Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Morocco ilivyogeuza soka kiwanda na Tanzania inavyoweza kujifunza

Muktasari:

  • Mafanikio hayo hayakutokana na bahati wala kizazi kimoja cha vipaji. Yamejengwa kupitia uwekezaji wa muda mrefu katika miundombinu, akademi, makocha, utambuzi wa vipaji na mfumo wa kitaifa unaounganisha shule, soka la vijana, klabu na timu za taifa.

NCHI ya Morocco imekuwa miongoni mwa mifano inayovutia zaidi barani Afrika kwa namna ilivyoweza kujenga mfumo wa kuzalisha wachezaji na kukuza vipaji vya vijana wazawa badala ya kutegemea zaidi soko la wachezaji wa kigeni.

Mafanikio hayo hayakutokana na bahati wala kizazi kimoja cha vipaji. Yamejengwa kupitia uwekezaji wa muda mrefu katika miundombinu, akademi, makocha, utambuzi wa vipaji na mfumo wa kitaifa unaounganisha shule, soka la vijana, klabu na timu za taifa.

Kiini cha mkakati huo ni Mohammed VI Football Academy, iliyoanzishwa kama sehemu ya mradi wa muda mrefu wa kuimarisha soka la Morocco.

FIFA inaeleza kuwa akademi hiyo, iliyofunguliwa rasmi mwaka 2019 baada ya mchakato wa ujenzi wa miaka kadhaa, ina miundombinu inayokidhi viwango vya FIFA na imekuwa kitovu cha mfumo mpana wa maendeleo ya vipaji.

Mfumo huo hauishii Rabat; Morocco imejenga mtandao wa vituo vya maendeleo katika maeneo mbalimbali, huku vituo vya Sale, Casablanca, Ben Guerir na Laayoune vikitumika katika mchakato wa kuibua na kuendeleza vipaji.

Matokeo yake yanaonekana wazi. Wachezaji kama Nayef Aguerd, Youssef En-Nesyri na Azzedine Ounahi wamepitia mfumo wa maendeleo unaohusishwa na akademi hiyo.

Pia, CAF iliripoti mwaka 2025 kwamba wachezaji watano waliokuwa sehemu ya kikosi cha Morocco katika AFCON, Aguerd, Ounahi, Oussama Targhalline, En-Nesyri na Abdelhamid Aït Boudlal, walitoka katika Mohammed VI Football Academy.

Hii ndiyo tofauti kati ya kuwa na akademi kama jengo na kuwa na akademi kama mfumo wa kitaifa wa kuzalisha vipaji.

Kuanzia mtaani hadi timu ya taifa

Moja ya masomo makubwa ya Morocco ni kwamba utafutaji wa kipaji hauanzi kwenye ligi kuu. Unaanza mtoto akiwa mdogo.

Shirikisho la Soka la Morocco (FRMF) limeeleza mfumo huo unaanzia kwenye soka la mchangani, ambako vipaji hutambuliwa, kisha kupelekwa kwenye akademi za klabu, vituo vya kikanda na hatimaye kituo cha taifa cha ubora.

Shirikisho hilo pia limeunganisha soka na mfumo wa elimu kupitia programu za michezo shuleni.

Nchi inapokuwa na mfumo mzuri wa kugundua na kukuza mtoto mwenye kipaji, klabu haihitaji kila mara kutumia fedha nyingi kumtafuta mchezaji aliyekomaa kutoka nje.

Inajenga thamani ndani ya nchi. Mchezaji anapofikia kiwango cha juu, anaweza kuuzwa ndani ya Afrika au Ulaya, hivyo fedha inayozalishwa na soka inarudi katika mfumo wa maendeleo ya vipaji.

Morocco pia imeendelea kuongeza fursa za watoto kucheza soka katika mazingira salama.

Mwaka 2025, FIFA ilizindua FIFA Arena nchini Morocco na baadaye ikaingia makubaliano ya kusaidia kujenga viwanja vidogo 30 kote nchini.

