Man United yamgeuzia kibao Carrick ikipanga kumfukuza
Muktasari:
- Uamuzi wa Manchester United kuachana na Michael Carrick umekuja siku 15 tangu ilipopanga kubaki naye baada ya kichapo cha mabao 3-0 nyumbani na Bournemouth.
Manchester, England. Manchester United imepanga kubadili msimamo wake juu ya Meneja Michael Carrick na sasa inataka kumtimua kutokana na mwenendo usioridhisha wa timu hiyo.
Inaripotiwa kwamba Mtendaji Mkuu wa Klabu hiyo, Omar Berrada na Mkurugenzi wa Soka, Jason Wilcox wamepanga kukutana na mwekezaji mdogo wa klabu hiyo, Sir Jim Ratcliffe na kumpa mapendekezo ya kumtimua Carrick.
Sare ya mabao 4-4 nyumbani dhidi ya Aston Villa, Jumapili iliyopita, ilipelekea Man United kushuka hadi katika nafasi ya 18 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England (EPL).
Ilikuwa ni mechi ya tatu tangu uongozi wa Man United uamue kumpa muda Carrick baada ya kichapo cha mabao 3-0 nyumbani dhidi ya Bournemouth, Oktoba 25.
Tangu hapo Man United imecheza mechi tatu, ambapo imepata ushindi mara moja, imetoka sare moja na imepoteza mchezo mmoja.
Ilitegemewa kwamba kipindi cha mapumziko cha wiki mbili kupisha mechi za timu za taifa kingekuwa muhimu kwa Carrick kufanya tathmini ya kikosi na kujiunda upya ili kuhakikisha timu hiyo inarudi kwenye mstari.
Hata hivyo mambo yamekuwa ni tofauti na ndio uongozi wa Man United unaona ni sahihi kumuweka kando kiungo wao huyo wa zamani.
Meneja wa zamani wa Newcastle United, Eddie Howe ni miongoni mwa makocha wanaopewa nafasi kubwa ya kuchukua mikoba ya Carrick.
Howe kwa sasa hana timu anayofundisha tangu alipoachana na Newcastle United baada ya msimu uliopita kumalizika.
Pia Meneja wa zamani wa Chelsea, Antonio Conte amekuwa akitajwa katika orodha ya wanaotazamwa kukabidhiwa jukumu hilo.
Yupo pia Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Marekani, Mauricio Pochettino.