Pep Guardiola kuishuhudia Man City Etihad
Muktasari:
- Guardiola anatarajiwa kuwepo Etihad Jumatano, Oktoba 14, wakati City itakapowakaribisha mabingwa hao watetezi wa Ulaya, katika mchezo ambao utakuwa wa kwanza wa nyumbani tangu klabu hiyo ipatikane na hatia katika sehemu kubwa ya mashtaka 115 ya ukiukaji wa kanuni za kifedha za Ligi Kuu England.
MANCHESTER, ENGLAND: PEP Guardiola anatarajiwa kurejea Uwanja wa Etihad wiki ijayo kushuhudia Manchester City ikikipiga dhidi ya Paris Saint-Germain katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, ikiwa ni mara yake ya kwanza kufika uwanjani hapo tangu kuondoka klabuni hapo mwishoni mwa msimu uliopita.
Guardiola anatarajiwa kuwepo Etihad Jumatano, Oktoba 14, wakati City itakapowakaribisha mabingwa hao watetezi wa Ulaya, katika mchezo ambao utakuwa wa kwanza wa nyumbani tangu klabu hiyo ipatikane na hatia katika sehemu kubwa ya mashtaka 115 ya ukiukaji wa kanuni za kifedha za Ligi Kuu England.
Mapema mwezi huu, tume huru iliibua hukumu dhidi ya City kwa mashtaka yanayohusiana na ukiukaji wa kanuni za fedha za Ligi Kuu England kati ya misimu ya 2009/10 na 2017/18.
City imeendelea kupinga makosa hayo na imewasilisha rufaa dhidi ya uamuzi huo. Kwa mujibu wa ripoti ya Ligi Kuu, klabu hiyo ilidaiwa kuongeza kwa udanganyifu mapato yake ya kibiashara kwa pauni830 milioni kupitia mikataba iliyotajwa kuwa “feki”.
Baada ya hukumu hiyo, Guardiola mwenye umri wa miaka 55 alitoa kauli ya kuiunga mkono City, akisisitiza kuwa ataendelea kuwa upande wa klabu hiyo.
“Natamani kila shabiki wa Manchester City duniani ajue kwamba nipo hapa, zaidi ya wakati mwingine wowote. Nipo na nitaendelea kuwa upande wa klabu yangu, mmiliki wangu, mwenyekiti wangu, Ferran (Soriano), wachezaji, benchi la ufundi, Enzo (Maresca) na ninyi mashabiki wetu wa kipekee.
“Niweke wazi, tutapita katika kipindi hiki pamoja. Nawapenda nyote,” aliandika Guardiola.
City itarejea uwanjani baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa kwa kuvaana na Liverpool Jumapili kwenye Uwanja wa Anfield, kabla ya kuikabili PSG siku nne baadaye Etihad.
Guardiola aliondoka City baada ya kuitumikia kwa miaka 10, kipindi ambacho aliiongoza kutwaa mataji sita ya Ligi Kuu England, likiwamo rekodi ya ubingwa mara nne mfululizo kuanzia msimu wa 2020/21.
Pia alitwaa Ligi ya Mabingwa Ulaya, mataji matatu ya FA Cup na matano ya Kombe la Ligi.
Kabla ya kuondoka, Guardiola aliwahi kuzungumzia mashtaka dhidi ya City Novemba 2024, akisisitiza kuwa angeendelea kubaki klabuni hapo hata kama timu hiyo ingeshushwa daraja.