Nyota wa Hull City anusurika kifo
Muktasari:
- Thomas, mwenye miaka 27, alipata ajali hiyo jana asubuhi akiwa kwenye gari lake aina ya Land Rover Defender lenye thamani ya Pauni 60,000 (zaidi ya Sh200 milioni), ambalo lilipinduka katikati ya barabara.
LONDON, ENGLAND: WIKI chache baada ya kusajiliwa na Hull City kwa Pauni 10.5milioni (zaidi ya Sh37 bilioni), winga Sorba Thomas amenusurika kwenye ajali mbaya ya gari iliyotokea karibu na uwanja wa mazoezi wa klabu hiyo.
Thomas, mwenye miaka 27, alipata ajali hiyo jana asubuhi akiwa kwenye gari lake aina ya Land Rover Defender lenye thamani ya Pauni 60,000 (zaidi ya Sh200 milioni), ambalo lilipinduka katikati ya barabara.
Cha kushangaza, mchezaji huyo wa kimataifa wa Wales alinusurika bila kupata jeraha lolote, huku klabu hiyo ikithibitisha kuwa alitoka kwenye gari hilo akiwa salama kabisa.
Ajali hiyo imetokea siku chache baada ya diwani wa eneo hilo, Phil Redshaw, kuandika barua kwa uongozi wa Hull City akiomba wachezaji na wafanyakazi wa klabu hiyo kuwa makini zaidi wanapotumia barabara hiyo.
Redshaw, aliyefika eneo la tukio katika Millhouse Woods Lane, amesema kumekuwa na matukio kadhaa ya magari kukaribia kugongana katika barabara hiyo ya makazi, iliyopo karibu na uwanja wa mazoezi wa Hull City uliopo Cottingham.
“Niliandika kwa katibu wa Hull City Jumapili kuwaomba wawatahadharishe wachezaji kuwa makini wanapoendesha kwenye barabara hii kutokana na malalamiko ya wakazi,” amesema Redshaw.
“Nilitaka awakumbushe wafanyakazi wao kuendesha kwa uangalifu zaidi kwa sababu kila msimu wanapata wachezaji wapya.”
Redshaw amesema baadhi ya nyumba za wakazi zipo moja kwa moja pembeni mwa njia hiyo, huku malori yakilazimika kutumia sehemu hiyo ya barabara kupita.
Picha zilizosambaa zilionyesha Land Rover Defender ya Thomas ikiwa imepinduka katikati ya barabara, huku ikiwa na namba maalumu ya usajili.
Mashabiki waliingiwa na hofu walipoona picha hizo, hasa kutokana na ukubwa wa ajali hiyo. Mashuhuda walidai kuliona gari la Thomas likiteleza huku likiwa limeanguka upande wa paa baada ya ajali iliyodaiwa kutokea kwa mwendo mkubwa.
Hata hivyo, Hull City ilitoa taarifa haraka kuthibitisha kuwa Thomas hakuwa ameumia, ikiwa ni saa chache kabla ya timu hiyo kucheza dhidi ya Chelsea kwenye Uwanja wa Stamford Bridge.