Kisa bao Mourinho amwagia sifa Bellingham
Muktasari:
- Bellingham alianza mchezo huo wa Jumanne akiwa benchi, uamuzi uliofanywa na Mourinho kutokana na ratiba yenye msongamano ya Madrid pamoja na kuwa na wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa kikosini.
MADRID, HISPANIA: KOCHA Jose Mourinho amemsifu kiungo wa Real Madrid, Jude Bellingham akimtaja kuwa bila shaka ndiye kiungo bora zaidi duniani, baada ya nyota huyo kufunga bao la kuvutia lililoibua mabadiliko makubwa katika ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya PSV Eindhoven kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Bellingham alianza mchezo huo wa Jumanne akiwa benchi, uamuzi uliofanywa na Mourinho kutokana na ratiba yenye msongamano ya Madrid pamoja na kuwa na wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa kikosini.
Hata hivyo, baada ya Madrid kwenda mapumziko ikiwa nyuma kwa bao 1-0 dhidi ya PSV, Mourinho aliona umuhimu wa kufanya mabadiliko ili kuimarisha kikosi chake. Hapo ndipo Bellingham alipoingizwa uwanjani.
Akizungumza baada ya mchezo, Mourinho alisema kiungo huyo wa England ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa katika maeneo yote ya mchezo.
“Ni mchezaji wa kipekee mwenye kila kitu. Ana nguvu za kimwili, anauelewa mchezo na ana kila kitu kinachohitajika. Leo amebadilisha kabisa mwelekeo wa mchezo,” alisema Mourinho.
Nahodha Fede Valverde aliisawazishia Madrid dakika ya 50 kabla ya Bellingham kuonyesha ubora wake dakika ya 60 kwa kufunga bao la kuvutia lililoifanya timu hiyo kuongoza.
Akiwa nje kidogo ya eneo la hatari, Bellingham aligusa mpira mara mbili kujiandaa kabla ya kupiga shuti kali la ‘volley’ kwa kutumia sehemu ya nje ya mguu wake wa kulia, lililojaa ufundi na usahihi wa hali ya juu kiasi cha kumwacha kipa wa PSV, Matej Kovar, akiwa hana nafasi ya kuokoa.
Akizungumzia bao hilo, Bellingham alisema hakulitarajia kulifunga kwa namna hiyo, kwani awali alikuwa akitafuta nafasi ya kumpasia mchezaji mwenzake.
“Kwa kweli nilishangaa kidogo. Nilijua ningeweza kuutuliza vizuri mpira na kuumiliki. Lakini kwa kawaida, katika eneo kama lile huwa natafuta kuona kama kuna mchezaji mwenzangu ninayeweza kumpasia.
“Mpira ulipanda vizuri na nikaamua kuupiga. Lilikuwa bao zuri na muhimu kwa timu kwa sababu lilikuwa bao la pili na lilitusaidia kuudhibiti mchezo,” alisema.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 alisherehekea bao hilo kwa mtindo wake wa kawaida, akisimama mbele ya mashabiki wa Madrid huku mikono yake ikiwa imetandazwa, wakati mashabiki hao wakimshangilia kwa wimbo maarufu wa ‘Hey Jude’.
Hilo lilikuwa bao lake la nne katika mechi tano zilizopita alizoichezea Real Madrid.
Alipoulizwa kama anastahili kulinganishwa na gwiji wa Madrid na Ufaransa, Zinedine Zidane, aliyeshinda tuzo ya Ballon d’Or na Kombe la Dunia mwaka 1998, Bellingham alionyesha unyenyekevu akisema nyota huyo bado yuko mbali na kiwango chake.
“Nadhani Zidane ni bora zaidi yangu. Ana ufundi na mvuto mkubwa zaidi katika uchezaji wake, pia ni mwanasoka ninayemkubali sana,” alisema.
SIJALI BALLON D’OR
Katika mchezo huo, Kylian Mbappe alifunga mabao mawili huku Vinicius Junior akifunga bao la tano na kukamilisha ushindi huo mkubwa, baada ya Madrid kuanza kwa kusuasua kipindi cha kwanza.
Alipoulizwa kama kwa sasa anacheza soka bora zaidi katika maisha yake, Bellingham alisema kwake jambo muhimu ni kuendelea kufanya vizuri katika mechi zinazofuata badala ya kutegemea mafanikio ya mchezo uliopita.
“Nadhani kiwango chako hupimwa kwa mchezo unaofuata. Ulichofanya katika mchezo uliopita hakina umuhimu mkubwa. Kwa sasa ninapaswa kuelekeza nguvu zangu katika maandalizi ya mchezo unaofuata.
“Kufikiria kuhusu kiwango changu bora au kuwa mchezaji bora duniani hakunipi maana yoyote,” alisema.
Bellingham aliongeza kuwa uwezo wa timu kubadilika na kupandisha kiwango hata inapokuwa haichezi vizuri ndiyo unaotofautisha timu kubwa na nyingine.
“Tunaendelea kuonyesha ile mentality ya timu nzuri, kwamba hata kama huchezi vizuri, unaweza kubadilisha kiwango chako wakati wowote,” alisema.
Mbali na mafanikio yake uwanjani, Bellingham pia amekuwa akizoea maisha nchini Hispania, jambo alilodai limemsaidia kukua kisoka na nje ya uwanja.
Akizungumzia uwezo wake wa kuzungumza Kihispania, kiungo huyo alikiri bado huwa na wasiwasi anapozungumza lugha hiyo mbele ya watu, ingawa amekuwa akiimarika kadiri muda unavyokwenda.
“Naendelea kuboresha uwezo wangu. Huwa naingiwa na wasiwasi kidogo ninapozungumza nanyi, lakini ni rahisi zaidi ninapokuwa kwenye vyumba vya kubadilishia nguo,” alisema kwa utani.