Reijnders mdomoni mwa Nottingham Forest
Muktasari:
- Mchezaji huyo ambaye alianza vizuri maisha yake katika kikosi cha Man City msimu uliopita akitokea AC Milan, baadaye alipoteza namba na kuanza kusugua benchi kutokana na ushindani uliokuwepo, licha ya kwamba pale alipoingia uwanjani alionyesha ubora.
KIUNGO wa kimataifa wa Uholanzi na Manchester City, Tijjani Reijnders mwenye umri wa miaka 28 ameibuka kuwa mchezaji anayelengwa na Nottingham Forest, ambayo iko tayari kutoa Pauni 55 milioni ili kumnasa katika dirisha hili la usajili linaloendelea Ulaya kwa sasa.
Mchezaji huyo ambaye alianza vizuri maisha yake katika kikosi cha Man City msimu uliopita akitokea AC Milan, baadaye alipoteza namba na kuanza kusugua benchi kutokana na ushindani uliokuwepo, licha ya kwamba pale alipoingia uwanjani alionyesha ubora.
Forest imedhamiria kuhakikisha kwamba inaboresha eneo la kiungo ambalo limeshapoteza wachezaji kadhaa waliotimka mara tu baada ya msimu uliopita kumalizika, huku kukiwa na nyota wengine wa maeneo tofauti wanaotarajiwa kuondoka katika dirisha hili, hivyo ni lazima izibe mapengo yatakayoachwa.
Reijnders mwenyewe anadaiwa kwamba hayupo tayari kuondoka Man City akitaka kubaki ili kupigania namba kikosini msimu ujao.
Licha ya kutaka kusalia, lakini kuna ongezeko la ushawishi kutoka nje ya England na hivi karibuni kulikuwa na ofa kutoka Italia ambako aliwahi kung’ara kabla ya kutua zake Man City. Ofa pia zipo kutoka Saudi Arabia.
Folarin Balogun
MSHAMBULIAJI wa Marekani, Folarin Balogun mwenye umri wa miaka 25 amepewa ofa ya kujiunga na Tottenham Hotspur kupitia mawakala, huku mustakabali wake katika kikosi cha Monaco haujawa wazi, baada ya kuwepo kwa timu nyingi zinazomtaka kufuatia ubora aliounyesha wakati wa Kombe la Dunia 2026.
Diogo Costa
KIPA wa FC Porto na timu ya taifa ya Ureno, Diogo Costa mwenye umri wa miaka 26 ameanza kuzengewa na Chelsea inayofuatilia uwezekano wa kumsajili. Mchezaji huyo awali alikuwa akihusishwa na Manchester United na ana kipengele cha kuvunjwa mkataba cha takribani Pauni 51 milioni kwa timu inayomtaka.
Geronimo Rulli
GERONIMO Rulli mwenye miaka 34 ambaye ni kipa wa Olympique Marseille na timu ya taifa ya Argentina, anawindwa na Manchester City, huku mazungumzo yakiendelea kati ya klabu hizo. Hata hivyo, nyota huyo pia ana ofa kadhaa kutoka timu mbalimbali zinazocheza Ligi Kuu Hispania.
Savinho
TOTTENHAM Hotspur imeanza mawasiliano na Manchester City kuhusu winga wa kimataifa wa Brazil, Savinho mwenye umri wa miaka 22. Spurs pia inamfuatilia mshambuliaji wa Liverpool na Uholanzi, Cody Gakpo, 27, pamoja na kiungo mshambuliaji wa Eintracht Frankfurt, Mfaransa Jean-Mattéo Bahoya mwenye miaka 21.
Nicolas Jackson
TOTTENHAM Hotspur inamtaka mshambuliaji wa Chelsea, Nicolas Jackson mwenye umri wa miaka 25, lakini bado haijawasilisha ofa rasmi. Chelsea inamtathmini mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Senegal kwa thamani ya Pauni 65 milioni, baada ya kucheza kwa mkopo Bayern Munich msimu uliopita.
Jadon Sancho
WINGA wa zamani wa Manchester United na timu ya taifa ya England, Jadon Sancho, 26, ana makubaliano ya awali na klabu kadhaa Ulaya, Saudi Arabia na Mashariki ya Kati, huku akiendelea kutathmini machaguo aliyopokea. Hata hivyo, kambi ya mchezaji huyo inadaiwa kumshawishi abaki England.
Pedro Neto
IWAPO Savinho atahamia Tottenham Hotspur, Manchester City inadaiwa itamgeukia winga wa Chelsea na Ureno, Pedro Neto mwenye umri wa miaka 26, huku tayari ikiwa imeanza mawasiliano na kambi yake kuhusu uwezekano wa uhamisho. Neto ni miongoni mwa mastaa bora kabisa katika kikosi cha matajiri wa London.
Pep Chavarria
CHELSEA iko karibu kukamilisha usajili wa beki wa kushoto wa Hispania, Pep Chavarria mwenye umri miaka 28 kutoka Rayo Vallecano, baada ya mchezaji huyo kukubaliana masharti binafsi na klabu hiyo ya London. Hata hivyo, kambi yake pia ilikuwa inafanyia kazi ofa zingine zilizowasilishwa mezani kwao.
Manor Solomon
HULL City iliyopanda Ligi Kuu England msimu uliopita imeingia katika vita na West Ham United iliyoshuka daraja kuwania saini ya winga wa Tottenham hotspur na timu ya taifa ya Israel, Manor Solomon mwenye miaka 27, anayethaminiwa kwa karibu Pauni 20 milioni. Solomon hana namba kikosi cha kwanza cha Spurs.