Ronaldo ampa kongole Messi
Muktasari:
- Messi, 39, alicheza mechi yake ya mwisho akiwa na Argentina dhidi ya Benin wiki hii, akianza katika ushindi wa mabao 3-0 na kufikisha jumla ya mechi 208 alizoichezea nchi yake.
BUENOS AIRES, ARGENTINA: CRISTIANO Ronaldo ameweka pembeni ushindani wake wa muda mrefu na Lionel Messi, akimtumia ujumbe wa heshima baada ya nyota huyo wa Argentina kufunga rasmi ukurasa wake wa miaka 21 akiwa na timu ya taifa.
Messi, 39, alicheza mechi yake ya mwisho akiwa na Argentina dhidi ya Benin wiki hii, akianza katika ushindi wa mabao 3-0 na kufikisha jumla ya mechi 208 alizoichezea nchi yake.
Nyota huyo wa zamani wa Barcelona alihitimisha safari yake kwa namna ya kuvutia, akifunga bao moja kwa penalti na kutoa pasi mbili za mabao kabla ya kupewa heshima kubwa na mashabiki 85,000 waliojazana uwanjani Buenos Aires.
Baada ya mchezo huo, Messi alishindwa kuyazuia machozi alipokuwa akitoa hotuba ya kuwaaga mashabiki, akieleza jinsi anavyopenda kuendelea kuichezea Argentina milele.
Ronaldo, ambaye kwa miaka mingi amekuwa mpinzani mkubwa wa Messi katika soka la dunia, alitumia ujumbe wa Messi kwenye Instagram kumuenzi mshindi huyo wa Kombe la Dunia 2022.
“Baada ya miaka mingi ya kuitetea nchi yako na historia itakayoishi milele. Una heshima yangu yote kwa kila kitu ulichofanikiwa ukiwa na Argentina. Kumbatio,” aliandika Ronaldo.
Messi na Ronaldo wamekuwa wakishindana kwa miaka mingi katika tuzo ya Ballon d’Or, huku Messi akitwaa mara nane dhidi ya tano za Ronaldo.
Messi alifunga safari yake ya kimataifa akiwa ameisaidia Argentina kushinda Kombe la Dunia mwaka 2022, Copa America na mataji mengine, huku Ronaldo akiwa bado anaendelea kuichezea Ureno.
Katika ujumbe wake wa kuaga, Messi amesema safari yake ilikuwa ya kipekee licha ya kuwa na nyakati za furaha na huzuni.
“Jana ilikuwa mechi yangu ya mwisho na tayari ninaikosa jezi ya bluu na nyeupe. Najua nimefanya uamuzi sahihi.
“Ilikuwa safari ya ajabu iliyojaa furaha na huzuni, lakini nina hakika kila hatua niliyopiga ilikuwa na thamani.
“Naondoka nikiwa na shukrani, fahari na amani. Nawapenda nyote na nitawakumbuka. Asanteni kwa kila kitu,” aliandika.
Messi aliingia uwanjani akiwa ameambatana na watoto wake watatu, Thiago, 13, Mateo, 10, na Ciro, nane, kabla ya kupewa burudani ya kipekee na mashabiki waliojazana uwanjani.
Katika hotuba yake ya takribani dakika 10, Messi amesema anajivunia kuwa raia wa Argentina na kwamba ataikumbuka sana nafasi ya kuichezea nchi yake.
“Nawapenda nyote na ninajivunia kuwa Muargentina. Naondoka nikiwa na shukrani, fahari na amani. Asanteni kwa kila kitu,” amesema.