Ndula ya Kobe sokoni mwakani
Muktasari:
- Kifo cha nyota huyo wa Los Angeles Lakers aliyeaga dunia Januari 27, 2000, kiliondoka na simulizi tamu ya mchezaji aliyekuwa amestaafu kikapu miaka minne tangu alipocheza mchezo wake wa mwisho mjini Utah, Mei, 2016, ambao pia ulikuwa wa kuagana na mchezo alioupenda zaidi maishani mwake.
LOS ANGELES, MAREKANI: Kobe Bryant ‘The Black Mamba’ alifariki dunia huko Calabasas, California, miaka sita iliyopita kwa ajali ya gari ya helkopta akiwa na bintiye, Gianna, wakienda kutembelea miradi yake ya kikapu.
Kifo cha nyota huyo wa Los Angeles Lakers aliyeaga dunia Januari 27, 2000, kiliondoka na simulizi tamu ya mchezaji aliyekuwa amestaafu kikapu miaka minne tangu alipocheza mchezo wake wa mwisho mjini Utah, Mei, 2016, ambao pia ulikuwa wa kuagana na mchezo alioupenda zaidi maishani mwake.
Kobe alitumia maisha yake yote ya miaka 20 katika Ligi ya Kikapu Marekani (NBA) kucheza Los Angeles Lakers na kushinda mataji mbalimbali makubwa, huku akiondoka na utajiri mkubwa ulioambatana na kubuni au kubuniwa kwa biashara nyingi zilizokuwa na chapa au jina lake hasa ‘The Black Mamba’.
Miongoni mwa chapa za biashara zilizokuwa na jina la mwamba huyo ni zile za kampuni mbalimbali za vifaa vya michezo ikiwamo Nike ambao walizalisha viatu na fulana zenye ‘kijichata’ cha chapa yake, ambapo bidhaa yao maarufu ilikuwa kiatu cha mpira wa kikapu cha Nike Kobe 7 ‘Invisibility Cloak’.
Viatu hivyo vilivyojizolea umaarufu vinatarajiwa kurejea sokoni mwakani, 2027, ikiwa takriban miaka 14 imepita tangu vilipotolewa kwa mara ya kwanza Oktoba 2012. Viatu hivyo, vilivyobuniwa chini ya jina la nyota huyo wa zamani wa NBA, ni miongoni mwa miundo iliyovutia zaidi katika mkusanyiko wa viatu vyake. Na sasa vinarejeshwa kupitia mfululizo wa Kobe Protro, unaolenga kuboresha teknolojia na vifaa vya viatu vya zamani huku ukihifadhi muonekano wake wa awali.
“Invisibility Cloak” vilipata umaarufu kutokana na rangi zake zinazobadilika kulingana na mwanga na pembe ya eneo ambalo mtazamaji anapokaa. Sehemu ya katikati ya soli na kisigino ina mng’ao unaobadilika kati ya rangi ya zambarau, bluu na kijani, unaofanana na mng’ao wa ngozi ya nyoka.
Muonekano wake wa kipekee unaongezwa na sehemu ya juu yenye michoro inayofanana na ngozi ya nyoka, jambo linalovipa mwonekano wa kisasa na wa kuvutia.
Inaelezwa kwamba toleo jipya la viatu hivyo litakuwa na teknolojia ya kisasa chini ya mfumo wa Protro, ambao Nike hutumia kuboresha viatu vya zamani vya Kobe kwa teknolojia na vifaa vya kisasa vinavyolenga kuongeza ufanisi wa matumizi uwanjani, huku ikihifadhi muundo wa awali.
Hata hivyo, kampuni hiyo bado haijafichua maboresho mahususi yatakayofanywa katika toleo la mwaka 2027.
Uzinduzi huo ni sehemu ya juhudi za kuhuisha mkusanyiko wa viatu vilivyobeba jina la Kobe Bryant, kwa kurejesha sokoni miundo iliyopendwa na mashabiki miaka mingi iliyopita. Matoleo mengine maarufu ya Kobe 7 ni pamoja na “Cheetah,” lililotolewa kwa msimu wa Krismasi pamoja na “What The” na mfululizo wa “Poison Dart Frog.”
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Sneaker Files na akaunti ya @zsneakerheadz, Nike Kobe 7 Protro “Invisibility Cloak” vinatarajiwa kuuzwa kuanzia Februari 2027. Uzinduzi huo huenda ukaendana na wiki ya NBA All-Star ya mwaka huo, ingawa tarehe rasmi bado haijatangazwa na Nike.
Kurejea kwa viatu hivyo kunatarajiwa kuwavutia mashabiki wa Kobe Bryant na wakusanyaji wa viatu vya mpira wa kikapu, hasa kutokana na muundo wake wa kipekee na historia yake tangu vilipotolewa kwa mara ya kwanza 2012.