Pauni 128 Milioni zamvutia Vinicius Emirates
Muktasari:
- Mabingwa hao wa Ligi Kuu England wanataka kuongeza makali kwenye safu yao ya ushambuliaji kwa kumsajili winga huyo wa Brazil, ambaye amebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake na Real Madrid.
LONDON, England: ARSENAL ipo tayari kuingia katika historia ya Ligi Kuu England kwa kuvunja rekodi ya usajili ili kuinasa saini ya nyota wa Real Madrid, Vinicius Jr, huku dili hilo likitajwa kugharimu zaidi ya Pauni 128milioni.
Mabingwa hao wa Ligi Kuu England wanataka kuongeza makali kwenye safu yao ya ushambuliaji kwa kumsajili winga huyo wa Brazil, ambaye amebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake na Real Madrid.
Kwa mujibu wa taarifa, Vinicius anayelipwa karibu Pauni15 milioni kwa mwaka, anataka mkataba mpya wenye thamani ya zaidi ya Pauni25 milioni kwa mwaka, akiamini anastahili malipo makubwa kutokana na mchango wake kwa mafanikio ya klabu hiyo.
Hata hivyo, Real Madrid inadaiwa kumwekea mezani ofa ya karibu Pauni 19milioni kwa mwaka na haipo tayari kuongeza zaidi ya kiwango hicho, jambo linaloongeza uwezekano wa nyota huyo kutafuta changamoto mpya.
ARSENAL TAYARI KUVUNJA REKODI
Ripoti zinaeleza kuwa Real Madrid itahitaji ofa ya takribani Pauni 128 milioni ili kumuuza Vinicius.
Iwapo Arsenal itatoa kiasi hicho, itavunja rekodi ya usajili wa ghali zaidi katika historia ya England, ambayo kwa sasa inashikiliwa na Liverpool baada ya kumsajili Alexander Isak kwa Pauni125 milioni.
Mbali na ada ya usajili, Arsenal pia italazimika kuvunja mfumo wake wa mishahara ili kumshawishi Vinicius kutua Emirates.
Inaelezwa kuwa viongozi wa klabu hiyo wako tayari kumfanya Mbrazil huyo kuwa mchezaji anayelipwa zaidi katika historia ya Premier League, akizidi mshahara wa Bukayo Saka wa Pauni 350,000 kwa wiki na hata ule wa Erling Haaland, unaoripotiwa kufikia Pauni 525,000 kwa wiki.
BRUNO GUIMARAES BADO KWENYE RADA
Wakati huo huo, Arsenal inaendelea na mazungumzo ya kumsajili nahodha wa Newcastle United, Bruno Guimaraes.
Taarifa zinaeleza kuwa klabu hizo zimekaribia kufikia makubaliano ya ada ya Pauni 80milioni, huku masuala ya maslahi binafsi ya kiungo huyo wa Brazil yakielezwa kutokuwa kikwazo.
Iwapo dili zote mbili zitakamilika, Arsenal itakuwa imetuma ujumbe mzito kwa wapinzani wake kuwa ina nia ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu na kufanya vizuri zaidi katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.