Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kivuli cha Ferguson chaitesa Man United

KIVULI Pict

Muktasari:

  • Carrick alijikuta katika hali inayofanana na aliyowahi kukumbana nayo Ole Gunnar Solskjaer, aliyewahi kusimama mbele ya mashabiki akiomba radhi baada ya United kufungwa mabao 4-1 na Watford Novemba 2021, matokeo yaliyochangia kufutwa kazi kwake.

MANCHESTER, ENGLAND: KILA kocha anayekabidhiwa mikoba ya Manchester United anaonekana kuingia katika mtego uleule uliowanasa waliomtangulia. Sasa mzunguko huo wa kushindwa na kufukuzwa umeanza kumkabili Michael Carrick, ambaye anakabiliwa na wakati mgumu baada ya matokeo mabaya na kuongezeka kwa sintofahamu ndani ya klabu hiyo yenye historia kubwa.

Carrick alijikuta katika hali inayofanana na aliyowahi kukumbana nayo Ole Gunnar Solskjaer, aliyewahi kusimama mbele ya mashabiki akiomba radhi baada ya United kufungwa mabao 4-1 na Watford Novemba 2021, matokeo yaliyochangia kufutwa kazi kwake.

Safari hii, Carrick alifanya vivyo hivyo baada ya United kufedheheka kwa kipigo cha mabao 4-1 dhidi ya Como katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, kabla ya kuchapwa 3-0 nyumbani na Bournemouth katika Ligi Kuu huku mashabiki wakiwa wamekata tamaa kutokana na mwenendo wa timu yao.

Carrick ni kocha wa saba wa kudumu tangu Sir Alex Ferguson alipoondoka mwaka 2013, baada ya kuitumikia United kwa miaka 26 na kutwaa mataji 38.

Katika kipindi kilichofuata, klabu hiyo imepitia nyakati za mafanikio chini ya Louis van Gaal, Jose Mourinho na Erik ten Hag, lakini mwisho wa safari kwa makocha hao umekuwa mmoja: kufutwa kazi.

Kwa Carrick, kubadili mwelekeo huo kunahitaji zaidi ya matokeo machache mazuri. Mbali na mwenendo usioridhisha uwanjani, kumekuwa na dalili za kutoridhika ndani ya kikosi.

KIVU 01

Beki Lisandro Martinez aliikosoa safu ya uongozi, akimlenga mkurugenzi wa soka Jason Wilcox baada ya kipigo cha Ligi ya Mabingwa dhidi ya Atletico Madrid. Nahodha Bruno Fernandes naye alihoji mbinu za timu baada ya mchezo dhidi ya Como.

Matukio hayo yanaibua swali kubwa: Je, tatizo la Manchester United ni makocha pekee, au kuna jambo kubwa zaidi linaloendelea ndani ya klabu hiyo?

Kwa miaka mingi, makocha wamekuwa wakibeba lawama na kulazimika kujieleza mbele ya mashabiki waliokatishwa tamaa. Lakini je, ni sahihi kuendelea kuwafanya wao kuwa wahusika wakuu wa kushindwa kwa United, bila kuhoji zaidi viongozi wanaowateua na kuamua mwelekeo wa klabu?

Hapo ndipo swali gumu linapojitokeza: Je, Manchester United imekuwa klabu isiyoweza kusimamiwa kwa ufanisi?

Tangu Ferguson aondoke, United imefundishwa na makocha saba tofauti ambao ni David Moyes, Van Gaal, Mourinho, Solskjaer, Ten Hag, Ruben Amorim na sasa Carrick. Pia, klabu hiyo imewahi kutumia makocha wa muda kama Ryan Giggs, Ralf Rangnick, Ruud van Nistelrooy na Darren Fletcher.

Viongozi wa United, kuanzia aliyekuwa makamu mwenyekiti mtendaji Ed Woodward, familia ya Glazer inayomiliki sehemu kubwa ya klabu, hadi mmiliki mwenza Sir Jim Ratcliffe, wamejaribu njia mbalimbali za kurejesha mafanikio yaliyopatikana chini ya Ferguson. Hata hivyo, jitihada hizo hazijazaa matokeo yaliyotarajiwa.