Wakati huo huo, programu ya Football for Schools inalenga kufikia shule 3,000 nchini humo. Hivyo, dhana si kusubiri mtoto aje kwenye akademi; mfumo unakwenda kumtafuta mtoto pale anapokuwa shuleni, mtaani na katika jamii.

Wachezaji kigeni ruksa

Morocco haikuwakataa kabisa wachezaji wa kigeni. Badala yake, imekuwa na sera zinazolenga kuhakikisha mchezaji wa kigeni anaongeza ubora wa ligi bila kuua nafasi ya mchezaji wa ndani.

Kwa mfano, kanuni za Morocco zimewahi kuweka masharti makali kuhusu wachezaji wa kigeni, yakihitaji kiwango fulani cha uzoefu wa kimataifa.

Kanuni hizo zililenga kuhakikisha mchezaji wa kigeni anayesajiliwa ana thamani ya kiufundi na si mchezaji anayekuja kuchukua nafasi ambayo inaweza kutumiwa na kipaji cha ndani.

Morocco si mfano wa kupunguza wachezaji wa kigeni bali ni mfano wa kujenga mfumo ambao mchezaji wa ndani hawezi kupuuzwa.

Tanzania inaweza kufanya nini?

Tanzania tayari ina baadhi ya vipande vya mfumo huo. TFF imeanzisha programu za maendeleo ya vipaji, mafunzo ya makocha vijana na imekuwa ikiwekeza katika miundombinu.

TFF pia imeeleza mpango wa kuimarisha vituo vya mafunzo na akademi za vijana, huku programu ya U14 ikiendelea kuwanoa vijana katika ufundi, mbinu na maandalizi ya kimwili.

Lakini, hatua inayofuata ni kuunganisha juhudi hizi kuwa mfumo mmoja wa kitaifa.

Kwanza, kila klabu ya Ligi Kuu inapaswa kuwa na akademi yenye viwango vinavyopimika, si akademi kwa jina.

Leseni ya klabu inaweza kuhusishwa na ubora wa timu za U15, U17 na U20, ubora wa makocha, viwanja vya mazoezi na mpango wa kuwapeleka vijana kwenye kikosi cha kwanza.

Pili, Tanzania inahitaji mtandao wa vituo vya vipaji katika mikoa yote. Mtoto kutoka Kigoma, Mtwara, Mwanza au Arusha hapaswi kulazimika kuhamia Dar es Salaam kwanza ndipo mfumo umtambue.

Morocco imeonyesha umuhimu wa kuwa na mfumo unaosaka vipaji katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Tatu, idadi ya wachezaji wa kigeni inaweza kutumiwa kama chombo cha maendeleo, si kama adui wa soka la ndani.

Kwa sasa, klabu za Tanzania zinaweza kusajili hadi wachezaji 12 wa kigeni katika Ligi Kuu. Na utegemezi huo unaonekana pia kwenye ushindani wa ufungaji; mwaka 2026, gazeti la The Citizen lilibainisha kwamba kwa misimu minne mfululizo, tuzo ya Golden Boot ya Ligi Kuu Tanzania imechukuliwa na mchezaji wa kigeni.

Badala ya kupiga marufuku wageni ghafla, Tanzania inaweza kuweka masharti ya kimkakati: wageni wawe na kiwango fulani cha ubora, klabu iwe na idadi ya chini ya wachezaji wazawa kwenye kikosi, na kila klabu iwe na mpango wa kuwapa dakika vijana wake.

Mchezaji wa kigeni awe mwalimu wa vitendo kwa mchezaji Mtanzania, si kizuizi cha maendeleo yake. Tanzania inapaswa kuacha kupima mafanikio kwa idadi ya mataji pekee. Klabu inaweza kushinda ubingwa leo kwa kununua wachezaji 10 kutoka nje, lakini ikiwa baada ya miaka mitano haina wachezaji watatu au wanne waliotengenezwa kwenye akademi yake, mfumo huo haujajenga thamani ya muda mrefu.