Ronaldo amlipua Jesus, aomba radhi Ureno
Muktasari:
- Ronaldo, 41, amesema Jesus alimwahidi angemwingiza kipindi cha pili na kumtumia kwa takribani dakika 30, lakini licha ya kuanza kupasha misuli moto wakati wa mapumziko, alikaa benchi hadi mchezo ulipomalizika.
NAHODHA wa Ureno na mshambuliaji wa Al Nassr, Cristiano Ronaldo, amevunja ukimya kuhusu kuondoka kambini mwa timu hiyo ya taifa, akifichua kuwa uamuzi huo ulitokana na ahadi ambayo kocha Jorge Jesus alimpa kabla ya mchezo dhidi ya Norway, lakini hakuitimiza.
Ronaldo, 41, amesema Jesus alimwahidi angemwingiza kipindi cha pili na kumtumia kwa takribani dakika 30, lakini licha ya kuanza kupasha misuli moto wakati wa mapumziko, alikaa benchi hadi mchezo ulipomalizika.
Katika taarifa ndefu aliyochapisha kwenye mitandao yake ya kijamii, Ronaldo pia aliomba radhi kwa mashabiki na wachezaji wenzake kwa kuondoka kambini, huku akisema yuko tayari kukubali adhabu yoyote atakayopewa.
“Kocha alikiuka ahadi yake kwangu. Aliniambia nitacheza dakika 30 dhidi ya Norway na nilikubaliana naye. Nilianza kupasha misuli moto kuanzia mapumziko ya kipindi cha kwanza, lakini mwisho wa mchezo sikuitwa kuingia uwanjani,” amesema Ronaldo.
Mshambuliaji huyo amesema tukio hilo lilikuwa la kipekee katika zaidi ya miaka 18 aliyocheza timu ya taifa, akieleza kuwa ilikuwa mara ya kwanza kutocheza hata dakika moja katika mchezo ambao hakuwa nje kwa sababu ya majeraha au adhabu.
Ronaldo amesema baada ya mchezo alijisikia vibaya kiasi cha kushindwa kwenda kuwasalimia mashabiki kama ilivyo kawaida yake.
“Ninaomba radhi kwa mashabiki kwa kutokwenda kuwasalimia baada ya mchezo. Nilikuwa nimekasirika na nilihitaji kuwa peke yangu. Haikuwa kwa sababu ya kutowapenda mashabiki wala kutothamini timu ya taifa,” amesema.
Baada ya tukio hilo, Ronaldo amesema alikutana na Jesus pamoja na Simão Coutinho wa Al Nassr kwa ajili ya kutafuta namna ya kulimaliza suala hilo.
Kwa mujibu wa Ronaldo, katika mazungumzo hayo walikubaliana kwamba Jesus angeeleza hadharani kilichotokea na kuweka wazi kuwa yeye hakuwahi kudai apewe muda maalumu wa kucheza, bali mpango wa kumtumia ulitoka kwa kocha mwenyewe.
Pia amesema walikubaliana Jesus angekiri kuwa kumtaka apashe misuli moto bila hatimaye kumtumia lilikuwa kosa ambalo lisingejirudia.
Hata hivyo, Ronaldo amesema alishangazwa na kauli za Jesus katika mkutano wa waandishi wa habari uliofuata, akidai hazikulingana na makubaliano yao ya faragha.
“Nilisikia kauli na ukali ambao sikuamini kuwa nilistahili. Nilihisi kulikuwa na mtazamo wa ‘mimi nataka, mimi naweza na mimi ndiye ninaeamuru’, jambo ambalo lilikuwa tofauti na tulichokubaliana katika mazungumzo yetu,” amesema.
Ronaldo amesisitiza kuwa hajawahi kuingilia maamuzi ya makocha kuhusu kikosi, mbinu au mfumo wa uchezaji katika kipindi cha takribani miaka 25 akiwa kwenye soka la ushindani.
“Katika miaka yangu 25, sijawahi kuingilia uamuzi wa kiufundi au wa kimfumo wa kocha. Sijawahi kumwambia kocha nani acheze, nani akae benchi au timu icheze kwa namna gani. Ninaheshimu maamuzi yao kwa sababu hilo ni jukumu lao,” amesema.
Kwa mujibu wa Ronaldo, kilichomuudhi zaidi hakikuwa kutocheza dhidi ya Norway, bali kuvunjwa kwa makubaliano aliyodhani yamefanyika kwa uaminifu kati yake na Jesus.
Amesema baada ya kuhisi kuwa hatakiwi tena kambini, aliamua kuondoka badala ya kusubiri tukio jingine litakalomfanya ajisikie hivyo.
“Nilifanya kile ambacho nimekuwa nikisema siku zote kwamba nitafanya pale nitakapohisi sina umuhimu tena. Nilifunga mizigo yangu na kuondoka,” amesema.
Licha ya uamuzi huo, Ronaldo amewataka wachezaji wenzake kutobeba lawama kwa kilichotokea na akaomba radhi kwa kuondoka kambini akiwa nahodha wa Ureno.
“Naomba radhi kwa wachezaji wenzangu. Uwajibikaji wa kuondoka kambini ni wangu pekee. Mimi ni nahodha na najua hilo linaongeza uzito wa jukumu langu. Niko tayari kukubali adhabu yoyote nitakayopewa,” amesema.
Hata hivyo, Ronaldo amesema bado yuko tayari kuendelea kuitumikia Ureno na kurejea kwenye kikosi mara atakapomaliza adhabu, endapo atakuwa fiti na akiendelea kucheza katika kiwango kitakachomuwezesha kuitwa.
“Ukweli ni kwamba ikiwa nitakuwa mzima kiafya, nikiendelea kucheza katika kiwango kinachoniruhusu kuitwa, nitakuwa tayari kuichezea Ureno tena. Ninapofikiria timu ya taifa, ninachofikiria ni kushindana na kushinda,” amesema.
Kwa upande wake, Jesus hajaifunga milango ya Ronaldo kurejea kwenye kikosi cha Ureno, akisema suala hilo liko mikononi mwa mshambuliaji huyo, huku akijaribu kupunguza ukubwa wa mvutano huo na kueleza kuwa haupaswi kuwa sababu ya kudumu ya kuwatenganisha.