Mpango wa Kobbie Mainoo ni kusepa jumla
Muktasari:
- Staa huyo mwenye umri wa miaka 20 anataka kuachana na miamba hiyo ya Old Trafford kutokana na kukosa nafasi ya kucheza chini ya kocha Mreno, Ruben Amorim.
MANCHESTER, ENGLAND: KIUNGO Kobbie Mainoo ameripotiwa kwamba akili yake ipo kwenye kuachana jumla na Manchester United.
Staa huyo mwenye umri wa miaka 20 anataka kuachana na miamba hiyo ya Old Trafford kutokana na kukosa nafasi ya kucheza chini ya kocha Mreno, Ruben Amorim.
Mainoo ameanzishwa kwenye mechi moja tu msimu huu, ile Man United ilipokutana na udhalilishaji mkubwa wa kufungwa na timu ya daraja la chini, Grimsby Town kwenye Kombe la Ligi, Agosti. Staa huyo alilazimisha kuondoka kwa mkopo mwishoni mwa msimu uliopita, kwenye dirisha la majira ya kiangazi, lakini Man United iligoma kumruhusu aondoke.
Amorim alitarajia kumpanga Mainoo kwenye mechi ya Aston Villa, Jumapili iliyopita, lakini alipata majeraha mazoezini na kumfanya akose pia mechi iliyofuatia ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Newcastle United, Ijumaa iliyopita.
Kutokana na dirisha la uhamisho la Januari likibakiza siku chache tu kufunguliwa, Mainoo ameibuka upya na mpango wake wa kuondoka, lakini safari hii isiwe kwa mkopo.
Staa huyo anataka kuondoka jumla kwenda kujiunga na timu itakayompa nafasi ya kucheza ili kuweka hai matumaini yake ya kuwamo kwenye kikosi cha England kitakachokwenda kwenye fainali za Kombe la Dunia 2026 huko Amerika.
Napoli ni kati ya timu zinazomhitaji, ambako kama dili litatiki basi atakwenda kukutana na wachezaji wenzake wa zamani wa Old Trafford, kiungo Scott McTominay na straika Rasmus Hojlund.
Hata hivyo, Man United itashawishika kumuuza Mainoo kama tu itapokea ofa ya pesa ndefu kwa sababu kwa sasa ina pengo kubwa kwenye safu ya kiungo. Bruno Fernandes ni majeruhi na Casemiro amemaliza dakika 90 kwenye mechi tatu tu za Man United kwa msimu huu. Kinyume cha hapo, Man United itamruhusu Mainoo kuondoka kama itawapata viungo inaowasaka, ambapo kwenye mipango yao yupo Elliot Anderson, Carlos Baleba na Adam Wharton.