Mtego wa mbio EPL vs matokeo uwanjani
Muktasari:
- Mathalan, katika Ligi Kuu England, Manchester United ilipoteza pointi baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Tottenham Hotspur, na wakosoaji hawakupoteza muda kuhoji juhudi na kujituma kwa wachezaji, wakitumia takwimu za kimwili za timu hiyo kuunga mkono hoja zao.
LIVERPOOL, ENGLAND: HUKO Ulaya kuna mambo mengi linapokuja suala la takwimu katika soka; siku hizi umbali wa kukimbia wa timu hufuatiliwa zaidi kwa vifaa vya kisasa vya kiteknolojia kama viashiria vya timu ama kufanya vizuri au vibaya. Hata hivyo, kuna ushahidi mdogo unaoonyesha kwamba kukimbia umbali mrefu zaidi kunamaanisha kuwa ni timu bora muda mrefu.
Mathalan, katika Ligi Kuu England, Manchester United ilipoteza pointi baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Tottenham Hotspur, na wakosoaji hawakupoteza muda kuhoji juhudi na kujituma kwa wachezaji, wakitumia takwimu za kimwili za timu hiyo kuunga mkono hoja zao.
Kiungo wa zamani wa Tottenham, Jamie Redknapp, ambaye alikuwa mchambuzi wa Sky Sports, alisema: “Kuna mwenendo ambao siupendi ninapozitazama timu, nao ni pale ambapo timu pinzani inakimbia zaidi yako, na takwimu hazidanganyi. Katika Ligi Kuu England kwa sasa, nahisi kuna mambo kadhaa ambayo hayawezi kujadiliwa; lazima ukimbie zaidi ya timu pinzani ikiwa unataka kushinda, au angalau ukaribie kiasi kwamba tofauti hiyo isiwe kubwa sana. Jumamosi (wiki iliyopita), Tottenham ilikimbia kilomita tano zaidi ya Man Utd.”
Takwimu za kimwili kama umbali uliokimbizwa na idadi ya mbio za kasi zinazidi kupatikana kwa urahisi katika soka la kisasa. Kwa kuwa siyo vigumu sana kuzielewa kwa ujumla, ni jambo linaloeleweka kwamba zinaweza kutumiwa na watu wengi. Na ndivyo ilivyo. Katika wiki za hivi karibuni, huenda mashabiki wa Man Utd wamekuwa wakizifahamu zaidi takwimu hizo kuliko mashabiki wa klabu nyingine yoyote.
Imezoeleka kwamba United inaposhindwa kufikia matarajio, wachambuzi, watangazaji, watu maarufu kwenye mitandao ya kijamii na wengine huangalia takwimu za umbali wa kukimbia za timu hiyo wakitafuta maelezo yanayoweza kueleza kila kitu.
Hata hivyo, kwa haki, jambo hilo haliihusu United pekee; Liverpool na Chelsea pia zililengwa na hukumu kama hizo msimu uliopita. Kwa hiyo haimaanishi kwamba kuna aina fulani ya njama dhidi ya timu hiyo. Ni kwamba suala hilo linaonekana kuwa muhimu zaidi kutokana na mijadala inayozunguka kikosi hicho cha Michael Carrick mara kwa mara.
Lakini je, ni haki kufanya hivyo? Kuna uhusiano wa kiwango gani kati ya timu kukimbia umbali mrefu na kufanya vizuri? Ingawa takwimu zinaweza kuonekana rahisi kwa mtazamo kujibu swali hilo siyo jambo rahisi. Huenda hilo linaonyesha jinsi takwimu hizo zilivyo na maana nyingi katika mchezo wa timu kiasi kwamba siyo busara kutoa uzito mkubwa kwa jumla ya takwimu pekee. Hata hivyo, hili ni swali linalostahili kuangaliwa kwa kina.
Njia ya kwanza ya kutathmini suala hilo ni kulinganisha msimamo wa Ligi Kuu England na orodha ya timu kwa umbali wa kukimbia pamoja na umbali uliokimbizwa kwa kasi kubwa. Ni kweli kwamba njia hiyo ni rahisi na ya awali, lakini ni mwanzo mzuri wa kuangaliwa.
NAMBA SASA
Kama inavyoonekana katika takwimu zilizo hapa chini, msimamo wa Ligi Kuu England wa msimu uliopita hauendani sana na orodha ya timu kulingana na umbali wa jumla uliokimbizwa au umbali wa kukimbizwa kwa kasi kubwa kwa kila mchezo. Ni kweli kwamba Arsenal na Manchester City zilikuwa juu katika takwimu za umbali wa jumla, lakini timu zilizomaliza nafasi ya tatu hadi ya nane zilikuwa na takwimu za wastani tu, au hata chini ya hapo.
