Risasi zalindima mechi ya ndondo, Mmoja auawa sita wajeruhiwa
Muktasari:
- Tukio hilo lilitokea katika jiji la San Francisco del Rincón, Jimbo la Guanajuato, Mexico, majira ya saa 8:40 mchana Jumapili, ambapo washambuliaji waliwasili kwa pikipiki hadi eneo la pembeni ya uwanja na kuanza kufyatua risasi kuelekea kwenye umati wa watu.
MEXICO CITY, MEXICO: Mechi ya soka ya mashabiki imegeuka kuwa tukio la kusikitisha baada ya watu wenye silaha kuwafyatulia risasi wachezaji na watazamaji, na kusababisha mtu mmoja kuuawa huku wengine sita wakijeruhiwa.
Tukio hilo lilitokea katika jiji la San Francisco del Rincón, Jimbo la Guanajuato, Mexico, majira ya saa 8:40 mchana Jumapili, ambapo washambuliaji waliwasili kwa pikipiki hadi eneo la pembeni ya uwanja na kuanza kufyatua risasi kuelekea kwenye umati wa watu.
Wachezaji na watazamaji walitawanyika kwa hofu wakijaribu kujiokoa, huku shahidi mmoja akifanikiwa kurekodi tukio hilo kwa simu yake.
Watu saba walipigwa risasi katika shambulio hilo, huku sita wakiendelea kupata matibabu hospitalini. Mmoja kati ya waliojeruhiwa alifariki baadaye hospitalini baada ya ndugu zake kumpeleka kupata matibabu kwa usafiri wao wenyewe.
Aliyefariki ametajwa kuwa Julio César, mfanyabiashara wa vyakula mwenye umri wa miaka 25. Wengine waliotajwa kujeruhiwa ni Israel, 25, na Christian Antonio.
Afisa wa manispaa aliyefika eneo la tukio alisema taarifa za awali zinaonyesha washambuliaji walikuwa wakiwalenga watu wawili, lakini wengine waliokuwa wakikimbia walijeruhiwa kwa bahati mbaya.
“Walionekana kuwalenga watu wawili, lakini wengine walikimbia na kuwa waathirika wa tukio hilo,” alisema afisa huyo.
Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Jimbo la Guanajuato imefungua uchunguzi wa mauaji na inaendelea kuwatafuta washambuliaji waliohusika.
Uongozi wa jiji la San Francisco del Rincón umesema utawasaidia waliojeruhiwa pamoja na familia zao, huku ukishirikiana na vyombo vya uchunguzi katika kufuatilia tukio hilo.
Hili si tukio la kwanza la aina hiyo kutokea katika mechi za soka za mashabiki katika jimbo hilo. Januari mwaka huu, shambulio jingine lilitokea katika jiji la Salamanca na kusababisha watu 11 kuuawa.
Uchunguzi wa tukio la San Francisco del Rincón unaendelea huku mamlaka zikiendelea kuwatafuta waliohusika na shambulio hilo.