Mourinho anamtaka Benzema Benfica
Muktasari:
- Benzema ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu, ataruhusiwa kuondoka kujiunga na Mourinho aliyewahi kumfundisha akiwa Madrid kama atakuwa tayari kufanya hivyo kwani Ittihad haina mpango wa kumzuia au kudai ada kubwa ya uhamisho.
MADRID, HISPANIA: KOCHA mpya wa Benfica, Jose Mourinho anahitaji huduma ya mshambuliaji wa zamani wa Real Madrid, Karim Benzema kutoka Al-Ittihad ambayo ipo tayari kumuuza kwa bei chee.
Benzema ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu, ataruhusiwa kuondoka kujiunga na Mourinho aliyewahi kumfundisha akiwa Madrid kama atakuwa tayari kufanya hivyo kwani Ittihad haina mpango wa kumzuia au kudai ada kubwa ya uhamisho.
Kwa mujibu wa mwandishi Ekrem Konur, Mourinho anataka kumsajili Benzema Benfica na huenda akajaribu kumsajili Januari na ikishindikana atasubiri hadi mwisho wa msimu huu.
Mara kadhaa Benzema ambaye ni raia wa Ufaransa amekuwa akimsifu kocha huyo kutoka Ureno kuwa alibadilisha sana maisha yake ya soka na kumfanya kuwa mchezaji bora huyu anayeonekana sasa.
Taarifa kutoka Saudi zinaeleza Al-Ittihad ipo tayari kukubali ada ya takriban Euro 7 milioni ili kumruhusu Benzema kuondoka kabla ya mkataba wake kuisha.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 37 atalazimika kukubali kupunguzwa mshahara kwa kiwango kikubwa iwapo atajiunga na miamba hiyo ya Ureno.
Kwa sasa analipwa Pauni 83 milioni na inawezekana akaenda kulipwa chini ya Pauni 10 milioni kwa mwaka atakapotua Benfica.
Mourinho alifundisha miaka mitatu Real Madrid kati ya 2010 na 2013, na alimfanya Benzema kuwa mchezaji muhimu.
Akiwa chini ya Mourinho Madrid, Benzema alifunga mabao 78 katika mechi 150, na kushinda Copa del Rey pamoja na taji la La Liga. Ndani ya kipindi hicho, Mourinho alimbadilisha Benzema na kuwa mmaliziaji hatari.
Mourinho amejiunga na Benfica baada ya kufukuzwa kazi na Fenerbahce ya Uturuki sababu kubwa ikielezwa kuwa ni kushindwa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.