Pedro Rodriguez atupa taulo
Muktasari:
- Pedro, ambaye amewahi kuzitumikia Barcelona, Chelsea, AS Roma na Lazio, amefunga ukurasa wa maisha yake ya soka akiwa mmoja wa wachezaji waliopata mafanikio makubwa katika kizazi cha dhahabu cha Hispania.
BARCELONA, HISPANIA: MSHAMBULIAJI wa zamani wa Hispania, Pedro Rodriguez, ametangaza kustaafu soka akiwa na miaka 39 baada ya kumaliza safari ya miaka 20 katika mchezo huo.
Pedro, ambaye amewahi kuzitumikia Barcelona, Chelsea, AS Roma na Lazio, amefunga ukurasa wa maisha yake ya soka akiwa mmoja wa wachezaji waliopata mafanikio makubwa katika kizazi cha dhahabu cha Hispania.
Mchezaji huyo alianza kujijenga Barcelona, ambako alipanda kutoka akademi ya klabu hiyo na baadaye kuwa sehemu muhimu ya kikosi kilichokuwa chini ya kocha Pep Guardiola.
Akiwa Barcelona, Pedro alitwaa mataji mbalimbali, ikiwamo Ligi ya Mabingwa Ulaya, Ligi Kuu Hispania na Kombe la Dunia la Klabu.
Aliondoka Barcelona mwaka 2015 na kujiunga na Chelsea ya England, ambako pia alifanikiwa kutwaa Ligi Kuu kabla ya kuendelea na safari yake Italia.
Katika timu ya taifa ya Hispania, Pedro alikuwa sehemu ya kikosi kilichotwaa Kombe la Dunia mwaka 2010 nchini Afrika Kusini.
Miaka miwili baadaye, alishiriki pia katika kikosi cha Hispania kilichotwaa Euro 2012.
Kwa ujumla, Pedro amecheza mechi 794 za klabu, akifunga mabao 197, huku akiwa ameichezea Hispania mara 65 na kufunga mabao 17.
Ametangaza kustaafu akiwa ameshinda mataji 25 makubwa katika kipindi chake cha miaka 20, akiacha alama katika klabu na timu ya taifa.
Uamuzi huo umehitimisha safari ndefu ya mchezaji aliyeshuhudia na kushiriki katika kipindi ambacho Barcelona na Hispania vilitawala soka la dunia.
Pedro sasa anaanza ukurasa mpya wa maisha baada ya kuaga mchezo uliompa mafanikio makubwa katika kipindi chake chote cha uchezaji.