Mariga avuliwa umakamu wa rais FKF, Ambani apinga
Muktasari:
- Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Soka Kenya (FKF) umemvua cheo makamu wa rais wa shirikisho hilo, McDonald Mariga pamoja na wajumbe sita wa Kamati ya Utendaji ya Taifa (NEC) kwa madai ya kukiuka Katiba na kanuni za FIFA.
Meru, Kenya. Kiungo wa zamani wa timu ya taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’ na Inter Milan, McDonald Mariga, ameondolewa katika nafasi yake ya makamu wa rais wa Shirikisho la Soka Kenya (FKF) sambamba na ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya Taifa (NEC).
Uamuzi ho ulifikiwa leo Jumamosi, Novemba 7, 2026, katika kikao kilichofanyika kaunti ya Meru.
Mbali ya Mariga, wajumbe wengine sita wa NEC nao wameng'olewa.
Waliofukuzwa pamoja na Mariga ni Robert Kenneth Macharia (Kaunti ya Kati), Bernard Korir Lagat (Kaunti ya Bonde la Ufa la Juu), Violet Kerubo Momanyi (Mwakilishi wa Wanawake), Collins Opiyo Kalee (Kaunti ya Nyanza), Gabriel Mghendi (Kaunti ya Pwani) na Daniel Akala Shikanda (Kaunti ya Nairobi).
KURA 65 DHIDI YA 1
Katika kura zilizopigwa chini ya ulinzi mkali wa polisi, wajumbe 65 walipiga kura ya kumwondoa Mariga, huku Mwenyekiti wa AFC Leopards, Boniface Ambani akiwa pekee aliyepinga.
Kikao hicho kilichoongozwa na Rais wa FKF, Hussein Mohammed, kilihudhuriwa pia na wawakilishi wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na lile la Afrika (CAF).
CHANZO CHA MOTO NI NINI?
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na FKF baada ya kikao hicho, wajumbe hao saba wanatuhumiwa kukiuka mara kwa mara Katiba ya FKF na kanuni za FIFA.
Miongoni mwa tuhuma zilizowakabili ni pamoja na azimio la Aprili 24, mwaka huu, lililodaiwa kutaka kumwondoa Rais Hussein Mohammed na viongozi wengine, kutohudhuria mara kwa mara vikao vya NEC vilivyoitishwa kihalali, na kutoa mawasiliano bila idhini kwa niaba ya shirikisho.
CHANZO CHA SAKATA
Ugomvi kati ya Mariga na Hussein ulianza baada ya fainali za CHAN 2025 zilizofanyika jijini Nairobi. Kundi la Mariga lilidai kuwepo na ubadhirifu wa Sh 40.48 milioni za Kenya (Sh823 milioni) zilizotumika kwenye bima ya michuano hiyo.
Kundi hilo lilimtangaza Mariga kuwa Rais wa muda na kutaka uchunguzi ufanyike kuhusu fedha za shirikisho, hatua ambayo FIFA iliikataa na kuitaka pande hizo mbili zikae mezani mazungumzo.
FKF imesema itatoa taarifa zaidi kuhusu namna nafasi hizo saba zitakavyojazwa. Hata hivyo, inaelezwa kuwa kundi la Mariga linatarajia kupinga uamuzi huo mahakamani Jumatatu Novemba 9, 2026.