Nyota amkosoa kocha “mbinu zako hazifanyi kazi”
Muktasari:
- Hojbjerg mwenye umri wa miaka 31, ambaye kwa sasa anakipiga Marseille, alitoa kauli hiyo baada ya Denmark kufungwa mabao 3-2 na Norway katika mchezo wa Ligi ya Mataifa Ulaya uliochezwa Oslo hivi karibuni.
COPENHAGEN, DENMARK: KIUNGO wa zamani wa Tottenham na Southampton, Pierre-Emile Hojbjerg, amemkosoa hadharani kocha wa Denmark, Brian Riemer, akisema mbinu yake ya kumchezesha pamoja na Morten Hjulmand kwenye kiungo cha ulinzi “haifanyi kazi”.
Hojbjerg mwenye umri wa miaka 31, ambaye kwa sasa anakipiga Marseille, alitoa kauli hiyo baada ya Denmark kufungwa mabao 3-2 na Norway katika mchezo wa Ligi ya Mataifa Ulaya uliochezwa Oslo hivi karibuni.
Mchezaji huyo hakukubaliana na uamuzi wa Riemer wa kumuanza pamoja na Hjulmand, 27, akisema wawili hao wana aina inayofanana ya uchezaji na hivyo mmoja wao anapaswa kuanzia benchi.
Hojbjerg alisema hata yeye angekubali kuanzia benchi iwapo hilo lingekuwa na manufaa kwa timu, akisisitiza kuwa ushirikiano wake na Hjulmand “haujawa ukifanya kazi”.
“Tatizo ni kwamba tuna wachezaji wawili wenye aina inayofanana ya uchezaji katika kiungo,” Hojbjerg alisema, akinukuliwa na Foot Mercato.
“Huenda kocha anapaswa kumchagua mmoja na kumwacha mwingine benchi. Mwisho wa siku, tunapaswa kufikiria kile kilicho bora kwa timu na si maslahi yetu binafsi.
“Siwezi kuona aibu kusema hivi. Bila shaka, ni jukumu la kocha kutafuta kikosi kinachomfaa.
“Si jukumu langu kuamua nani acheze. Lakini kama nilivyosema, ni wazi kwamba hii haifanyi kazi. Ni jambo la aibu kidogo.”
Denmark ilikaribia kufanya mabadiliko makubwa katika mchezo huo baada ya Norway kuongoza kwa mabao mawili katika Uwanja wa Ullevaal.
Oscar Bobb na Erling Haaland waliifungia Norway kabla Mikkel Damsgaard na Rasmus Hojlund kuisawazishia Denmark.
Hata hivyo, Haaland, nyota wa Manchester City mwenye umri wa miaka 26, aliifungia Norway bao la tatu dakika ya 74 na kuwapa wenyeji ushindi.
Norway ilimaliza mchezo ikiwa pungufu baada ya David Møller Wolfe kuonyeshwa kadi nyekundu katika muda wa nyongeza, lakini Denmark haikuweza kutumia faida hiyo kusawazisha.