Ulaya ilifunga na ladha zotezote
Muktasari:
- Mechi za ligi nchini Hispania zilianza kwa heshima maalumu kwa mshambuliaji wa Tenerife, hayati Jesus de Miguel, aliyefariki dunia baada ya mchezo wa Daraja la Pili, Jumatatu.
MADRID, HISPANIA: KIUNGO wa kimataifa wa Hispania, Fermin Lopez, aliibuka kuwa mhimili muhimu katika mchezo muhimu akiisaidia Barcelona inayoongoza Ligi Kuu Hispania (LaLiga), kutoka nyuma na kupata ushindi wa mabao 2-1 ugenini dhidi ya Atletico Madrid, mwishoni mwa wiki.
Mechi za ligi nchini Hispania zilianza kwa heshima maalumu kwa mshambuliaji wa Tenerife, hayati Jesus de Miguel, aliyefariki dunia baada ya mchezo wa Daraja la Pili, Jumatatu.
Nako nchini Italia, mwenendo usioridhisha wa Napoli uliendelea baada ya kutoka sare ya bao 1-1 nyumbani dhidi ya Lazio, matokeo yaliyoimarisha nafasi ya timu hiyo ya ugenini kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu (Serie A).
NAPOLI ISIYO NA NGUVU
Mshambuliaji wa Lazio, Davide Frattesi, aliifungia timu yake bao la kwanza dakika ya 28 baada ya Tijjani Noslin, aliyekuwa upande wa kushoto kumpa pasi akiwa anatazamana na safu ya ulinzi ya Napoli iliyoonekana legelege.
Mashabiki wa wenyeji walionyesha wazi hasira, lakini walishuhudia timu yao ikirejea mchezoni na kusawazisha kupitia bao la kujifunga la Alfonso Pedraza baada ya mapumziko. Bao hilo liliinusuru Napoli na kipigo cha tatu mfululizo. Hata hivyo, kocha Massimiliano Allegri ataendelea kukabiliwa na presha kutokana na timu yake kupata ushindi mara nne na sare tatu katika mechi 11 za Serie A ilizocheza hadi sasa.
Lazio, ambayo iliendelea kutopoteza pamoja na wapinzani wao wa mjini, Roma, wakiwa pointi mbili nyuma, ilibaki kileleni kwa tofauti ya pointi moja dhidi ya Inter Milan, iliyoshinda 2-0 dhidi ya Como. Pio Esposito aliipa Inter bao la kuongoza kabla ya Marcus Thuram kuongeza la pili dakika ya 19. Kipigo hicho kilikatiza mfululizo wa ushindi wa Como katika mechi sita za mashindano yote.
Juventus ilitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Fiorentina katika Derby d’Italia, huku Christian Pulisic akiifungia AC Milan bao katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Genoa. Bao la Nikola Krstovic liliitosha Atalanta kuichapa Monza 1-0 ugenini.
FERMIN NA NYOTA YAKE
Fermin, mwenye umri wa miaka 23, aling'ara katika mchezo uliokutanisha timu yenye safu bora zaidi ya ushambuliaji na ile yenye safu bora zaidi ya ulinzi katika La Liga.
Atletico, iliyokuwa imefungwa mabao manane pekee kabla ya mchezo huo, ilitawala mwanzoni na kupata bao kupitia Giuliano Simeone.
Barcelona ilipata wakati mgumu kupenya safu ya ulinzi ya Atletico iliyokuwa imejipanga vizuri hadi Fermin aliposawazisha kwa shuti la kupinda la mguu wa kushoto lililojaa kwa usahihi kabla ya mapumziko.
Fermin alikamilisha ushindi huo wa kurejea mchezoni dakika ya 66 baada ya Lamine Yamal kumpa pasi ndani ya eneo la hatari, nyuma ya safu ya ulinzi ya Atletico. Ushindi huo uliifanya Barcelona kuendelea kuongoza ligi ikiwa na pointi tatu zaidi ya Real Madrid. Atletico inashika nafasi ya tatu, ikiwa na pointi tano nyuma ya Barcelona.
Awali, katika mechi nyingine mwamuzi Cesar Soto Grado alisimamisha mchezo wa La Liga kati ya Real Betis na Elche dakika ya tisa ili mashabiki, wachezaji, wafanyakazi wa timu na maofisa wa mchezo kutoa heshima kwa De Miguel, aliyefariki baada ya kugongana na mchezaji mwenzake uwanjani wakati wa mechi ya Tenerife Jumatatu.
Heshima kama hiyo ilitolewa dakika ya tisa katika mechi zote za ligi ya Hispania mwishoni mwa wiki iliyopita, kwa kuwa De Miguel alikuwa akivaa jezi namba tisa. Kifo chake pia kilikumbukwa katika matukio ya heshima kabla ya michezo kuanza.
Mabao ya dakika za mwisho yaliyofungwa na Rodrigo Riquelme na Marc Bartra yaliipa Betis ushindi wa 2-0 na kuimarisha nafasi yake ya nne.
LEVERKUSEN YAPUMUA
Patrik Schick, aliihakikishia Bayer Leverkusen ushindi wa mabao 2-1 katika mchezo wa dabi ndogo ya Rhine dhidi ya Cologne kwa kufunga bao la dakika za mwisho, kabla ya nyota wa Cologne, Said El Mala, kurejesha msisimko kwa kufunga katika muda wa nyongeza.
Ushindi huo utampa nafuu kocha wa Leverkusen, Carles Martínez, baada ya timu yake kupoteza mechi mbili mfululizo nyumbani. Nayo Freiburg, inayoendelea kufanya vizuri, iliichapa Union Berlin inayosuasua mabao 2-0.
LILLE YAENDELEA KUIVUTA PSG
Supastaa Nathan Ngoy alifunga bao la ushindi na kuipa Lille ushindi wa mabao 2-1 ugenini dhidi ya Rennes katika Ligi Kuu Ufaransa (Ligue 1), ikiendelea kuweka presha kwa PSG inayoongoza. Lille iko nyuma kwa pointi mbili dhidi ya mabingwa watetezi, PSG, baada ya raundi 10 za ligi.
Naye mshambuliaji Keyliane Abdallah aliifungia Marseille bao la ushindi katika ushindi wa mabao 2-1 ugenini dhidi ya Lens, matokeo yaliyoipandisha Marseille hadi nafasi ya nne, ikiwa na pointi tano nyuma ya PSG.
Kwingineno, Monaco ilipoteza pointi katika muda wa nyongeza baada ya kutoka sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya Le Mans.