Neville atuma ujumbe kwa Mikel Arteta
Muktasari:
- Licha ya Arsenal kutoka sare kupitia bao la dakika za mwisho la Gabriel Martinelli, Arteta alikosolewa kwa kumwacha benchini Eberechi Eze na Bukayo Saka na badala yake kuanza na Mikel Merino na Leandro Trossard.
LONDON, ENGLAND: LEJENDI wa Manchester United na mchambuzi wa soka, Gary Neville amedai kwamba Mikel Arteta atajutia kutokubali kwamba ana woga katika kushambulia jambo ambalo lilionekana katika mechi iliyopita ya Ligi Kuu England dhidi ya Manchester City mwishoni mwa wiki iliyopita.
Licha ya Arsenal kutoka sare kupitia bao la dakika za mwisho la Gabriel Martinelli, Arteta alikosolewa kwa kumwacha benchini Eberechi Eze na Bukayo Saka na badala yake kuanza na Mikel Merino na Leandro Trossard.
Wachambuzi na mashabiki waliona kwamba amefanya uamuzi huo ili kujilinda kwani alishawahi kumwacha Eze benchini na kuanza na Merino.
Baada ya sare ya 1-1 katika mchezo huo uliopigwa kwenye dimba la Emirates, Arteta alitetea uamuzi wake wa kwamba alicheza kwa kuvizia na kusisitiza kwamba walitawala mchezo dhidi ya kikosi cha Pep Guardiola.
Lakini beki wa zamani wa Manchester United, Neville, anaamini kocha huyo ambaye kwa sasa yupo kwenye shinikizo la kuchukua taji msimu huu amekosea na atakuja kujuta.
"Sidhani kama mashabiki 60 au elfu 70,000 wa Arsenal waliokuwapo uwanjani wote wamekosea kusema timu ilikuwa inashambulia kwa kusitasita. Sidhani pia kama sisi tuliokuwa studioni au waliokuwa nyumbani wakitazama runinga wote wamekosea. Kitu kikubwa kwangu ni wachezaji. Arteta anatangaza kikosi siku ya Ijumaa mchana na anamwacha Eze, anamwacha Martinelli, anamwingiza Trossard na Merino, anawapa nafasi wachezaji kuanza kuzisema mbinu na machaguo yake."
"Angeweza kushambulia zaidi katika mechi yake dhidi ya Liverpool lakini hakufanya hivyo, na angeweza kushambulia zaidi dhidi ya Man City lakini pia hakufanya hivyo. Atajutia hili kama hatobadilika."