Bellingham mambo safi Madrid
Muktasari:
- Madrid imekuwa na nia ya kumwongezea mkataba kiungo huyo kutokana na mchango wake mkubwa tangu alipojiunga na klabu hiyo.
MADRID, HISPANIA: KIUNGO wa Real Madrid na timu ya taifa ya England, Jude Bellingham, anakaribia kusaini mkataba mpya wa miaka mitano utakaomfanya kuwa miongoni mwa wachezaji wanaolipwa fedha nyingi zaidi barani Ulaya.
Madrid imekuwa na nia ya kumwongezea mkataba kiungo huyo kutokana na mchango wake mkubwa tangu alipojiunga na klabu hiyo.
Mazungumzo ya kuongeza mkataba yalianza Septemba mwaka huu, huku pande hizo zikilenga kuongeza muda wa kuitumikia klabu hiyo hadi mwaka 2031.
Kwa mujibu wa taarifa, mazungumzo yanaendelea vizuri na viongozi wa Madrid wana matumaini ya kukamilisha dili hilo hivi karibuni.
Bellingham, ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2029, anatarajiwa kuongezewa maslahi yatakayomfanya kulingana na mshahara anaolipwa nyota mwenzake Vinicius Junior.
Vinicius alisaini mkataba mpya msimu uliopita unaoripotiwa kumwezesha kupata pauni 500,000 (zaidi ya Sh1 bilioni) kwa wiki baada ya makato ya kodi.
Hata hivyo, Kylian Mbappe ndiye anayeendelea kuwa mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi ndani ya kikosi hicho.
Real Madrid pia inaendelea na mazungumzo ya mikataba mipya kwa kiungo Fede Valverde, wakati tayari imeongeza mikataba ya nyota Arda Guler na Aurelien Tchouameni hadi mwaka 2032.
Bellingham, mwenye umri wa miaka 23, amekuwa katika kiwango kizuri na kocha Jose Mourinho hivi karibuni alimwelezea kuwa mchezaji wa aina yake.
Kiungo huyo amefunga mabao sita msimu huu, huku kukiwa na uwezekano wa kupumzishwa katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya PSV Eindhoven.
Akizungumzia mchango wake, kipa wa Madrid, Thibaut Courtois, amesema Bellingham ni mchezaji mwenye kiu kubwa ya ushindi na tabia ya kuhamasisha wenzake.
"Jude anataka kushinda kila kitu. Ni mshindani wa kweli na anapokuwa hafurahishwi na jambo fulani, utaona wazi. Pia ni kiongozi uwanjani," alisema Courtois.
Aliongeza kuwa Bellingham ana uwezo mkubwa wa kukimbia na kucheza kwa nguvu kwa muda mrefu bila kuchoka.
"Unapomtazama uwanjani, unaweza kudhani ana umri mkubwa zaidi. Ana nguvu nyingi na ni vigumu kumpokonya mpira. Akiwa katika kiwango chake, tunacheza vizuri zaidi," alisema.
WACHEZAJI WANAOLIPWA FEDHA NYINGI ULAYA
Erling Haaland (Manchester City) – Pauni 510,000.
Kylian Mbappe (Real Madrid) – Pauni 503,000.
Vinicius Junior (Real Madrid) – Pauni 500,000.
Harry Kane (Bayern Munich) – Pauni 402,000.
Virgil van Dijk (Liverpool) – Pauni 350,000.