Man City, PSG ni mechi ya kikubwa UEFACL
Muktasari:
- Kuelekea mchezo huo, kompyuta maalumu ya utabiri ya Opta imefanya mambo yake; safari hii Manchester City inapewa nafasi kubwa kidogo ya kushinda, ikiwa na uwezekano wa kufanya hivyo wa asilimia 44.1 ikilinganishwa na PSG asilimia 32.
MANCHESTER ENGLAND: KILE kipute cha Ligi ya Mabingwa Ulaya kinaendelea tena le baada ya mechi za jana Jumanne kupigwa katika viwanja vinane, na leo wakubwa barani humo watakuwa wakiendelea kuusaka ubingwa wa msimu huu wa 2026/27, mchezo mkubwa ukitarajiwa kuwa kwenye Uwanja wa Etihad ambapo Manchester City itawakaribisha mabingwa watetezi, PSG.
Kuelekea mchezo huo, kompyuta maalumu ya utabiri ya Opta imefanya mambo yake; safari hii Manchester City inapewa nafasi kubwa kidogo ya kushinda, ikiwa na uwezekano wa kufanya hivyo wa asilimia 44.1 ikilinganishwa na PSG asilimia 32.
Huo utakuwa mchezo wa tisa kati ya Manchester City na PSG, City ikishinda mara nne kati ya nane zilizopita, sare mara mbili na kupoteza mara mbili. Katika mechi nne ilizocheza nyumbani dhidi ya PSG, City haijapoteza hata moja ikiwa imeshinda tatu na kutoka sare moja.
Hata hivyo, katika mchezo huo PSG inaweza kuwa timu ya pili kucheza mechi 10 au zaidi mfululizo dhidi ya timu za England katika historia ya Kombe la Ulaya na Ligi ya Mabingwa Ulaya bila kupoteza.
Itakumbukwa hata hivyo kwamba Manchester City ilijibu changamoto zilizojitokeza katika kipindi cha wiki kadhaa zilizopita kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Liverpool kwenye Uwanja wa Anfield Jumapili kwenye Ligi Kuu England katika mchezo ambao Liverpool ilimaliza ikiwa na wachezaji 10.
Mashabiki wa City waliokuwa sehemu ya wageni walifurahia ushindi huo na kujivunia namna timu yao ilivyoonyesha uthubutu, baada ya kupatikana na hatia ya kukiuka kanuni za kifedha Ligi Kuu England kati ya 2009 na 2018. City imewasilisha rufaa huku ikisubiri taarifa kuhusu adhabu itakayochukuliwa dhidi yake.
Lakini, wakati City ikiwa katika ubora wake ikiwa haijapoteza mechi, katika miaka michache iliyopita PSG imebadilika kutoka timu iliyokuwa ikikaribia kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya bila mafanikio na kuwa mabingwa wa mashindano hayo mara mbili.
KAZI IMEANZA
Timu ya kocha Luis Enrique haijaanza vizuri sana msimu wa Ligi Kuu Ufaransa (Ligue 1), lakini huenda ikawa na nafasi ya kutumia miezi michache ya mwanzo kujipanga kabla ya kufikia kiwango chake bora. Hata hivyo, PSG ilianza harakati za kutetea taji la Ulaya kwa mara ya tatu mfululizo kwa kishindo mwezi uliopita ilipoifunga Slovan Bratislava mabao 6-1.
Katika mechi hiyo mshambuliaji Ousmane Dembele alikuwa mchezaji wa tatu wa PSG kufunga mabao mawili au zaidi na kutoa pasi mbili au zaidi zilizozaa mabao katika mchezo mmoja wa Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwafuata Kylian Mbappe na Lionel Messi. Liverpool pekee ndiyo timu nyingine iliyowahi kuwa na wachezaji watatu tofauti waliofanya hivyo katika mashindano hayo ambao ni Roberto Firmino, Mohamed Salah na Yossi Benayoun.
Dembele amehusika moja kwa moja katika mabao 31 kwenye mechi 41 za Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na PSG, akifunga 20 na asisti 11. Kwa sasa anashika nafasi ya tano kwa mchango wa mabao katika historia ya klabu hiyo kwenye mashindano hayo. Wanaomzidi ni Mbappe mwenye mabao 65 katika mechi 64; Neymar 37 katika mechi 41; Edinson Cavani 33 katika mechi 54 na Angel Di Maria 32 katika mechi 54.
