Mourinho Miaka 25, pesa kibao
Muktasari:
- Kocha huyu alikuwa na nafasi ya kwenda Saudi Arabia au kurudi England ambako angepewa pesa nyingi zaidi lakini alichagua kutua Benfica kwa sababu anahitaji kujiunga na timu inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya na pesa sio kipaumbele chake.
LISBON, URENO: WIKI kadhaa zilizopita, kocha Jose Mourinho alijiunga na Benfica ikiwa ni siku kadhaa baada ya kutupiwa virago vyake na mabosi wa Fenerbahce ya Uturuki.
Kocha huyu alikuwa na nafasi ya kwenda Saudi Arabia au kurudi England ambako angepewa pesa nyingi zaidi lakini alichagua kutua Benfica kwa sababu anahitaji kujiunga na timu inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya na pesa sio kipaumbele chake.
Wakati anajiunga na Benfica, Mourinho pia alikuwa ndio anatimiza miaka 25 ya kuhudumu kama kocha mkuu katika timu mbalimbali alizofundisha barani Ulaya.
Leo tunazitazama akaunti zake na utajiri alionao hadi sasa kiasi cha kutowekea kipaumbele masuala ya pesa.
ANAPIGAJE PESA
Utajiri wake kwa sasa unakadiriwa kufikia Dola 150 milioni, akiwa na Fenerbanhce alikuwa akikunja Dola 11 milioni kwa mwaka na baada ya kuvunjia alilipwa fidia na kumfanya kupata zaidi ya Dola 14 milioni mbali ya mshahara ambao aliupata kwa mwaka wa kwanza.
Ukiondoa mshahara Mourinho ni mmoja kati ya makocha wachache ambao wamekuwa wakiingiza pesa za kutosha kupitia madili mbalimbali ya nje ya uwanja.
Amekuwa akifanya kazi za ubalozi na kampuni kama Adidas, Braun, American Express, Jaguar, Samsung, Heineken, EA Sports, Atlantis Hotels, Aud, Top Eleven na Hublot.
Mbali ya madili hayo ambayo yupo nayo kwa sasa aliwahi pia kuwa balozi wa kampuni ya kubetisha ya Paddy Power.
Kupitia kampuni hizi anaripotiwa kupata zaidi ya Dola 15 milioni kwa mwaka, mbali ya mshahara anaoupata kama kocha.
MSAADA KWA JAMII
Kocha huyu amekuwa akishiriki mechi mbalimbali za hisani kama Soccer Aid Initiative na Game4Grenfell, ambapo amekuwa akihudumu kama kocha na muda mwingine huwa kipa.
Wakati wa janga la virusi vya Corona mwaka 2020, Mourinho alishirikiana Age UK na Love Your Doorstep kutoa msaada wa vyakula kwa watu mbalimbali huko England.
Mourinho alikuwa sehemu ya kampeni ya Comic Relief mwaka 2016 ambayo ilikuwa na lengo la kusaidia watu wanaoishi bila ajira na wale wenye ulemavu.
Amekuwa balozi wa muda mrefu wa umoja wa mataifa kupitia mpango wa dunia wa chakula ambao una lengo la kusaidia watoto waishio kwenye mazingira magumu msaada wa chakula na maji.
MJENGO
Ana nyumba kwao Ureno na London. Nyumba ya London ina vyumba sita, aliinunua kwa Pauni 6.5 milioni na sasa inadaiwa kuwa na thamani ya Pauni 25 milioni.
BATA NA MAISHA BINAFSI
Amekuwa katika ndoa na mrembo wake Matilde Faria tangu mwaka 1989 na wamebahatika kupata watoto wawili, mmoja wa kike aitwaye Matilde na wa kiume anaitwa Jose Mario Mourinho Jr.
Mwanawe wa kiume ndio anaonekana kufuata nyayo zake kwenye masuala ya mpira wa miguu na anadaiwa kuwa anasomea ukocha kwa sasa.