Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kisa kifo cha DE Miguel, kipa afungiwa mechi 12

Muktasari:

  • Hata hivyo, licha ya adhabu hiyo, bado haijafahamika kama Owono atarejea tena kucheza soka, huku kocha wake, Carles Manso, akisema klabu itampa muda wa kutosha kuamua mustakabali wake.

TENERIFE, HISPANIA: KIPA wa FC Andorra, Jesus Owono, ameadhibiwa kwa kufungiwa mechi 12 kufuatia tukio la kugongana na mshambuliaji wa Tenerife, Jesus de Miguel, lililosababisha kifo cha nyota huyo wa soka mwenye umri wa miaka 30.

Hata hivyo, licha ya adhabu hiyo, bado haijafahamika kama Owono atarejea tena kucheza soka, huku kocha wake, Carles Manso, akisema klabu itampa muda wa kutosha kuamua mustakabali wake.

Tukio hilo la kusikitisha lilitokea mapema mwezi huu wakati mchezo baina ya Andorra na Tenerife ukiwa katika dakika za nyongeza za kipindi cha pili.

De Miguel alikuwa akijaribu kuanzisha shambulizi la kushtukiza kwa upande wa Tenerife baada ya kupokea mpira mrefu, lakini alikutana na goti la Owono aliyekuwa akiruka kuondoa mpira karibu na mstari wa kati wa uwanja.

Baada ya kugongana, De Miguel alianguka chini huku akionekana kupata maumivu makali. Wachezaji wenzake walipata mshtuko mkubwa na wahudumu wa afya waliingia haraka uwanjani kutoa msaada.

Owono alionyeshwa kadi nyekundu kutokana na tukio hilo, kabla mwamuzi kuamua kusitisha mchezo kutokana na uzito wa hali iliyokuwa imetokea.

De Miguel alipewa huduma ya kwanza kwa zaidi ya dakika tano, huku baadhi ya wachezaji wenzake wakionekana kulia kwa uchungu.

Baadaye aliondolewa uwanjani kwa machela huku mashabiki wote wakisimama kumpa heshima.

Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya Hispania, De Miguel alipata matatizo makubwa ya kiafya akiwa njiani kuelekea hospitalini na aliripotiwa kupata mshtuko wa moyo akiwa ndani ya gari la wagonjwa.

Licha ya juhudi za madaktari, baadaye alifariki dunia, huku klabu yake ya Tenerife ikithibitisha kifo chake kupitia taarifa rasmi iliyotolewa Novemba 3, 2026.

Katika taarifa hiyo, Tenerife ilieleza ma sikitiko makubwa kutokana na kumpoteza mchezaji huyo na kutoa pole kwa familia yake, ndugu, marafiki na mashabiki wote.

De Miguel alikuwa amekuwa baba mwaka uliopita, huku taarifa zikieleza kuwa mkewe na mtoto wao wa kike walikuwa uwanjani wakati tukio hilo lilipotokea.

Kwa upande wake, Owono amekuwa akikumbwa na wakati mgumu kufuatia tukio hilo, huku baadhi ya mashabiki wa Tenerife wakisikika wakimzomea na kumwita muuaji.

Katika taarifa yake ya awali, kipa huyo alieleza maumivu makubwa aliyokuwa akiyapitia kutokana na kumpoteza De Miguel.

“Hizi ni siku ngumu zaidi katika maisha yangu. Ninashindwa kupata maneno sahihi ya kuelezea kilichotokea na bado ni vigumu kwangu kukubaliana na hali hii.

“Nina maumivu makubwa kutokana na kumpoteza Jesus. Mawazo yangu yako kwake, familia yake na wote waliompenda. Kwa sasa siwezi kufikiria jambo jingine zaidi ya Jesus na maumivu tunayopitia. Pumzika kwa amani, Jesus,” alisema Owono. Kocha Manso alisema klabu haitamlazimisha Owono kurejea uwanjani, bali itahakikisha inampa msaada wa kutosha katika kipindi hiki kigumu.

“Tutampa nafasi na uhuru wa kufanya uamuzi wowote anaouona unafaa, iwe ni kurejea kucheza, lini arejee au kama ataamua kutorejea kabisa.

“Tunachopaswa kufanya ni kumuunga mkono kwa kila namna na kuhakikisha tunakuwa karibu naye,” alisema Manso.

Tukio hilo limeacha majonzi makubwa katika soka la Hispania, huku familia ya marehemu ikiomba iheshimiwe na kupewa faragha katika kipindi hiki kigumu.