Nigeria yaanza kwa kipigo WAFCON
Muktasari:
- Baada ya kipindi cha kwanza kumalizika bila mabao, Malawi ilirejea kwa kasi kipindi cha pili kupitia nyota wao Temwa Chawinga aliyefunga dakika ya 73 kabla ya dada yake, Tabitha Chawinga, kuongeza la pili dakika ya 79 na kuzima matumaini ya Super Falcons.
MABINGWA watetezi wa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON), Nigeria, wameanza vibaya safari ya kutetea taji baada ya kupokea kipigo cha mabao 3-2 kutoka kwa wageni wa mashindano hayo, Malawi, katika mchezo wa Kundi C uliopigwa kwenye Uwanja wa Stade El Barid nchini Morocco.
Baada ya kipindi cha kwanza kumalizika bila mabao, Malawi ilirejea kwa kasi kipindi cha pili kupitia nyota wao Temwa Chawinga aliyefunga dakika ya 73 kabla ya dada yake, Tabitha Chawinga, kuongeza la pili dakika ya 79 na kuzima matumaini ya Super Falcons.
Baadae Nigeria ikafunga bao la kwanza kupitia kwa Rasheedat Ajibade alirejesha matumaini kwa mkwaju wa penalti dakika ya 90+2, lakini Temwa akafunga bao la tatu kwa Malawi dakika ya 90+5.
Wakati baadhi wakiamini kuwa mechi hiyo imetamatika Uchenna Kanua akaongeza bao la pili kwa Nigeria na kuifanya mechi hiyo itamatike kwa Super Falcons kupoteza kwa mabao 3-2.
Kilichoiangusha Nigeria leo ni mabeki wake kushindwa kuwadhibiti ndugu wawili Temwa na Tabitha Chawinga kwenye safu ya ushambuliaji ambao wameonekana kuwa silaha kubwa ya timu hiyo,.
Ushindi huo umeifanya Malawi kuandika historia kwa kuipiga Nigeria kwa mara ya kwanza kabisa kwenye fainali za WAFCON.
Kwa Nigeria, matokeo hayo yameongeza presha mapema kwenye mbio za kutetea ubingwa, huku yakiendeleza rekodi isiyopendeza ya mechi za ufunguzi.
Kabla ya michuano ya mwaka huu, Super Falcons walikuwa wamepoteza mechi mbili tu za kwanza kwenye historia ya WAFCON, dhidi ya Afrika Kusini mwaka 2018 na tena mwaka 2022. Kipigo cha Malawi sasa kinakuwa cha tatu, na mara ya tatu mfululizo kuanza fainali kwa kupoteza mchezo wa ufunguzi.
Licha ya kuwa mabingwa mara 10 wa Afrika na timu yenye mafanikio makubwa zaidi katika historia ya WAFCON, Nigeria sasa italazimika kupambana katika michezo iliyobaki ya Kundi C ili kufufua matumaini ya kutinga hatua ya robo fainali na kuendelea na ndoto ya kutwaa taji la 11.
Baada ya mechi hiyo ili Nigeria ijihakikishie nafasi yake inapaswa kushinda mechi ijayo dhidi ya Zambia itakayopigwa Agosti 01.
Ikumbukwe Zambia imetoka kutembeza kichapo cha mabao 6-0 dhidi ya Misri kwenye mechi ya kwanza kundi hivyo mechi baina ya timu hizo mbili haitakuwa rahisi kutokana na uhitaji wa pointi tatu kwa timu zote.