Moyes, aliyependekezwa kwa kiasi kikubwa na Ferguson, alishindwa kuhimili ukubwa wa jukumu hilo baada ya kuondoka Everton. Van Gaal na Mourinho walikuwa makocha wenye rekodi kubwa za mafanikio katika klabu kubwa za Ulaya, lakini nao hawakuweza kuijenga upya United kwa kiwango kilichotarajiwa.

KIVU 02

Solskjaer alikuwa chaguo tofauti na Mourinho. Alipata nafasi baada ya kuonyesha matokeo mazuri alipokuwa kocha wa muda, ingawa hakuwa na rekodi kubwa ya ukocha iliyothibitisha kuwa angeweza kuhimili changamoto ya kuinoa United kwa muda mrefu.

Ten Hag aliteuliwa baada ya kuiongoza Ajax iliyokuwa na wachezaji wengi vijana hadi nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Amorim naye alichukuliwa kuwa mmoja wa makocha vijana waliokuwa wakihitajika zaidi Ulaya baada ya mafanikio yake Sporting Lisbon.

Licha ya historia na uwezo wao, wote waliishia kuondoka. United imeendelea kuwa changamoto ngumu kwa kila kocha anayepewa jukumu la kuirejesha katika hadhi yake ya zamani.

Mafanikio yaliyopatikana katika kipindi hicho yamekuwa machache yakilinganishwa na historia ya klabu. Van Gaal alitwaa Kombe la FA mwaka 2016, Mourinho akashinda Kombe la Europa Ligi mwaka 2017, huku Ten Hag akitwaa Kombe la FA mwaka 2024 baada ya ushindi muhimu dhidi ya Manchester City.

KIVU 03

Hayo ni mafanikio yanayostahili kutambuliwa, lakini hayalingani na matarajio ya klabu iliyokuwa ikitawala soka la England na kushindana kwa mafanikio makubwa barani Ulaya.

United haikufika katika hali yake ya sasa kwa siku moja. Kushuka kwake kulianza kuonekana tangu mpango wa kumrithi Ferguson uliposhindwa kutekelezwa kwa ufanisi, licha ya ukweli kwamba kumtafuta mrithi wa kocha aliyekuwa na mafanikio ya kiwango hicho haikuwa kazi rahisi.

Carlo Ancelotti, Pep Guardiola na Jurgen Klopp ni miongoni mwa makocha wakubwa walioweza kuikataa nafasi ya kuinoa United au kuelekea katika mwelekeo mwingine. Desemba 2019, hali hiyo ilionekana wazi zaidi: Ancelotti alikuwa Everton, Guardiola akiinoa Manchester City na Klopp akiwa Liverpool. Wote walikuwa wakifanya kazi ndani ya umbali wa maili 35 katika eneo la kaskazini magharibi mwa England, lakini hakuna aliyekuwa Old Trafford.

Badala yake, United ilikuwa na Solskjaer, aliyeteuliwa kutokana na mafanikio ya muda na uhusiano wake mzuri na mashabiki. Hata hivyo, hakudumu hata miaka mitatu katika nafasi hiyo.

Sasa Carrick anaonekana kufuata njia inayofanana na ya Solskjaer. Wote walikuwa wachezaji waliopendwa na mashabiki wa United na walipata matokeo mazuri walipopewa timu kwa muda. Lakini rekodi zao za ukocha kabla ya kupewa jukumu hilo haikuwa ya kiwango kikubwa.

KIVU 04

Carrick aliwahi kufutwa kazi Middlesbrough, iliyokuwa ikishiriki Championship, wakati Solskjaer aliondolewa Cardiff City Septemba 2014 baada ya miezi tisa tu kutokana na matokeo mabaya katika ligi hiyo.

Hali hiyo imeifanya United kufikia hatua ya kujiuliza kama kipindi cha sasa ndicho kigumu zaidi tangu Ferguson aondoke. Kwa kuzingatia mwenendo wa timu, mazingira ya ndani na kiwango cha matumaini miongoni mwa mashabiki, kuna hoja kuwa klabu hiyo haijawahi kuwa katika hali ya kukatisha tamaa kiasi hiki katika miaka ya karibuni.

