MR MAJIVUNO: Ronaldo adai yeye bora kuliko Messi na wakongwe wengine
"Ni suala la maoni. Naheshimu maoni. Labda kwa maoni yako Messi ni bora zaidi yangu, lakini kwa akili yangu mimi ni zaidi kuliko Messi. Ni rahisi tu kama hivyo"
RONALDO
Muktasari:
Alipoulizwa kuhusu ulinganisho wake na hasimu wake wa Barcelona na timu ya taifa ya Argentina, Lionel Messi ambaye amechaguliwa mara nne kuwa mwanasoka bora wa dunia huku akifunga mabao 418 katika mechi 492, Ronaldo aliendelea kung’ang’ania kwamba yeye alikuwa bora zaidi.
LONDON, ENGLAND
UKITAKA majivuno nenda kwa Cristiano Ronaldo. Hajasubiri kutangazwa, amejitangaza mwenyewe kuwa yeye ni bora kuliko Lionel Messi na mastaa wengine wakongwe wa zamani. Amedai kwamba yeye ni namba moja katika soka.
Ronaldo alitoa kauli za kushangaza za majigambo wakati akihojiwa na Mwandishi wa BBC, Dan Roan huku akisema kuwa kiwango alichofikia katika soka ni cha juu zaidi na wala mwanadamu hawezi kuendelea tena zaidi ya hapo alipofika.
Staa huyo wa Real Madrid na timu ya taifa ya Ureno mwenye umri wa miaka 30 ndiye mfungaji bora wa Real Madrid wa muda wote baada ya kumpiku Raul Gonzalez wiki mbili zilizopita, pia ni mfungaji bora wa muda wote wa Ligi ya Mabingwa akiwa na mabao 82 huku pia akiwa amefanikiwa kutwaa tuzo ya mwanasoka bora wa dunia mara tatu.
“Sihitaji kusema kuwa nipo katika historia ya soka, mimi ni mkongwe mahiri, takwimu zinaongea,” alianza kujigamba Ronaldo katika mazungumzo hayo.
“Kuendelea kuwa bora zaidi ya hapa ni vigumu sana. Inabidi nijitahidi kuendelea kubaki hapa hapa tu kwa sababu hilo nadhani ndilo jambo gumu kwa mchezaji. Katika akili yangu najua mimi ndiye bora zaidi. Sijali watu wanachodhani au wanachosema. Katika akili yangu, siyo kwa mwaka huu tu, bali siku zote, mimi ni bora sana,” alisema Ronaldo.
Alipoulizwa kuhusu ulinganisho wake na hasimu wake wa Barcelona na timu ya taifa ya Argentina, Lionel Messi ambaye amechaguliwa mara nne kuwa mwanasoka bora wa dunia huku akifunga mabao 418 katika mechi 492, Ronaldo aliendelea kung’ang’ania kwamba yeye alikuwa bora zaidi.
“Ni suala la maoni tu, naheshimu maoni. Labda kwa maoni yako Messi ni bora zaidi yangu, lakini kwa akili yangu mimi ni zaidi kuliko Messi. Ni rahisi tu kama hivyo,” aliongeza Ronaldo.
Katika mahojiano hayo, Ronaldo pia aliulizwa kuhusu uwezekano wa kurudi tena katika klabu yake ya zamani ya Manchester United ambayo ilimuuza kwenda Real Madrid kwa dau la Pauni 80 milioni mwaka 2009 na kuvunja rekodi ya uhamisho.
“Nimesema mara nyingi, hakuna ajuaye ya baadaye. Kwa sasa nina furaha hapa Real Madrid lakini hakuna ajuaye ya baadaye. Nitalisema hili jibu mara nyingi kwa sababu hakuna ajuaye ya baadaye, lakini najisikia vzuri kuwa hapa. Bado nina mkataba na Real Madrid na nina furaha hapa,” aliongeza Ronaldo.
Katika hali ya kushangaza, Ronaldo aliibuka na kumtetea Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho ambaye anapitia kipindi kigumu na timu yake ya Chelsea hasa katika Ligi Kuu ya England huku akidai kwamba kocha huyo anamweka kileleni kwa ubora.
“Sishangazwi kwa sababu katika soka lolote linaweza kutokea. Ni kocha ambaye nimefanya naye kazi kwa miaka miwili na najua ubora wake. Najua sio yeye tu, bali hata Chelsea ipo katika wakati mgumu. Nikiwa kama raia wa Ureno nataka kumwona mtu wa Ureno akiwa juu muda wote. Kwa hiyo hilo ndilo ninalomtakia Mourinho apite katika hali hii mbaya na kuwafanya mashabiki wa Chelsea wawe na furaha,” alisema Ronaldo.
Ronaldo ambaye aliibukia katika Klabu ya Sporting Lisbon ya Ureno alidai kwamba anataka kuendelea kupiga soka kwa miaka mitano au sita ijayo kabla hajatundika daruga lake na kuachana na soka.