Dai Dai ya Shakira yavunja rekodi
Muktasari:
- Wimbo huo wa Kombe la Dunia 2026, michuano iliyofanyika Marekani, Canada na Mexico, umefikisha views bilioni moja kwenye mtandao wa YouTube, ni miezi mitatu baada ya kutolewa Mei 15, 2026. Hakuna uliowahi kufanya hivyo.
WIMBO wa Dai Dai, umeendelea kuvuta mashabiki kwa kasi na sasa umefika kwenye hatua kubwa iliyouingiza kwenye historia kubwa ya nyimbo za Kombe la Dunia.
Wimbo huo wa Kombe la Dunia 2026, michuano iliyofanyika Marekani, Canada na Mexico, umefikisha views bilioni moja kwenye mtandao wa YouTube, ni miezi mitatu baada ya kutolewa Mei 15, 2026. Hakuna uliowahi kufanya hivyo.
Kwa hali hiyo, Dai Dai imeingia kwenye historia ikiwa miongoni mwa nyimbo za Kombe la Dunia zilizofikisha views bilioni moja kwa haraka zaidi.
HISTORIA YA NYIMBO ZA KOMBE LA DUNIA
Ukiangalia historia ya nyimbo za Kombe la Dunia, hasa kipindi ambacho mtandao wa YouTube ulikuwa bado haujaanza kupata umaarufu kama ilivo hivi sasa, utaona tofauti ni kubwa.
Mwaka 2006, "The Time of Our Lives", ulioimbwa na Il Divo na Toni Braxton, ulikuwa wimbo wa Kombe la Dunia lililofanyika nchini Ujerumani, Lakini haukufikia hata karibu na kiwango cha views cha sasa, hadi hivi sasa una views takribani milioni 10 YouTube.
Mwaka 2010 mambo yalibadilika, Shakira na Freshlyground walitoa "Waka Waka (This Time for Africa)" kwa ajili ya Kombe la Dunia lililofanyika nchini Afrika Kusini na wimbo huo haukuwa tu wa mashindano kwani uligeuka kuwa maarufu kwa kizazi na kizazi.
Miaka kadhaa baadaye, Januari 2016, Waka Waka ulifikisha views bilioni moja YouTube. Hadi sasa umeendelea kuongezeka na umefikia zaidi ya views bilioni 4.7.
Baada ya hapo, mwaka 2014, Brazil ilipata "We Are One (Ole Ola)", ulioimbwa na Pitbull, Jennifer Lopez na Claudia Leitte. Wimbo huo uliungwa mkono na majina makubwa, muziki wa Brazil na kutumika katika sherehe za Kombe la Dunia. Hata hivyo, ulitumia miaka mingi kufikisha views bilioni moja YouTube.
Mwaka 2018 katika Kombe la Dunia nchini Urusi, ulitoka "Live It Up", ulioimbwa na Nicky Jam, Will Smith na Era Istrefi, licha ya kuwa na wasanii maarufu, haukufikia umaarufu wa Waka Waka au We Are One kwenye YouTube. Takwimu za sasa zinaonyesha una zaidi ya views milioni 50.
Mwaka 2022, "Hayya Hayya (Better Together)", ulioimbwa na Trinidad Cardona, Davido na Aisha, nao ukawa sehemu ya nyimbo za Kombe la Dunia la Qatar. Ulifanya vizuri, lakini bado haukufikia views bilioni moja. Kwa takwimu za kulinganisha, una takribani views milioni 140.
SASA NI ZAMU YA DAI DAI
Kilichofanya safari ya Dai Dai kuwa ya kipekee ni mchanganyiko wa wasanii ambao si rahisi kuupata, kwani kuna Shakira, msanii ambaye tayari ana historia kubwa na Kombe la Dunia kupitia Wimbo wa Waka Waka na upande mwingine ni Burna Boy, mmoja wa wasanii wakubwa wa Afrika wa kizazi hiki.
Hapo ndipo nguvu ya wimbo ilipoanzia Afrika, Amerika Kusini na mashabiki kutoka duniani kote wakikutana katika wimbo mmoja.
WIMBO HUO HAUJABEBWA NA MAJINA YA WASANII PEKEE
Pia kuna tofauti ya wakati ambao wimbo umetoka, tofauti na mwaka 2006, leo mtandao wa YouTube ni sehemu kubwa ya watu kusikiliza na kutazama muziki.
Wimbo unaweza kutolewa, ukusambaa TikTok na mitandao mingine, ukatumika kwenye video za mashabiki, ukaenea katika nchi mbalimbali, na kila hatua hiyo inawaleta watu tena kwenye video rasmi ya wimbo.
Ndiyo maana Dai Dai ulianza kupata views kwa kasi kubwa. Ndani ya mwezi mmoja tu, ulikuwa tayari umevuka views milioni 225 YouTube.
Hapo ndipo tunapata siri nyingine kuwa si wimbo wa Kombe la Dunia pekee, bali pia ni wimbo wa wasanii wawili ambao tayari wana mashabiki wengi duniani.
Shakira ana historia ya Waka Waka, Burna Boy ana nguvu ya muziki wa Afrobeats. Unapowachanganya wasanii hao kwenye jukwaa kubwa zaidi la michezo duniani, unapata kitu kinachovuka mipaka ya lugha na bara.
Dai Dai ilifikisha views bilioni moja ndani ya siku 113, ni miezi mitatu, wakati Waka Waka ilichukua karibu miaka sita, na We Are One ilichukua miaka mingi zaidi ili kufikia views bilioni moja.
Hata hivyo, miaka ya nyuma wimbo ulitegemea zaidi redio, televisheni, CD na uwanja wa mpira ili kuwafikia watu lakini leo, sekunde chache za video zinaweza kuwafikia mamilioni ya watu kwa wakati mmoja.