United vs City: Vita kali Old Trafford leo
Muktasari:
- Mchezo huu unaotarajiwa kuanza saa 10:30 jioni kwa saa za Afrika Mashariki, unawakutanisha wababe hao wakiwa na morali tofauti baada ya kupata ushindi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya katikati ya wiki.
MANCHESTER, ENGLAND: MACHO ya mashabiki wa soka duniani leo Jumapili yatakuwa Old Trafford, ambako mahasimu wakubwa wa jiji la Manchester, Manchester United na Manchester City, watakutana katika pambano la nne la Ligi Kuu England msimu wa 2026/27.
Mchezo huu unaotarajiwa kuanza saa 10:30 jioni kwa saa za Afrika Mashariki, unawakutanisha wababe hao wakiwa na morali tofauti baada ya kupata ushindi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya katikati ya wiki.
Manchester City iliifunga Porto 2-0, huku United ikifanya mambo yake kwa kishindo baada ya kuichapa Sabah mabao 4-0 ikiwa imerejea kwenye michuano hiyo baada ya kupita miaka mingi.
Licha ya matumaini makubwa yaliyokuwepo kabla ya msimu kuanza, hali imeanza kuwa tofauti kwa Manchester United, ambayo imekusanya pointi nne pekee katika michezo yake mitatu ya mwanzo ya Premier League.
Kikosi cha Michael Carrick kilianza vibaya kwa kupoteza 2-0 dhidi ya Hull City, kabla ya kuibuka na ushindi wa mabao 5-2 dhidi ya Ipswich Town.
Wiki iliyopita, United iliongeza sare nyingine yenye maumivu baada ya kutoka 2-2 dhidi ya Everton, timu iliyokuwa na wachezaji 18 pekee wenye uzoefu wa kikosi cha kwanza.
Bao la kusawazisha la Ainsley Maitland-Niles liliwanyima United ushindi na kuifanya timu hiyo kuweka rekodi isiyopendeza ya kufungwa mabao mawili katika kila mchezo wa kwanza kati ya mitatu ya ligi.
Ni mara ya pili tu katika kipindi cha miaka 50 kwa United kuanza msimu kwa kuruhusu mabao mawili katika kila mechi tatu za mwanzo, baada ya kufanya hivyo msimu wa 2020/21.
Hata hivyo, historia inaonyesha si wakati wa kuingiwa na hofu mapema. Msimu huo United ilimaliza ikiwa nafasi ya pili kwenye ligi.
CARRICK ATAKA REKODI
Ushindi wa 4-0 dhidi ya Sabah umeipa United nguvu mpya, huku timu hiyo ikipata 'clean sheet' yake ya kwanza msimu huu na kufikisha michezo mitatu mfululizo ikifunga zaidi ya bao moja.
Carrick pia amekuwa na rekodi nzuri nyumbani katika kipindi chake cha pili kama kocha, akishinda michezo tisa kati ya 10 ya Premier League kwenye uwanja wao wa Old Trafford.
Sasa anataka kuandika historia kwa kuwa kocha wa kwanza wa Manchester United katika miaka 113 kushinda mechi zake mbili za mwanzo za Manchester Derby katika ligi.
CITY YAENDELEA KUNG'ARA
Kwa upande wa pili, Manchester City inaingia kwenye mchezo huo ikiwa kileleni mwa msimamo wa Premier League.
Kikosi cha kocha Maresca kimeanza msimu kwa ushindi wa michezo mitatu mfululizo na sasa kinatafuta ushindi wa nne mfululizo.
City ilishinda 1-0 dhidi ya Coventry City wiki iliyopita kupitia kichwa cha mshambuliaji wake hatari, Erling Haaland.
Kwa sasa City inaongoza kwa tofauti ya mabao yaliyofungwa dhidi ya Arsenal, ambao ni mabingwa watetezi, kabla ya Gunners kucheza na Sunderland jana usiku.
Ushindi dhidi ya United utaifanya City kuanza msimu kwa kushinda michezo yote minne ya kwanza ya Premier League kwa mara ya saba katika historia yake rekodi mpya, ikiipita Chelsea iliyowahi kufanya hivyo mara sita.
SILAHA YA CITY
Haaland ndiye anayeendelea kuwa tishio kubwa zaidi kwa United.
Mshambuliaji huyo amefunga mabao manane katika mechi saba za ligi dhidi ya Manchester United, ingawa ni mawili pekee aliyofunga akiwa Old Trafford.
Jumanne usiku alifunga mabao mawili dhidi ya Porto, na kufikisha jumla ya mabao 42 katika mechi 39 za hatua ya makundi ligi ya Mabingwa Ulaya.
Hilo linaifanya United kuwa na kazi kubwa ya kumzuia mshambuliaji huyo mwenye kasi, nguvu na uwezo mkubwa wa kufunga.
Hata hivyo, City itamkosa Jeremy Doku anayesumbuliwa na tatizo la misuli, wakati Nico O'Reilly amerudi kuwa fiti kwa asilimia 100 baada ya kupona tatizo la mgongo.
KUHUSU KIKOSI
United imepata ahueni baada ya Luke Shaw kukosekana kwenye kikosi kilichoikabili Sabah. Carrick amefafanua kuwa beki huyo wa kushoto hakukosekana kutokana na jeraha kubwa, bali alikuwa akisumbuliwa na misuli.
Shaw anatarajiwa kuwa tayari kucheza mchezo wake wa 300 wa Premier League.
Hata hivyo, Carlos Baleba, Matthijs de Ligt, Manuel Ugarte, Tom Heaton na Amad Diallo bado hawatapatikana kutokana na majeraha.
Mjadala mkubwa Old Trafford kwa sasa ni nani aanze kati ya Benjamin Sesko na Matheus Cunha. Wote walifunga dhidi ya Sabah, lakini Marcus Rashford ndiye anaweza kujikuta akiachwa nje ya kikosi cha kwanza.
Kwa City, Enzo Fernandez anatarajiwa kuendelea kwenye kikosi cha kwanza baada ya kufanya vizuri dhidi ya Porto, huku Elliot Anderson akitarajiwa kumpisha Ayyoub Bouaddi.