Pambano la Joshua, Fury mambo safi
Muktasari:
- Kwa mujibu wa promota wa masumbwi, Eddie Hearn, mazungumzo ya mwisho kuhusu muda wa kuanza pambano hilo yanaendelea.
MABONDIA Anthony Joshua na Tyson Fury watapanda uliongoni kuzichapa Desemba 11 mwaka huu, katika pambano litakalopigwa kwenye Uwanja wa Manispaa, Cardiff, Wales.
Kwa mujibu wa promota wa masumbwi, Eddie Hearn, mazungumzo ya mwisho kuhusu muda wa kuanza pambano hilo yanaendelea.
Hearn amesema pambano hilo litaanza muda ambao kiu ya wapenzi wa mchezo huo itakatwa, huku akikanusha uwezekano wa kuanza saa za asubuhi.
Hearn amesema suala hilo limehusisha pia mazungumzo na uongozi wa Uwanja wa Principality pamoja na mamlaka za eneo hilo ili kuamua muda unaofaa wa kuanza kwa tukio hilo.
“Watu wanazungumzia pambano kuanza saa 3:00 asubuhi kwa saa za Uingereza? Sidhani kama mtaliona likianza muda huo,” amesema Hearn.
Kwa mujibu wa Hearn, mazungumzo kuhusu muda wa kuanza yanaweza kuwa miongoni mwa sababu zilizochelewesha tangazo rasmi la pambano hilo, huku waandaaji wakitaka kwanza kuhakikisha taratibu zote na makubaliano na mamlaka za eneo hilo zinakamilika.
Joshua na Fury wamekuwa wakihusishwa na pambano hilo kwa miaka kadhaa, huku mazungumzo kati ya kambi zao yakianza, kusimama na kurejea mara kadhaa bila kufikia makubaliano ya mwisho. Hata hivyo, safari hii kuna dalili kwamba pambano hilo linaelekea kufanyika, ingawa bado baadhi ya mambo ya mwisho yanahitaji kukamilishwa kabla ya kutangazwa rasmi.
Moja ya mambo yanayojadiliwa kwa sasa ni muda wa kuanza kwa pambano hilo.
Waandaaji wanatarajiwa kuzingatia muda utakaowezesha pambano kuu kufuatiliwa na mashabiki wengi katika masoko mbalimbali duniani.
Kauli hiyo imekuja baada ya kuwepo kwa matarajio kwamba pambano hilo linaweza kuanza usiku wa manane au mapema sana kutokana na hitaji la kulifikisha kwa watazamaji wa kimataifa katika muda unaofaa.
Awali, kulikuwa na mapendekezo ya pambano hilo kufanyika New York, Marekani. Hata hivyo, Hearn na Joshua walisisitiza kwamba wangependelea pambano hilo lifanyike nchini Uingereza.
Endapo litathibitishwa rasmi, pambano hilo litakuwa moja ya mapambano makubwa zaidi kuwahi kusubiriwa na mashabiki wa ndondi nchini Uingereza, kutokana na historia ndefu ya mazungumzo kati ya Joshua na Fury kuhusu kukutana ulingoni.