Mpango kumteka Mbappe wavuja
Muktasari:
- Mpango huo ulidaiwa kulenga watu maarufu 26 wanasoka, wasanii wa rap na wafanyabiashara matajiri.
PARIS, UFARANSA, NYOTA wa Ufaransa na Real Madrid, Kylian Mbappe alikuwa miongoni mwa watu maarufu waliolengwa katika mpango wa kutekwa nyara uliopangwa na genge moja nchini Ufaransa, mamlaka za nchi hiyo zimefichua.
Mpango huo ulidaiwa kulenga watu maarufu 26 wanasoka, wasanii wa rap na wafanyabiashara matajiri.
Gazeti la Ufaransa, Le Parisien, liliripoti kwamba mpango huo ulidaiwa kuratibiwa na kijana mwenye umri wa miaka 18, aliyetajwa kwa jina la Clement L.
Awali, kiongozi huyo wa genge la ujambazi alikuwa tayari amefungwa kwa kosa la wizi wa kutumia silaha baada ya kutambuliwa kuwa mmoja wa watu wawili waliohusika katika shambulio dhidi ya mfanyabiashara wa saa mjini Paris. Ilibainika pia kwamba Clement L alikuwa tayari anashikiliwa akisubiri kesi ya tuhuma za kuendesha biashara ya ukahaba pamoja na wizi.
Kiongozi huyo alikuwa gerezani, lakini baadaye iligundulika kuwa alikuwa akiendelea kutoa maelekezo kwa wenzake akiwa gerezani kupitia simu mbili za mkononi na kutumia Snapchat kwa jina la Lester Z. Chanzo kilicho karibu na uchunguzi huo kililiambia Le Parisien kwamba anwani za watu 26 matajiri, akiwemo Mbappe zilipatikana kwenye simu hizo.
Nyota huyo wa Real Madrid alikuwa miongoni mwa orodha iliyojumuisha mfanyabiashara mmoja raia wa China, wafanyabiashara wa vito na mfanyabiashara wa nyama kutoka Uturuki.
“Simu mbili zilikamatwa na walinzi wa gereza, na yaliyokuwamo ndani yake yalikuwa yakifichua mambo mengi. “Pia alitaka kumlenga msanii mmoja wa rap na mchezaji wa soka Kylian Mbappe,” chanzo kilisema.
Alipohojiwa, kijana huyo alidai kuwa siyo mpangaji mkuu wa mpango huo na akaomba aondolewe katika kifungo cha upweke, akidai aliacha shule alipokuwa akisomea mafunzo ya ufundi katika fani ya upishi, lakini sasa anataka kurejea masomoni na kuwa mpishi.
Licha ya ombi lake, mamlaka ziliamua aendelee kuwekwa katika mahabusu ya peke yake wakati uchunguzi wa tukio hilo ukiendelea.