Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Pochettino atajwa mbadala wa Carrick

POCHE Pict

Muktasari:

  • Matokeo hayo yameifanya timu hiyo kuwa na ushindi mara mbili pekee katika mechi 10 za Ligi Kuu England msimu huu, hali inayotajwa kuwa mwanzo mbaya zaidi wa United tangu Sir Alex Ferguson alipochukua mikoba ya Ron Atkinson miaka 40 iliyopita.

LONDON, ENGLAND: MUSTAKABALI  wa kocha wa Manchester United, Michael Carrick, umeendelea kuwa shakani baada ya uongozi wa klabu hiyo kuanza kutafakari uwezekano wa kumtimua na kumleta kocha mpya wakati wa mapumziko ya mechi za kimataifa.

Carrick amekuwa katika wakati mgumu kufuatia matokeo yasiyoridhisha yaliyosababisha Manchester United kushuka hadi eneo la kushuka daraja, licha ya kutoka sare ya mabao 4-4 dhidi ya Aston Villa katika Uwanja wa Old Trafford, Jumapili.

Matokeo hayo yameifanya timu hiyo kuwa na ushindi mara mbili pekee katika mechi 10 za Ligi Kuu England msimu huu, hali inayotajwa kuwa mwanzo mbaya zaidi wa United tangu Sir Alex Ferguson alipochukua mikoba ya Ron Atkinson miaka 40 iliyopita.

POCH 01

Jina la Mauricio Pochettino limeibuka kwa kasi kama mgombea anayepewa nafasi kubwa ya kuchukua nafasi ya Carrick

 Pochettino kwa sasa anaifundisha timu ya taifa ya Marekani, lakini mkataba wake una kipengele kinachoruhusu kuvunja mkataba kwa fidia ya pauni milioni saba.

Makocha wengine wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ni Eddie Howe na Julian Nagelsmann, ambao pia walikuwa kwenye orodha ya wanaofikiriwa na United kabla ya klabu hiyo kuamua kumpa Carrick muda zaidi wa kurekebisha mwenendo wa timu.

Katika mechi tatu zilizopita, United ilipoteza dhidi ya Chelsea, kisha kufanya maajabu kwa kuibuka na ushindi dhidi ya Roma katika Ligi ya Mabingwa Ulaya kabla ya kutoka sare na Aston Villa.

POCH 02

Pamoja na hali hiyo, bado hakuna uamuzi wa mwisho uliotolewa kuhusu hatma ya Carrick, ingawa matarajio ndani ya Old Trafford ni kuwa huenda kocha mpya akawa ameshachukua nafasi hiyo kabla ya mchezo dhidi ya Liverpool utakaopigwa Anfield.

Carrick alichukua nafasi ya Ruben Amorim katikati ya Januari na baadaye kupewa mkataba wa miaka miwili mwezi Mei baada ya kuiongoza United kumaliza nafasi ya tatu na kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Katika kipindi hicho alishinda mechi 15 kati ya 17 alizokuwa akiiongoza timu hiyo.

Hata hivyo, msimu huu mambo yamekuwa tofauti kabisa, huku ushindi wake pekee katika mechi 15 za mashindano yote ukiwa dhidi ya Ipswich na Sabah ya Azerbaijan.

Akizungumzia uwezekano wa kujiuzulu baada ya sare dhidi ya Aston Villa, Carrick alisisitiza kuwa hana mpango huo.

POCH 03

“Hilo halitatokea. Tupo Novemba. Sipendi hali tuliyopo wala nafasi tuliyofikia, lakini tunaweza kubadilisha mambo. Najua tunachotakiwa kufanya kama klabu, na jambo muhimu ni kushinda mechi,” amesema.

Iwapo Carrick atatimuliwa, Manchester United itakuwa inatafuta kocha wake wa nane wa kudumu tangu Sir Alex Ferguson alipostaafu miaka 13 na nusu iliyopita.

Pochettino ana uzoefu mkubwa wa Ligi Kuu England baada ya kuifundisha Tottenham, Chelsea na Southampton, huku pia akiwa na uzoefu wa kuiongoza Paris Saint-Germain.

Kwa upande wa Howe, ambaye aliwahi kuwa kocha wa Newcastle, inadaiwa United haijafanya mawasiliano naye hadi sasa. Kumchukua kungeigharimu klabu hiyo takribani pauni milioni tatu kama fidia.

Nagelsmann naye anatajwa kuwa chaguo jingine baada ya kuondoka kwenye nafasi ya ukocha wa timu ya taifa ya Ujerumani.

Sasa macho yote yanaelekezwa Old Trafford, huku mashabiki wakisubiri kuona kama Carrick ataendelea kupewa nafasi au atakuwa kocha mwingine wa kuondoka katika kipindi kigumu cha United.