Timu zilizomaliza katika 10 bora zilikimbia wastani wa kilomita 4,363 kwa msimu mzima, huku zilizomaliza katika 10 za mwisho zikikimbia wastani wa kilomita 4,332. Kwa kuangalia picha nzima, tofauti ya kilomita 31 kati ya wastani huo ni ndogo sana. Vilevile, kuna tofauti ndogo kati ya wastani wa umbali uliokimbizwa kwa kasi kubwa na timu zilizomaliza katika 10 bora, ambao ulikuwa kilomita 338.7, na zile zilizomaliza katika 10 za mwisho, zilizokuwa na wastani wa kilomita 328.4. Hata hivyo, tunazungumzia ongezeko la asilimia 3.0 pekee.
Hali ni hiyo hiyo unapoangalia takwimu za msimu huu; ni vigumu kuona uhusiano mkubwa. Hata hivyo, kulinganisha takwimu hizo na msimamo wa ligi hakuzingatii ukweli kwamba mafanikio hupimwa kwa kuzingatia matarajio. Bila shaka, Burnley haikutarajiwa kumaliza katika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi kwa sababu tu ilishika nafasi ya saba katika orodha ya timu zilizokimbia umbali mrefu zaidi.
Badala yake, unaweza kutumia utabiri mbalimbali ukiwamo wa Opta uliofanywa kabla ya msimu kuanza ili kupata picha ya timu zilizofanya vizuri, au angalau zilizofikia matarajio, na kubaini kama kulikuwa na mwenendo wa timu zilizozidi matarajio pia kukimbia zaidi ya nyingine.
Msimu uliopita, kulikuwa na timu 10 katika Ligi Kuu England zilizomaliza angalau nafasi moja juu ya nafasi iliyotabiriwa kuwa ndiyo ambayo zingemaliza nayo kwa uwezekano mkubwa, kulingana na Opta kabla ya msimu kuanza. Timu hizo zilikimbia wastani wa kilomita 4,369 katika msimu mzima.
Kwa upande mwingine, timu tisa zilizomaliza angalau nafasi moja chini ya nafasi iliyotabiriwa kuwa zingemalizia zilikuwa na wastani wa kilomita 4,308. Kwa hiyo, tena kuna tofauti, lakini ni ndogo sana; ongezeko la asilimia 1.4 tu kwa kundi la timu zilizozidi matarajio.
Hata hivyo, Sunderland, iliyozidi matarajio kwa nafasi 13, na Man Utd iliyozidi matarajio kwa nafasi tisa hazikuwa katika 10 bora kwa umbali wa kukimbia, licha ya kuwa timu zilizozidi utabiri kwa kiwango kikubwa zaidi kuliko nyingine zote. Crystal Palace iliyomaliza nafasi nane chini ya matarajio, na Newcastle iliyomaliza ya sita chini ya matarajio zilikuwa katika 10 bora kwa umbali wa kukimbia, lakini pia zilikuwa miongoni mwa timu zilizokatisha tamaa zaidi ukilinganisha na matarajio ya kabla ya msimu.
HAPA JE?
Unaweza pia kuangalia pointi zinazotarajiwa. Msimu uliopita, timu zilizokuwa katika nusu ya chini ya orodha ya umbali wa kukimbia zilizidi jumla ya pointi zake zilizotarajiwa kwa wastani wa alama 0.38. Kwa upande mwingine, timu zilizokuwa katika nusu ya juu ya orodha hiyo zilipata pointi chache kwa wastani wa 1.88 kuliko zile zilizotarajiwa kupata.
Kwa kifupi, inaonekana hakuna uhusiano mkubwa kati ya mafanikio ya timu kwa muda mrefu na umbali unaokimbizwa. Hata hivyo, hiyo haimaanishi kwamba hakuna uhusiano wowote katika takwimu zote. Katika takwimu za kimwili msimu wa 2025/26, kipimo kilichoonyesha uhusiano mkubwa zaidi na nafasi za mwisho katika msimamo wa Ligi Kuu England kilikuwa umbali uliokimbizwa wakati timu ikiwa na mpira.
Kipimo hicho siyo kamilifu, lakini kinaashiria kuwepo kwa uhusiano fulani kati ya kukimbia umbali mrefu zaidi timu ikiwa na mpira na kumaliza katika nafasi ya juu zaidi kwenye msimamo wa ligi. Hata hivyo, hilo halimaanishi moja kwa moja kwamba timu fulani ilimaliza juu kwa sababu tu ilikimbia zaidi ikiwa na mpira. Inawezekana kwamba takwimu hizo zinaonyesha timu hiyo ilikuwa na umiliki mkubwa wa mpira kutokana na kuwa na wachezaji bora zaidi. Pamoja na hayo, jambo hilo lilionekana kuwa la kuzingatia.
