Ngock: Safari hii tunataka kucheza Kombe la Dunia
Muktasari:
- Cameroon ni moja ya mataifa matatu ambayo hayajawahi kutwaa WAFCON lakini yamewahi kufika fainali tatu mwaka 2004, 2014 na 2016 huu ukiwa ushiriki wake wa 14 kwenye mashindano hayo.
KIUNGO wa Cameroon, Monique Ngock amesema fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON 2026) ni fursa ambayo hawataki kuipoteza, wakiamini zinaweza kuwapeleka hadi Kombe la Dunia la Wanawake la FIFA 2027.
Cameroon ni moja ya mataifa matatu ambayo hayajawahi kutwaa WAFCON lakini yamewahi kufika fainali tatu mwaka 2004, 2014 na 2016 huu ukiwa ushiriki wake wa 14 kwenye mashindano hayo.
Ngock amesema awali kabla ya timu kuongezwa walikosa nafasi ya kushiriki Kombe la Dunia lakini mwaka huu wanayo nafasi ya kufanya vizuri zaidi.
"Niliposikia ni rasmi tunacheza WAFCON sikuamini hadi leo, nilijawa na hisia. Kupewa nafasi nyingine ni fursa kubwa sana kwetu. Lakini hatupaswi kusahau kilichotokea, kwa sababu tunapaswa kujifunza kutokana na makosa yetu," amesema Ngock.
Kiungo huyo mwenye miaka 21 amesema WAFCON ya mwaka huu ni muhimu kwa Cameroon kwa kuwa timu zitakazofika hatua ya nusu fainali zitafuzu moja kwa moja Kombe la Dunia la Wanawake mwakani fainali zitakazofanyika Brazil.
Ngock, ambaye aliichezea Cameroon kwenye WAFCON akiwa na umri wa mdogo zaidi kwenye kikosi hicho miaka 17 na baadaye akashiriki Kombe la Dunia la Wanawake chini ya miaka 20 nchini Colombia mwaka 2024, amesema uzoefu alioupata kwenye mashindano makubwa unampa imani ya kuisaidia nchi yake kufanya vizuri safari hii.
Nyota huyo, aliyeng'ara katika ligi ya wanawake ya Ufaransa akiwa na Reims na baadaye kutimkia Fleury kabla ya kuhamia Washington Spirit ya Marekani, amesema yeye na wenzake wataingia uwanjani wakiwa na dhamira ya kupigania taifa hilo ili kuandika historia mpya.