Arsenal yashinda na kuifikia rekodi ya miaka 122
Muktasari:
- Ushindi huo pia ulikuwa ni mechi ya nane mfululizo bila kuruhusu bao, jambo lililowafanya kufikia rekodi ya klabu iliyowekwa mwaka 1903 katika misimu miwili tofauti.
PRAGUE, CZECH: MIKEL Merino amefunga mabao mawili wakati Arsenal ikiibuka na ushindi mnono wa 0-3 dhidi ya Slavia Prague katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, mechi ikichezwa Fortuna Arena, leo Jumanne Novemba 4, 2025 na kuongeza mfululizo wao wa ushindi hadi mechi nane mfululizo katika mashindano yote.
Ushindi huo pia ulikuwa ni mechi ya nane mfululizo bila kuruhusu bao, jambo lililowafanya kufikia rekodi ya klabu iliyowekwa mwaka 1903 katika misimu miwili tofauti.
Merino alianza kama mshambuliaji wa mwisho kuchukua nafasi ya Viktor Gyökeres aliyekuwa majeruhi, na kama alivyofanya msimu uliopita alipomrithi Kai Havertz, kiungo huyo alionyesha tena uwezo wake wa kucheza nafasi mbalimbali na kutoa mchango muhimu kwa Arsenal.
Bao la kwanza la Arsenal lilipatikana dakika ya 32 baada ya Video Assistant Referee (VAR) kumpa adhabu Lukas Provod kwa kugusa mpira kwa mkono kufuatia kona iliyopigwa na Bukayo Saka kuunganishwa kwa kichwa na Gabriel Magalhaes.
Saka alichukua jukumu la kupiga penalti na kuukwamisha mpira wavuni kwa mkwaju mkali uliokwenda moja kwa moja kwenye kona ya chini ya goli.
The Gunners hawakuwa katika kiwango bora kipindi cha kwanza na walilazimika kukabiliana na kipindi kigumu cha mwanzo, ambapo Provod alipiga shuti pembeni akiwa kwenye nafasi nzuri kwa Slavia Prague.
Lakini kikosi cha Mikel Arteta kilianza kipindi cha pili kwa kasi na kuongeza bao la pili sekunde chache baada ya kuanza, Merino akipiga shuti safi akimalizia krosi ya Leandro Trossard na mpira kujaa wavuni.
Merino aliongeza bao lake la pili dakika ya 68 baada ya kupanda juu na kumalizia kwa kichwa krosi ya Declan Rice, huku kipa wa wenyeji, Jakub Markovic akishindwa kuudhibiti mpira.
Kulikuwa pia na tukio jingine la kihistoria usiku huo, wakati Max Dowman, mwenye umri wa miaka 15 na siku 308, akawa mchezaji mdogo zaidi kuwahi kucheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, baada yakumrithi Trossard, akivunja rekodi ya Youssoufa Moukoko ambaye aliichezea Borussia Dortmund mwaka 2020 akiwa na miaka 16 na siku 18.
Slavia Prague walidhani wamepata penalti dakika 10 za mwishoni mwa mchezo baada ya Provod kuangushwa na Ben White, lakini VAR ilibatilisha uamuzi huo kutokana na mwamuzi kutazama tena tukio hilo kwenye skrini.
Ushindi huo umeendeleza mwanzo mzuri wa msimu kwa vinara wa Ligi Kuu ya England, Arsenal, ambao sasa wamepata ushindi katika mechi nne kati ya nne za Ligi ya Mabingwa huku bila ya kuruhusu bao ikifunga 11, pia wamepanda hadi rekodi ya kutopoteza katika mechi 13 mfululizo katika mashindano yote.