Yanga yaitupa nje Gaborone United, Shalulile, Toure waking’aa
Muktasari:
- Ushindi huu unaifanya Yanga kufuzu hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa jumla ya mabao 3-2, baada ya mechi ya kwanza iliyopigwa Septemba 5, 2026, kutoka sare ugenini ya kufungana bao 1-1, jijini, Botswana.
Yanga imetumia vyema faida ya kucheza nyumbani, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, dhidi ya Gaborone United ya Botswana, katika mechi ya marudiano ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika iliyochezwa leo Jumamosi, Septemba 12, 2026.
Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, ilishuhudiwa Yanga ikipata bao la kwanza mapema tu katika dakika ya saba, lililofungwa na mshambuliaji wake nyota, Peter Shalulile, kisha Cheikh Toure akafunga la pili katika dakika ya 84.
Bao la kwanza lilitokana na umaliziaji mzuri wa Shalulile aliyetumia vizuri mpira uliopigwa na Selemani Mwalimu 'Gomez' na kumkuta mfungaji huyo aliyemzidi ujanja kipa wa Gaborone United, Thabo Motswagole na kuujaza mpira wavuni.
Gaborone inayofundishwa na Kocha Mkuu, Sean Connor, ilianza na mkakati wa kutengeneza mashambulizi ya kushtukiza ikiwa ni mpango ilioutumia mechi ya kwanza iliyopigwa Septemba 5, 2026 na kuisha kwa sare ya bao 1-1.
Kwa upande wa Yanga ilianza mechi hiyo kwa kutengeneza mashambulizi ya mara kwa mara yaliyoipeleka hadi dakika 45, za kipindi cha kwanza ikiwa inaongoza kwa bao hilo la Shalulile.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kufanya mabadiliko ya kiufundi ambapo kwa Gaborone iliwatoa, Ambrosius Amseb na nafasi yake ikachukuliwa na Omphile Ramoagi, huku Thabo Maponda akimpisha Lethabo Ogotseng ili kutengeneza uwiano nzuri ya kikosi hicho katika eneo la kujilinda na la ushambuliaji.
Mabadiliko hayo yaliongeza nguvu kwa Gaborone United, iliyokuwa inapambana kwa lengo la kusawazisha bao lililofungwa mapema dakika ya saba na Shalulile.
Kwa upande wa Yanga, ilifanya mabadiliko ya kuwaingiza Albert Kangwanda, Housseine Zakouani, Oumar Komara na Cheikh Toure, huku ikiwatoa Stephane Aziz KI, Peter Shalulile, Mudathir Yahya na Seleman Mwalimu 'Gomez'.
Mabadiliko hayo ya Yanga yalizaa matunda katika dakika ya 84, baada ya Toure kufunga bao la pili na kuongeza presha zaidi kwa timu ya Gaborone United iliyokuwa inapambana kusawazisha.
Hata hivyo, dakika ya 87, Gaborone United ilipata bao la kufutia machozi lililofungwa na Lebogang Ditsele na kurejesha matumaini ya kusawazisha ambayo hayakuweza pia kufanikiwa.
Ushindi huu unaifanya Yanga kufuzu hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa jumla ya mabao 3-2, baada ya mechi ya kwanza iliyopigwa Septemba 5, 2026, kutoka sare ugenini ya kufungana bao 1-1, jijini, Botswana.
Yanga itakutana na CFFA FC ya Madagascar katika hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, iliyofuzu kwa kuitoa Lijabatho FC ya Lesotho.
CFFA FC imekata tiketi hiyo ya hatua inayofuata baada ya kuifunga Lijabatho FC ya Lesotho kwa jumla ya mabao 3-1, ikianza kwa ushindi wa 2-0, nyumbani, kisha marudiano ikatoka sare ya kufungana bao 1-1, ugenini.
Mechi za raundi ya pili ya hatua ya kusaka tiketi ya kufuzu makundi, itaanza kupigwa kati ya Oktoba 16 hadi 18, huku marudiano yakifanyika kuanzia kati ya Oktoba 23 hadi 25.