United bado inaweza kumpata kocha mpya kwa sababu ya jina na historia yake. Hata hivyo, mazingira yake ya sasa yanaweza kuifanya isiwe chaguo la kwanza kwa makocha wakubwa kama ilivyokuwa zamani.

Klabu hiyo italazimika kumshawishi kocha atakayepewa jukumu hilo kuwa Old Trafford kuna mustakabali wenye mafanikio, badala ya kuwa sehemu nyingine ya mzunguko wa kuajiri na kufukuza makocha.

KIVU 05

Changamoto hiyo inakuwa kubwa zaidi kwa kuzingatia hali ya kikosi cha sasa. Hata kocha mwenye rekodi kubwa ya mafanikio hawezi kuhakikishiwa kubadili mambo kwa muda mfupi bila uwekezaji mkubwa na marekebisho ya kina.

Carrick ndiye anayekaa mbele ya kamera na kubeba lawama kwa sasa, lakini tatizo la United linaonekana kuwa kubwa kuliko kocha mmoja. Uteuzi wake ulifanyika baada ya kuisaidia timu kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini matokeo mabaya yameanza kufuta matumaini yaliyokuwepo. Sehemu nyingine ya lawama inaelekezwa kwa Ratcliffe na uongozi wa klabu.

Mashabiki wa United wamekuwa wakifanya maandamano dhidi ya familia ya Glazer tangu ilipochukua udhibiti wa klabu mwaka 2005. Ununuzi huo uliohusisha mikopo uliiachia United mzigo mkubwa wa madeni, huku familia hiyo ikiendelea kuwa mmiliki mkuu licha ya hasira za mashabiki kwa miaka mingi.

Ratcliffe alipoingia katika umiliki wa sehemu ya klabu akiwa mshirika wa familia ya Glazer, naye alianza kukabiliwa na hasira za mashabiki kutokana na uhusiano wake na wamiliki hao wasiopendwa na wengi.

Kama ilivyokuwa kwa matajiri wengine waliofanikiwa katika biashara zao, Ratcliffe amekutana na ukweli kwamba kuendesha klabu ya soka ni jambo tofauti na kusimamia biashara katika sekta nyingine.

Amesema amewaachia watu wengine, akiwamo Wilcox na mtendaji mkuu Omar Berrada, kushughulikia maamuzi makubwa ya soka. Hata hivyo, kipindi chake kama kiongozi mkuu wa United kimeendelea kushuhudia ukosefu wa uthabiti na maamuzi yaliyotiliwa shaka.

Mfano mkubwa ni suala la Ten Hag. United ilikuwa imepanga kumfukuza kocha huyo kabla ya fainali ya Kombe la FA dhidi ya Manchester City mwaka 2024, lakini ushindi wa Wembley ulimpa nafasi ya kuendelea na kazi. Badala ya kuondoka, Ten Hag aliongezewa mkataba na kupewa takribani pauni milioni 200 kwa ajili ya usajili wa wachezaji. Hata hivyo, miezi sita baadaye alifutwa kazi. Malipo ya kuvunja mikataba yake na wafanyakazi wake yalizidi Pauni 10 milioni.

KIVU 06

Uamuzi huo ulionekana kuwa na gharama kubwa kifedha na kisoka, huku ukiibua maswali kuhusu namna viongozi walivyopima uwezo wa kocha huyo na kupanga mustakabali wa timu.

Kulikuwa pia na sakata la Dan Ashworth, aliyeteuliwa kuwa mkurugenzi wa michezo mwaka 2024 na baadaye kuondoka baada ya miezi mitano tu kutokana na kutokubaliana na viongozi wengine nyuma ya pazia.

Ashworth alijiunga na United Julai akiwa na sifa ya kuwa mmoja wa wasimamizi mahiri katika soka. Hata hivyo, muda wake klabuni ulikuwa mfupi kiasi cha kuibua taswira ya taasisi isiyo na mwelekeo thabiti.

Jambo la kushangaza ni muda alioutumia kusubiri kujiunga na United wakati akiwa kwenye likizo ya lazima ya kutojihusisha na kazi baada ya kuondoka Newcastle United ulikuwa karibu sawa na muda aliokaa kazini Old Trafford.

