Tenisi yapewa mamilioni ya ujenzi
Muktasari:
Rais wa Chama cha Tenisi Tanzania (TTA), Denis Makoyi alisema ujenzi wa kituo hicho utakamilika Januari, mwakani na mafunzo yataanza chini ya Kocha Salum Mvita.
Dar es Salaam. Shirikisho la Tenisi la Kimataifa (ITF), limeipa Tanzania Dola20,000 (zaidi ya Sh44 milioni) za ujenzi wa kituo cha mafunzo kitakachojengwa Dar es Salaam.
Rais wa Chama cha Tenisi Tanzania (TTA), Denis Makoyi alisema ujenzi wa kituo hicho utakamilika Januari, mwakani na mafunzo yataanza chini ya Kocha Salum Mvita.
Alisema ujenzi huo utafanywa na Kampuni ya BQ Contractors ambayo itaboresha viwanja vinne vilivyopo katika Klabu ya Gymkhana ya jijini.
“Huu ni msaada ambao tumepewa na ITF kwa maendeleo ya tenisi, tunaamini baada ya kukamilika kituo hiki, tutapata vijana wengi ambao watakuwa na mchango mkubwa kwenye timu ya Taifa,” alisema Makoyi.
Meneja Maendeleo na Biashara wa BQ Contractors, Hilu Bulla alisema ujenzi huo utahusisha kituo cha michezo na ukarabati wa viwanja vinne vya tenisi vilivyoko Gymkhana.
Naibu Katibu Mkuu wa TTA, Inger Njau alisema mafunzo yatahusisha vijana kati ya miaka 10 hadi 18.
“Hii ni fursa kwa wazazi kuwaleta watoto wenye vipaji vya tenisi katika kituo hicho kitakachoanza Januari mwishoni,” alisema Njau.