DE Bruyne mambo magumu Italia
Muktasari:
- Michele ameyasema hayo akizungumzia changamoto wanazokutana nazo katika maisha yao ya kila siku nchini Italia tangu De Bruyne alipojiunga na Napoli mwaka 2025, akitokea Manchester City, ambako alitumia miaka 10 na kujijengea jina kubwa katika soka.
NAPLES, ITALIA : MKE wa kiungo nyota wa Napoli, Kevin De Bruyne, Michele, amefichua kuwa familia yao inatamani kurejea kuishi nchini Ubelgiji, akisema kadiri watakavyoweza kuondoka Naples mapema ndivyo itakavyokuwa bora zaidi kwao.
Michele ameyasema hayo akizungumzia changamoto wanazokutana nazo katika maisha yao ya kila siku nchini Italia tangu De Bruyne alipojiunga na Napoli mwaka 2025, akitokea Manchester City, ambako alitumia miaka 10 na kujijengea jina kubwa katika soka.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 35 amekuwa akikumbana na changamoto mbalimbali tangu alipowasili Italia, ikiwamo matatizo ya utimamu wa mwili pamoja na kutokuelewana na aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Antonio Conte.
Hali hiyo haijaonekana kubadilika sana hata baada ya Max Allegri kuchukua mikoba ya ukocha, huku Napoli ikikabiliwa na kipindi kigumu cha matokeo na kuripotiwa kuwepo kwa mvutano baina ya De Bruyne na baadhi ya wachezaji wenzake.
Akizungumza katika mahojiano na jarida la NINA la nchini Ubelgiji, Michele alisema familia yao imekuwa ikijadili mara kwa mara kurejea katika eneo la Limburg, Ubelgiji, wanakoliona kuwa nyumbani kwao.
“Ni kweli tunafikiria kuhusu maisha yetu ya baadaye kwa pamoja. Mara nyingi tunajikuta tukisema tutakwenda kuishi Limburg. Kadiri tutakavyoweza kwenda huko mapema ndivyo itakavyokuwa vizuri zaidi,” alisema Michele.
Alikiri kuwa Naples ni jiji zuri lenye hali nzuri ya hewa na chakula kizuri, lakini akasema maisha ya familia yao yamekuwa magumu kutokana na umaarufu wa mumewe.
“Kevin anaishi maisha yenye mipaka mingi sana akiwa Napoli. Si maisha yenye furaha sana kwake. Zaidi ya hapo, hatuwezi kufanya mambo mengi pamoja kama familia tunapokuwa jijini,” alisema.
Aliongeza kuwa hali ilikuwa tofauti walipoishi Manchester, ambako watu walikuwa wamewazoea kiasi kwamba waliweza kutoka nje na kutembea bila kuvamiwa na mashabiki waliotaka kupiga picha.
Hata hivyo, Michele alisema hali hiyo haiwezekani Napoli kutokana na umaarufu wa De Bruyne, jambo linaloathiri uhuru wao wa kifamilia.
“Katika hatua fulani ya maisha, soka haliwezi kuendelea kuwa kipaumbele. Tayari umefanikiwa, umefanya kila kitu. Kwa nini basi ubadilishe maisha ya watoto wako na kuwaweka katika mazingira magumu?” alihoji.
De Bruyne na Michele walioana mwaka 2017 na wamejaliwa watoto watatu, Mason, Rome na Suri.
Kwa upande wake, De Bruyne aliwahi kukiri kutofurahishwa na mfumo wa uchezaji wa Conte, akisema hakupata nafasi ya kucheza katika nafasi anayopendelea.
Kiungo huyo alisema kulikuwa na tofauti kubwa za kifalsafa za soka kati yake na Conte, huku akifichua kuwa hakufurahishwa na namna timu ilivyokuwa ikicheza kwa kujilinda zaidi.
De Bruyne alisaini mkataba wa miaka miwili alipojiunga na Napoli, lakini mustakabali wake katika klabu hiyo sasa unaendelea kuibua maswali.