Mourinho awa mbogo, Vini Jr kuikosa El Clasico
Muktasari:
- Nyota huyo wa kimataifa wa Brazil alitolewa kwa kadi nyekundu katika ushindi wa bao 1-0 wa Real Madrid dhidi ya Villarreal Jumamosi iliyopita.
MADRID, HISPANIA: MSHAMBULIAJI wa Real Madrid, Vinicius Junior, atakosa mchezo wa El Clasico dhidi ya Barcelona baada ya kufungiwa mechi nne kufuatia kitendo cha kuvuta nywele za Nathan Saliba.
Nyota huyo wa kimataifa wa Brazil alitolewa kwa kadi nyekundu katika ushindi wa bao 1-0 wa Real Madrid dhidi ya Villarreal Jumamosi iliyopita.
Adhabu hiyo inamaanisha atakosa michezo dhidi ya Sevilla Oktoba 18, Barcelona Oktoba 25, Racing Santander Novemba Mosi na Valencia Novemba 7.
Tangazo la adhabu hiyo limeibua hasira kwa kocha Jose Mourinho, hasa kwa kuwa lilitolewa saa chache kabla ya timu yake kucheza dhidi ya Roma katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, mchezo ambao Vinicius alishiriki.
Akizungumza baada ya timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 4-3 katika mchezo huo wa kusisimua, Mourinho alihoji sababu za kutangaza adhabu hiyo muda mfupi kabla ya mchezo kuanza.
“Unafikiri ni jambo la kawaida kwa mchezaji wa timu ya Hispania, ambayo inakwenda kucheza mechi muhimu kwa soka la nchi hiyo, kuambiwa saa mbili kabla ya mchezo kwamba amefungiwa mechi nne?” alihoji Mourinho.
Ameongeza kuwa uamuzi huo ungeweza kutangazwa asubuhi iliyofuata badala ya kufanya hivyo wakati timu ikiwa njiani kuelekea uwanjani.
“Kwa sasa wanafanya mambo bila aibu. Mambo yamewekwa wazi. Mchezaji anapaswa kuambiwa saa mbili kabla ya mchezo kwamba amefungiwa mechi nne,” amesema.
Mourinho pia alieleza kuwa timu za Hispania zinapopata pointi katika mashindano ya Ulaya huchangia kuongeza hadhi ya soka la nchi hiyo na nafasi yake katika viwango vya soka barani Ulaya.
Katika mchezo dhidi ya Villarreal, Vinicius aliingia dakika ya 52 na baadaye akadhani amefunga bao la pili kwa timu yake.
Hata hivyo, mwamuzi alikagua marudio ya tukio kwenye kifaa cha video pembeni ya uwanja na kubaini kuwa mshambuliaji huyo alivuta nywele za Saliba kabla ya kufunga. Bao hilo lilifutwa na Vinicius akaonyeshwa kadi nyekundu.
Kamati ya nidhamu ya Shirikisho la Soka la Hispania ilimfungia mechi mbili kwa kitendo kilichotafsiriwa kuwa cha vurugu dhidi ya mchezaji ambaye hakuwa katika nafasi ya kugombea mpira, huku akiongezewa mechi nyingine mbili kwa kupinga maamuzi ya waamuzi.
Baada ya mchezo dhidi ya Villarreal, Mourinho hakuhudhuria mkutano na waandishi wa habari uliofuata mchezo huo.
Vinicius naye aliomba radhi kupitia mitandao ya kijamii, akisema anawaomba msamaha wachezaji wenzake na mashabiki wa Real Madrid kwa tukio hilo.