Mourinho, Benfica bado kidogo tu
Muktasari:
- Mourinho, 62, kwa sasa hana timu baada ya kufutwa kazi na Fenerbahce kutokana na kushindwa kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
LISBON, URENO: KOCHA Mreno, Jose Mourinho awasili Ureno kwa ajili ya kumalizia mazungumzo ya kusaini mkataba wa kuitumikia Benfica.
Mourinho, 62, kwa sasa hana timu baada ya kufutwa kazi na Fenerbahce kutokana na kushindwa kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Upatikanaji wake umeibua tetesi nyingi kuhusu wapi ataenda, lakini kwa mujibu wa tovuti ya A Bola, Mourinho yuko tayari kurejea nyumbani Ureno na makubaliano yanaweza kukamilika ndani ya saa chache zijazo.
Benfica imeripotiwa kupiga hatua kubwa katika mazungumzo na Mourinho, ambaye alipewa kazi yake ya kwanza ya ukocha na klabu hiyo mwaka 2000.
Hata hivyo, alisimamia mechi 10 pekee kabla ya mabadiliko ya uongozi wa klabu kumfanya aandike barua ya kujiuzulu na kujiunga na Uniao de Leiria.
Mourinho alipata mafanikio makubwa na FC Porto aliyoiwezesha kushinda Ligi ya Mabingwa na baada ya hapo alijiunga na Chelsea na kupata jina kubwa kisha akafundisha timu nyingine Ulaya kama Real Madrid, Manchester United, Tottenham na Inter Milan.
Mourinho alionekana akiwa amevalishwa skafu ya Benfica huku mashabiki wakiwa pembeni yake alipowasili Ureno kwa ndege akitokea Barcelona Jumatano jioni na akazungumza na wanahabari.
"Sina cha kuwaambia. Kabla sijapanda ndege, waliuliza kama ningevutiwa (kuifundisha Benfica). Nilisema ndiyo, naweza kuvutiwa. Benfica waliniuliza rasmi kama ningevutiwa na nikawaambia nitarudi Ureno ningefurahi kufanya mazungumzo zaidi. Niliondoka klabu yangu ya awali wiki nne zilizopita. Ukiuliza kama nilitarajia kukaa hadi mwisho wa msimu bila kazi ya ukocha hiyo si asili yangu. Nataka kufanya kazi. Sikutaka kusema ndiyo kwa klabu isiyo sahihi kwa sababu mimi ni mfanyakazi sana.
Nilipokutana na uwezekano wa kuifundisha Benfica, sikusita mara mbili. Nikasema: "Nimevutiwa na ningependa," alisema Mourinho.
Benfica hivi karibuni ilitengana na kocha wao Bruno Lage (aliyewahi kuifundisha Wolves), baada ya kuanza msimu vibaya.
Klabu hiyo inataka kupata kocha mpya kabla ya mchezo wa wikiendi hii dhidi ya Vila das Aves.
Rais wa klabu, Rui Costa, alisema: "Tumefikia makubaliano na Bruno Lage kuachana na sisi. Namshukuru kwa yote aliyotufanyia, lakini tunaamini huu ni muda wa mabadiliko. Kuhusu kocha mpya, tunatarajia awe benchi dhidi ya Vila das Aves Jumamosi ijayo."
"Kocha wa Benfica lazima awe mshindi. Ni lazima awe kocha mwenye uwezo wa kuwakilisha klabu ya ukubwa huu na kuirudisha timu hii kwenye viwango vinavyohitajika.
Hatuzungumzii majina. Benfica kwa sasa haina kocha. Kitu pekee kilichotokea baada ya mechi kilikuwa mazungumzo ya kuachana na Bruno Lage."