Lakini, huenda uhusiano mkubwa zaidi kati ya takwimu za kimwili na mafanikio unaonekana katika kiwango cha mchezo mmoja mmoja, badala ya msimu mzima. Tangu mwanzo wa msimu uliopita, kumekuwapo na matukio 86 katika Ligi Kuu England ambapo timu moja ilikimbia angalau kilomita tano chini ya wapinzani wake katika mchezo mmoja.
Katika michezo hiyo 86 timu iliyokimbia angalau kilomita tano chini ya wapinzani wake ilishinda mara 10 pekee. Kati ya ushindi huo, mara saba ilikuwa matokeo yaliyotarajiwa kutokea. Hiyo ni asilimia 11.6 ya ushindi. Hata hivyo, kuna mambo kadhaa ya kuzingatia. Muhimu zaidi, katika michezo 20 kati ya hiyo, angalau timu moja ilikuwa na mchezaji aliyetolewa nje kwa kadi nyekundu. Bila shaka, hali hiyo inaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa kiwango cha shughuli za kimwili za timu zote mbili.
Ukiondoa michezo hiyo 20 unabaki na ushindi mara nane kwa timu zilizokimbia angalau kilomita tano chini ya wapinzani wao katika michezo 66. Hii ina maana kwamba kiwango cha ushindi kinapanda kutoka asilimia 11.6 hadi asilimia kubwa (12.1). Ukiangalia michezo ambayo timu moja ilikimbia kati ya kilomita 2.5 na 4.99 chini ya wapinzani wake, huku ukiondoa michezo iliyokuwa na kadi nyekundu, kiwango cha ushindi kinaongezeka hadi asilimia 25.8. Hata hivyo, kiwango hicho bado siyo kikubwa sana. Kiwango cha kushindwa katika michezo hiyo ni asilimia 46.0.
Hii inaashiria kwamba kuna uhusiano fulani kati ya timu kukimbia zaidi kuliko wapinzani wake na kupata ushindi. Lakini haupaswi kukimbilia hitimisho; hauwezi kuwa na uhakika kamili kwamba umbali wa ziada unaokimbizwa ndio unaoamua matokeo kuliko mambo mengine mengi yanayoweza kuathiri mchezo.
IMEKAAJE KIMWILI?
Takwimu za kimwili pia mara nyingi zinahusiana kwa karibu na mtindo wa uchezaji. Hivyo, kiwango cha shughuli za kimwili cha timu moja katika mchezo kinaweza kuathiri moja kwa moja kiwango cha shughuli za wapinzani wake. Sababu inayowafanya watu wengi kutegemea takwimu hizo huenda ni rahisi kuzielewa na kuzihusisha na juhudi za wachezaji, kwa usahihi au bila usahihi hasa inapozungumziwa timu iliyopoteza mchezo.
Hata hivyo, ukweli kwamba hakuna uhusiano mkubwa kati ya umbali unaokimbizwa katika msimu mzima na mafanikio unaashiria kwamba suluhisho la muda mrefu siyo kuwachosha wachezaji kwa kuwalazimisha kukimbia kupita kiasi. Badala yake, ni kujua wakati sahihi wa kuongeza kasi na nguvu ili kupata matokeo bora zaidi.
Huenda Jurgen Klopp alieleza jambo hili vizuri zaidi mwanzoni kabisa mwa kipindi chake alipokuwa kocha Liverpool.
“Hatuhitaji kukimbia kilomita 115 (kwa kila mchezo) ili kupata mafanikio. Huhitaji kukimbia kama mwendawazimu ukiwa na mpira. Huo ni mwanzo tu. Lazima tujue wakati sahihi wa kuongeza presha; kufikiria vizuri zaidi na kutumia muda sahihi. Lakini ikiwa tunacheza dhidi ya timu iliyo bora zaidi kuliko sisi na hatuko tayari kukimbia zaidi yao, basi sisi ni vichaa,” alisema kocha huyo.
Na Pep Guardiola aliongeza maelezo kuhusu suala hilo katika msimu wake wa mwisho alipokuwa Manchester City.
“Jambo ni kujua wakati wa kukimbia. Kukimbia tu kwa ajili ya kukimbia? Naweza kwenda kwenye uwanja wa riadha na kuwaomba wakimbiaji wa marathoni wakimbie kwa niaba yetu. Suala siyo hilo, bali ni wakati gani unapaswa kufanya hivyo. Msimu uliopita, baadhi ya wachezaji walipokimbia, juhudi zao hazikuwa na manufaa. Jambo muhimu zaidi ni kuunganisha mambo hayo mawili,” alisema Guardiola.
Lakini, ukweli unabaki kuwa mambo yanapokuwa magumu nia ya kujituma huenda ikawa muhimu kuliko kitu kingine chochote machoni pa mashabiki wengi. Kuonekana huna juhudi, hata kama hali halisi ni tofauti ni kosa kubwa kwa timu inayopambana na matokeo mabaya.
Lakini, mara chache sana suluhisho huwa ni “kukimbia zaidi.”