewa nafasi mbele ya Ronaldo katika mchezo dhidi ya Denmark.