Rais Trump ndani fainali NBA
Muktasari:
- Fainali za NBA si tukio la kwanza kubwa la michezo ambalo Trump amehudhuria. Alihudhuria Super Bowl LIX, mashindano ya tenisi ya US Open mwaka 2025, na pia mchezo wa ubingwa wa College Football Playoff mwezi Januari mwaka huo.
SAN ANTONIO, MAREKANI: KWA MARA ya kwanza rais Marekani aliye madarakani atakuwepo uwanjani kushuhudia mchezo wa tatu wa fainali ya Ligi ya Kikapu ya NBA kati ya New York Knicks dhidi ya San Antonio Spurs.
Hiyo ni baada ya Rais Donald Trump kuthibitisha kuwa anapanga kuhudhuria fainali hiyo baada ya kualikwa na mmiliki na gavana wa timu ya Knicks, James Dolan.
Trump, ambaye kwa muda mrefu amekuwa shabiki wa New York Knicks, amesema anapanga kuhudhuria angalau mchezo mmoja wa Fainali za NBA katika ukumbi wa Madison Square Garden wiki ijayo kufuatia mwaliko kutoka kwa mmiliki wa timu hiyo.
Akijieleza kama “shabiki mkubwa” wa Knicks na James Dolan, Trump amesema atakuwepo ukumbini kwa angalau mchezo mmoja wiki ijayo. NBA inaamini kuwa tukio hilo litamfanya kuwa rais wa kwanza kuhudhuria mchezo wa Fainali za NBA.
“Jibu ni ndiyo, amenialika na ninaenda,” Trump amesema kuhusu mwaliko wa Dolan. Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ya Oval, amesema analenga kuhudhuria fainali itakayochezwa Jumatatu, lakini hakukataa uwezekano wa kuhudhuria mchezo wa nne siku ya Jumatano.
“Labda nitahudhuria yote mawili,” amesema Trump.
Trump, ambaye kwa sasa anakabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo vita nchini Iran, mvutano ndani ya Bunge la Marekani na uchaguzi wa katikati ya muhula unaokaribia, amesema alihakikisha ameangalia sehemu ya Mchezo wa kwanza Jumatano iliyopita, ambapo New York Knicks walishinda San Antonio Spurs na kuongoza mfululizo huo kwa ushindi wa 1-0.
“Nilikosa sehemu ya katikati ya mchezo kwa sababu siku hizi ninazungumza na majenerali usiku kucha, lakini niliangalia mwisho wa mchezo na walikuwa bora sana,” Trump amesema na kuongeza kuwa “Ilikuwa ya kushangaza kweli.”
Awali Kamishna wa NBA, Adam Silver, amesema jana kuwa Trump “anakaribishwa” kuhudhuria mchezo huo. Bila shaka Rais anakaribishwa kuhudhuria Mchezo wa fainali ya tatu,” Silver amesema katika hafla ya NBA Cares. “Rais huyu, Donald Trump, hata kabla hajaingia kwenye siasa, alikuwa shabiki mkubwa wa Knicks.”
Silver amewahi kuzungumzia uwezo wa michezo kuwaleta watu pamoja licha ya tofauti zao, na anaona tukio hili kama fursa nyingine ya aina hiyo.
“Nadhani michezo, hasa, ni jambo linalotuwezesha kuangazia yale tunayofanana badala ya yale yanayotutenganisha. Inaleta hisia ya umoja na kuwa sehemu ya jamii,” amesema Silver.
“Tunaona hali hiyo New York, na naamini Trump ni mtu wa New York kwa kiasi kikubwa. Ninafurahi kuona New Yorker mwingine akishiriki katika shauku na furaha inayozunguka timu hii ya Knicks.”
Fainali za NBA si tukio la kwanza kubwa la michezo ambalo Trump amehudhuria. Alihudhuria Super Bowl LIX, mashindano ya tenisi ya US Open mwaka 2025, na pia mchezo wa ubingwa wa College Football Playoff mwezi Januari mwaka huo.