Mtasema! Guardiola awalaza mastaa mazoezi
Muktasari:
- Pep Guardiola alifichua kwamba wachezaji wake hawatolala katika majumba yao siku ya Krismasi na badala yake watakuwa katika hosteli za kiwanja chao cha mazoezi ambako watatakiwa kuwasili kuanzia jioni baada ya kushinda na wapendwa wao asubuhi na mchana.
MANCHESTER, ENGLAND: WACHEZAJI wa Manchester City walilazimika kulala kwenye uwanja wa mazoezi wa timu hiyo siku moja kabla ya mchezo wao dhidi ya Everton uliopigwa jana kwenye dimba la Etihad.
Pep Guardiola alifichua kwamba wachezaji wake hawatolala katika majumba yao siku ya Krismasi na badala yake watakuwa katika hosteli za kiwanja chao cha mazoezi ambako watatakiwa kuwasili kuanzia jioni baada ya kushinda na wapendwa wao asubuhi na mchana.
Kabla ya mchezo wao dhidi ya Everton wa jana, Man City ilikuwa imepoteza mechi tisa kati ya 12 zao za mwisho, ikiwa ni rekodi mbaya zaidi katika kipindi cha uongozi wa Guardiola, na mechi yao ya mwisho kushinda ilikuwa ni Desemba 4 dhidi ya Nottingham Forest.
Huo sio utaratibu mpya kwa wachezaji wa Man City kulala katika hosteli za kiwanja cha mazoezi na ulianza mwaka 2014 ambapo ilikuwa ndio timu ya kwanza kufanya hivyo.
Katika kiwanja hicho cha mazoezi kuna vyumba 80 vya kulala, pia kiujumla walitumia pauni 150,000 kununua magodoro na mablanketi.
City Football Academy (CFA) ama Etihad Cumpus ilifunguliwa mwaka 2014 baada ya kufanyiwa maboresho yaliyogharimu zaidi ya Pauni 300 milioni.
“Tunafanya mazoezi leo (Jumanne), tutafanya pia kesho (Jumatano) jioni, kisha tutalala hapa na tutacheza mechi (ya jana), ni matumaini yangu watafurahi hilo, kwa sababu ni kazi yetu.”
Moja kati ya sababu za Guardiola kuwalaza mastaa hao kambini hapo ni kujaribu kurudisha umakini katika kipindi hiki kigumu kwao.
Licha ya kwamba iliwahi kuwa utaratibu wa kawaida kwa timu hii lakini ilipita muda mrefu bila ya kufanya hivyo na Mhispania huyo aliona mastaa wake wakilala kambini watakuwa kwenye hali nzuri kuelekea mchezo wao wa jana tofauti na wakishinda na familia hadi siku ya mechi kwani wanaweza kufanya vitu vitakavyosababisha wasicheze vizuri ikiwa pamoja na unywaji wa pombe kupitiliza.
Everton wameonyesha ubora wao hivi karibuni kwa kushinda 4-0 dhidi ya Wolves kabla ya kutoa sare za 0-0 dhidi ya Arsenal na Chelsea.
Man City inapambana kuboresha kiwango chake baada ya kuwa katika kipindi kigumu kwa zaidi ya miezi miwili sasa.
Tangu atue katika kikosi cha Manchester City mwaka 2016, Guardiola mwenye umri wa miaka 53, amekuwa ndiye mwenye mafanikio zaidi katika kipindi hicho hadi sasa, akifanikiwa kuchukua mataji sita ya Ligi Kuu England, moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya na la Klabu Bingwa Dunia pia ana makombe manne ya Carabao na mawili ya FA.