Old Trafford hali si shwari… Kuna kikao wiki ijayo!
Muktasari:
- Kwa sasa kocha huyo Mreno bado anapewa sapoti na mabosi wa Old Trafford licha ya kikosi hicho cha Man United kutolewa kwa aibu kwenye Kombe la Ligi na timu ya daraja la chini, Grimsby Town, Jumatano iliyopita.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA Ruben Amorim atakuwa na kikao kizito cha mazungumzo na mabosi wa Manchester United wiki ijayo baada ya kibarua chake huko Old Trafford kuwa kwenye majanga makubwa.
Kwa sasa kocha huyo Mreno bado anapewa sapoti na mabosi wa Old Trafford licha ya kikosi hicho cha Man United kutolewa kwa aibu kwenye Kombe la Ligi na timu ya daraja la chini, Grimsby Town, Jumatano iliyopita.
Lakini, sasa Man United inakabiliwa na mechi kadhaa zijazo ambazo ni ngumu kwelikweli, ikianzia ya nyumbani uwanjani Old Trafford dhidi ya Burnley, Jumamosi kisha itafuatia na mechi za Manchester City na Chelsea baada ya mapumziko ya kupisha mechi za kimataifa.
Na wachezaji waliowaweka kando kwenye kikosi hicho wanafuatilia jambo hilo kwa karibu, kwa sababu bado hawajapata timu za kwenda ili kutoka katika klabu hiyo ya Old Trafford.
Matatizo ya Amorim yanazidi kumzonga, akikabiliwa pia na sakata la kipa mpya, akijaribu kumsaka Senne Lammens wa Antwerp kwa ada ya Pauni 17 milioni huku dirisha la usajili la majira haya ya kiangazi likifungwa Jumatatu.
Kocha Amorim sasa anamtihani wa kuchagua baina ya Andre Onana na Altay Bayindir nani aanze golini kwenye mechi hiyo ya Burnley na wote wamefanya makosa makubwa.
Kocha huyo wa zamani wa Sporting Lisbon hakutaka kuficha kitu baada ya kile kilichomtokea Blundell Park, aliposema baadhi ya wachezaji “walizungumza kwa sauti” kuhusu walichotaka kitokee, akiwa na maana wachezaji hawakucheza kwa ajili ya kocha wao.
Imeleezwa baada ya mechi hiyo, Amorim alitakiwa kufafanua maneno yake yalikuwa na maana gani. Kwenye ule usiku wa mechi, Amorim alisema: “Hii kitu lazima ibadilike, huwezi kubadili wachezaji 22 tena. Ni ngumu kukabiliana na kila kitu.
“Tunahamia kwenye mechi ijayo na baada ya hapo tutakuwa na muda wa kufanya uamuzi. Hebu kwanza kipaumbele chetu kihamie kwenye mechi ijayo kisha tutakuwa na muda wa kuwaza vitu vingine. Tuna kazi ya kufanya, kuandaa na baada ya hapo tutafikiria mambo mengine.”
Mmiliki mwenza wa klabu hiyo, bilionea Jim Ratcliffe na mkurugenzi mtendaji mkuu, Omar Berrada hakuna uhakika kama walikuwapo Blundell Park kwenye mechi hiyo ya hovyo ya Kombe la Ligi, lakini mkurugenzi wa soka, Jason Wilcox alikuwapo.
Kinachoaminia ni Amorim bado anapewa sapoti na mabosi wake baada ya usajili wa Pauni 200 milioni kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi na wanamtazama kocha huyo mwenye umri wa miaka 40 kama mtu wa kuongoza mipango yao ya muda mrefu.
Kuna baadhi ya maswali yanaulizwa endapo kama kocha huyo ataamua kuachia ngazi au ataondolewa baada ya kuiongoza timu hiyo kwa miezi 10 na hakuna mabadiliko yoyote. Amorim alisema baada ya kichapo cha nyumbani mbele ya West Ham United, Mei mwaka huu ataondoka kwenye timu hiyo bila ya kuhitaji kulipwa fidia yoyote endapo kama ataona yeye si mtu sahihi kwenye kuinoa timu hiyo. Kuliripotiwa aliomba kujiuzulu Januari mwaka huu, ikiwa ni miezi mitatu tu tangu alipopewa kibarua hicho, hata hivyo hilo halikuthibitishwa.
Wakati huo huo, wachezaji ambao waliwekwa kando na Amorim kwenye kipindi cha pre-season wameanza kuwa na maswali mengi juu ya hatima ya maisha yao klabuni hapo Old Trafford.
Wachezaji watano wa kikosi cha kwanza Marcus Rashford, Alejandro Garnacho, Antony, Jadon Sancho na Tyrell Malacia, wote wameambiwa watafute timu ya kwenda. Na staa Rashford ameondoka kwenda kujiunga Barcelona kwa mkopo, huku Garnacho akiwa kwenye hatua za mwisho kukamilisha uhamisho wake wa kwenda Chelsea kabla ya dirisha kufungwa Jumatatu.
Kiungo Kobbie Mainoo ameripotiwa kuomba kuondoka kwa mkopo baada ya kuona anawekwa tu benchi, huku ripoti zikidai, Man United imegoma kumruhusu staa huyo aondoke.