Kulikuwa na madai Ashworth alilaumiwa kwa uamuzi wa kuendelea na Ten Hag. Nadharia nyingine ilidai kuwa alitaka United iwape kipaumbele makocha Waingereza kama Graham Potter na Gareth Southgate badala ya Amorim. Hatimaye, United ilimchagua Amorim, ambaye alisisitiza kutumia mfumo wa 3-4-3.

Mfumo huo ulikuwa umeibua mashaka kwa baadhi ya wadau, huku Liverpool ikichagua Arne Slot kumrithi Klopp.

Amorim aliondoka baada ya miezi 14, lakini si kabla ya kuonyesha kutoridhishwa na viongozi wa United na kukumbana na mkutano mkali na Wilcox. Hata kabla Carrick hajateuliwa, hali ya wafanyakazi wa United ilikuwa imeathiriwa na hatua za kupunguza gharama zilizotekelezwa chini ya Ratcliffe, zilizosababisha wafanyakazi wengi kuondoka katika kile kilichoelezwa kuwa ni mpango wa kuongeza ufanisi.

Kwa upande wa mashabiki, kutoridhika kuliongezeka zaidi msi mu huu baada ya klabu kuanzisha uchunguzi kuhusu matum izi ya tiketi. United ilikiri kuwa haikuwa imekadiria kwa usahihi idadi ya mashabiki waliokuwa wakishiriki taarifa za akaunti zao, na baadaye ikapunguza baadhi ya vitisho vya kufuta tiketi za msimu kwa mashabiki ambao hawakujibu maombi ya klabu kwa namna ilivyotaka.

Hata hivyo, viongozi wa United waliendelea kutetea uchunguzi huo, hatua iliyochochea zaidi hisia za mashabiki ambao tayari walikuwa hawaridhishwi na mwenendo wa timu. Kwa upande wa fedha, matatizo nayo hayajaisha licha ya Ratcliffe kuahidi kuboresha hali ya klabu kupitia udhibiti wa matumizi.

Takwimu zilizotolewa Septemba zilionyesha kuwa jumla ya madeni ya United bado ilikuwa karibu pauni bilioni moja.

Hata hivyo, klabu ilitangaza mapato ya rekodi ya Pauni 678 milioni na faida ya uendeshaji ya Pauni 23 milioni, licha ya kutoshiriki mashindano ya Ulaya kwa mara ya kwanza ndani ya muongo mmoja.

Huo ulikuwa mabadiliko makubwa ikilinganishwa na hasara ya Pauni 113 milioni iliyorekodiwa katika msimu wa 2023/24.

United pia ilithibitisha kutumia Pauni 64 milioni kununua ardhi kwa ajili ya ujenzi wa uwanja mpya. Ratcliffe anautazama mradi huo kama sehemu muhimu ya urithi wake klabuni na ishara ya dhamira yake ya kurejesha mafanikio.

Agosti, Berrada alisema mpango wa kujenga uwanja wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 100,000 bado unaendelea kama ulivyopangwa, huku gharama zikikadiriwa kuzidi pauni bilioni mbili.

Hata hivyo, pamoja na mipango hiyo ya muda mrefu, United bado inakabiliwa na tatizo la maamuzi mabovu ya uongozi na ukosefu wa mafanikio uwanjani. Mchanganyiko huo umeendelea kuathiri klabu, na sasa kuna hatari ya kuingia katika kipindi kingine cha mabadiliko ya makocha na viongozi bila suluhisho la kudumu.

Wakati huo huo, klabu ambazo United imekuwa ikizichukulia kama wapinzani wake wakuu zinaendelea kujenga mifumo imara zaidi, jambo linaloweza kuifanya timu hiyo ya Old Trafford izidi kubaki nyuma.

Kwa klabu iliyojijengea jina la kuwa miongoni mwa kubwa zaidi duniani, changamoto si kutafuta kocha mwingine pekee.

Ni kujibu swali la msingi: je, viongozi wa Manchester United wana mpango thabiti wa kuirejesha klabu katika kiwango chake cha zamani, au wataendelea kurudia makosa yale yale kwa gharama kubwa zaidi?