Mshambuliaji wa Leeds aingia rada za Man United
Muktasari:
- United inahitaji mshambuliaji baada ya Benjamin Sesko, kupata majeraha yatakayomuweka nje ya uwanja hadi Januari mwakani.
MANCHESTER, ENGLAND: Manchester United inafikiria uwezekano wa kumsajili mshambuliaji wa Leeds United, Dominic Calvert-Lewin, katika dirisha dogo la usajili la Januari mwakani baada ya mshambuliaji Benjamin Sesko, kupata jeraha.
Man United inataka kuimarisha safu yake ya ushambuliaji, ingawa kumsajili Calvert-Lewin kunaweza kuwapa ugumu kutokana na ushindani wa muda mrefu kati ya klabu hizo mbili.
Calvert-Lewin, 29, alijiunga na Leeds United kwa uhamisho wa bure mwaka 2025 baada ya kuondoka Everton, ambako kipindi chake cha mwisho kiliathiriwa na majeraha.
Tangu ajiunge na Leeds United amefunga mabao 20 katika mechi 49, yakiwamo matano katika michezo 10 ya mwanzo wa msimu huu. Pia alifunga dhidi ya Manchester United katika mchezo uliomalizika kwa sare ya 1-1 mapema mwezi huu.
Kiwango chake kizuri kimemwezesha kurejea katika kikosi cha timu ya taifa ya England baada ya kukosekana kwa takribani miaka mitano.
Man United inahitaji mshambuliaji kutokana na Sesko, 23, kutarajiwa kuwa nje ya uwanja hadi Januari mwakani kwa sababu ya jeraha la mfupa wa chini wa mguu.
Sesko hajacheza tangu Septemba 16, katika mchezo dhidi ya Brighton kwenye Kombe la Carabao.
Kutokana na hali hiyo, winga Bryan Mbeumo ametumika kama mshambuliaji wa kati katika mechi tano zilizopita za United katika mashindano yote.
Hata hivyo, uwezekano wa Calvert-Lewin kuhamia Old Trafford unakabiliwa na changamoto ya ushindani wa kihistoria kati ya United na Leeds. Mshambuliaji huyo ana mkataba na Leeds hadi mwaka 2028.
Klabu hizo zimewahi kubadilishana wachezaji licha ya ushindani wao, akiwamo Eric Cantona aliyejiunga na United mwaka 1992 na Rio Ferdinand mwaka 2002.
Katika majira ya kiangazi mwaka huu, kipa Karl Darlow pia alihamia Man United kutoka Leeds United, akiwa mchezaji wa kwanza kujiunga na klabu hiyo kutoka Leeds United tangu Alan Smith mwaka 2004.