Rashford aikataa Man United, asisitiza kubaki Barcelona
Muktasari:
- Rashford alijiunga na Barcelona kwa mkopo kutoka Manchester United katika usajili wa majira ya kiangazi msimu huu, na miamba hiyo ya Catalunya ina chaguo la kumsajili moja kwa moja msimu ujao.
Mshambuliaji Marcus Rashford ameweka wazi kwamba anataka kuondoka kabisa Manchester United na kubaki Barcelona baada ya msimu huu kumalizika.
Rashford alijiunga na Barcelona kwa mkopo kutoka Manchester United katika usajili wa majira ya kiangazi msimu huu, na miamba hiyo ya Catalunya ina chaguo la kumsajili moja kwa moja msimu ujao.
Akiwa tayari amefunga mabao matano katika mechi 12, mashambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 27, ameweka wazi mustakabali wake kabla ya pambano kubwa la El Clásico dhidi ya Real Madrid litakalopigwa keshokutwa Jumapili, Oktoba 26, 2025.
Alipoulizwa na ESPN kama anataka kubaki Barcelona, Rashford amesema: “Ndiyo, bila shaka. Ninafurahia kuwa katika klabu hii na naamini kwa yeyote anayependa soka aneipenda klabu hii. Barcelona ni moja ya klabu muhimu katika historia ya mchezo huu. Kwa mchezaji, ni heshima kubwa kucheza hapa.”
Rashford bado ana mkataba na Manchester United hadi mwaka 2028, lakini baada ya kusajiliwa kwa mkopo, inaonekana wazi kwamba hatarudi Old Trafford chini ya kocha wa sasa Rúben Amorim.
“Watu wanasahau hili, lakini miaka 23 au 24 ya maisha yangu yote nimekuwa Manchester United, kwa hiyo wakati mwingine unahitaji mabadiliko. Nafikiri labda ndivyo ilivyo kwangu, na ninafurahia kila kitu.” ameongeza.