Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwisho wa enzi, San Siro kubomolewa, mrithi huyu hapa

SAN SIRO Pict

Muktasari:

  • Uwanja huo utakaochukua idadi ya mashabiki 71,500, ujenzi wake utaanza mwaka 2028 huku ukitarajiwa kuanza kutumika msimu wa 2031/2032.

MILAN, ITALIA: Klabu kongwe za soka Italia, AC Milan na Inter Milan, zimetoa picha za awali za Uwanja wao mpya utakaogharimu mabilioni ya fedha, huku uamuzi wa kubomoa Uwanja wa San Siro ukikaribia kutekelezwa.

Uwanja huo mpya unatarajiwa kuchukua nafasi ya San Siro, ambao umekuwa nyumbani kwa timu hizo kwa miaka mingi. Unatarajiwa kuanza kutumika katika msimu wa 2031/32, huku ujenzi wake ukipangwa kuanza mwaka 2028.

Uwanja huo utaitwa Generali baada ya kampuni ya bima ya Generali kupata haki za kutumia jina hilo hadi mwaka 2052 kwa mkataba wa Pauni 543 milioni (Sh1.8 trilioni).

SAN 01

Kwa mujibu wa mipango iliyowasilishwa, uwanja huo utakuwa na uwezo wa kuchukua watazamaji 71,500 na utakuwa na muundo wa kisasa wenye ghorofa mbili, paa lenye umbo la kipekee na nguzo zinazounda herufi X.

Muundo wake umezingatia utambulisho wa klabu hizo mbili, ambapo sehemu moja itahusishwa na Inter Milan na nyingine AC Milan. Picha zilizowasilishwa zinaonyesha uwanja ukiwa na mwanga wa bluu wakati wa mechi za Inter na nyekundu wakati wa michezo ya AC Milan.

Mbali na mechi za soka, uwanja huo pia umepangwa kutumika kwa matamasha na shughuli nyingine za burudani. Eneo lake litakuwa na sehemu za wazi, pamoja na maeneo ya biashara na mapumziko.

Mipango ya kuondoka San Siro imekuwepo kwa miaka kadhaa, huku klabu hizo zikianza kutafuta njia ya kujenga uwanja mpya tangu mwaka 2019. Hata hivyo, mchakato huo ulikumbana na vikwazo kutokana na umuhimu wa kihistoria na kitamaduni wa uwanja huo.

Mwaka 2023, kulikuwa na uamuzi uliokwamisha uwezekano wa kuubomoa San Siro kutokana na hadhi yake ya kitamaduni. Hata hivyo, mwaka 2025, AC Milan na Inter Milan zilinunua eneo hilo, hatua iliyofungua njia ya kuendeleza mpango wa uwanja mpya.

Uwanja wa San Siro, ambao pia unajulikana kama Giuseppe Meazza, ulianza kutumika mwaka 1926. Baadaye, mwaka 1955, ulifanyiwa maboresho makubwa yaliyohusisha kuongeza sehemu ya viti na minara yake maarufu yenye umbo la mzunguko.

Wasanifu Norman Foster na David Manica, ambao kampuni zao Foster + Partners na Manica zilichaguliwa kuandaa usanifu wa uwanja huo, waliwasilisha mipango hiyo katika mkutano uliofanyika jana Alhamisi, Oktoba 29, 2026.

Akizungumzia mradi huo, Manica amesema changamoto kubwa ilikuwa kubuni uwanja mpya ambao ungeendeleza hisia na utambulisho unaohusishwa na San Siro.

Amesema lengo lao lilikuwa kuhifadhi roho ya uwanja wa zamani huku wakijenga jengo jipya lenye muundo tofauti.

San Siro pia ulikuwa umepangwa kuandaa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, lakini Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) liliondoa haki hiyo baada ya mamlaka za jiji la Milan kushindwa kutoa uhakika kwamba kazi za ukarabati wa uwanja na maeneo yanayouzunguka hazingeathiri maandalizi ya mechi hiyo.

Uwanja mpya unatarajiwa pia kuwa miongoni mwa maeneo yatakayoweza kuandaa mechi za Fainali za Mataifa ya Ulaya 2032 ambazo Italia itaandaa kwa pamoja na Uturuki.