Ni katika mchezo huo, mshambuliaji wa zamani wa City, Ferran Torres, alikuwawa mchezaji wa kwanza kufunga hat-trick katika mechi yake ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na klabu fulani tangu Robert Lewandowski alipofanya hivyo kwa Barcelona dhidi ya Viktoria Plzen Septemba 2022.
Vilevile PSG ilifanya matukio mengi zaidi ya kuunasa mpira katika eneo la juu la uwanja kabla ya kuanzisha mashambulizi (high turnovers), ikiwa na matukio 14, na pia ilikuwa na matukio mengi zaidi ya aina hiyo yaliyoishia kwa shuti, ikiwa na saba kuliko timu nyingine yoyote katika siku ya kwanza ya mechi za kampeni mpya ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Pia, ilikuwa na wastani mkubwa zaidi wa umiliki wa mpira, 72.1.
LEO VIPI?
Hata hivyo, safu ya ushambuliaji ya PSG inayocheza kwa kasi na kubadilishana pasi kwa ufanisi italazimika kutafuta njia ya kuipenya safu ya ulinzi ya City, ambayo tayari imecheza mechi tano bila kuruhusu bao msimu huu. Siyo kwamba City inakosa makali katika safu yake ya ushambuliaji.
Rayan Cherki amekuwa na wastani wa pasi 4.1 zinazopenya safu ya ulinzi ya wapinzani kwa kila dakika 90 alizocheza katika Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na City.
Tangu mwanzoni mwa msimu uliopita, huo ni wastani wa pili kwa ubora miongoni mwa wachezaji wote katika mashindano hayo waliocheza angalau dakika 300. Mchezaji pekee anayemzidi ni Lee Kang-In mwenye wastani wa pasi 4.5 ambaye kwa sasa amehamia Atletico Madrid akitokea PSG.
Kwa upande mwingine, iwapo atafunga bao katika mchezo huu, Erling Haaland atampita Sergio Aguero aliyefunga mabao 36 katika mechi 64, na kuwa mfungaji bora wa Manchester City katika historia ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kwa sasa, Haaland ana mabao 36 katika mechi 40.
Haaland pia amefunga mabao 42 katika mechi 39 za hatua ya makundi/hatua ya ligi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Hiyo ni idadi kubwa zaidi ya mabao yaliyofungwa na mchezaji yeyote tangu alipoanza kushiriki mashindano hayo msimu wa 2019/20.
Hata hivyo, jambo litakaloweza kuamua matokeo ya mchezo huo ni timu itakayoshinda vita ya kiungo, ambayo inatarajiwa kuwa ya kusisimua.
Vitinha wa PSG amekuwa miongoni mwa viungo waliofanya vizuri zaidi barani Ulaya katika misimu miwili iliyopita, kwani tangu kuanza kwa msimu uliopita anawaongoza viungo wote katika Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa pasi zilizofika kwa walengwa, akiwa nazo 1,703; pasi zilizopenya safu za wapinzani, 327; na matukio ya kuunasa tena mpira, 106.
Lakini, kumbuka kwamba kiungo huyo atakabiliana na viungo wenye nguvu wa City, Elliot Anderson na Enzo Fernandez. Anderson, hasa, ameanza vizuri sana akiwa na jezi ya City, huku akijaribu kusaidia kuziba pengo lililoachwa na Rodri aliyehamia Barcelona, ambapo alikuwa kinara katika ushindi dhidi ya Liverpool kwa kugusa mpira mara 100, pasi sahihi 71 kati ya 78 na kushinda mipambano ya kuwania mpira mara 11 kati ya 17. Hii ni fursa nyingine kwa kiungo huyo wa timu ya taifa ya England kuonyesha uwezo wake dhidi ya wapinzani wa kiwango cha juu.
HISTORIA MAN CITY VS PSG
Huo utakuwa mchezo wa tisa kati ya Man City na PSG. City imeshinda mechi nne kati ya nane zilizopita, sare mara mbili na kupoteza mara mbili. Katika mechi nne ilizocheza nyumbani dhidi ya PSG, haijapoteza, ikiwa imeshinda tatu na kutoka sare moja.
Miongoni mwa timu ambazo PSG imekutana nazo angalau mara tano katika mashindano makubwa ya Ulaya, Bayern Munich pekee ndiyo imeifunga PSG kwa asilimia kubwa zaidi ya mechi zake kuliko Manchester City. Bayern imeishinda PSG mara tisa katika mechi 17, sawa na asilimia 52.9, huku City ikiishinda mara nne katika mechi nane, sawa na asilimia 50.
PSG haijapoteza katika mechi zake 11 zilizopita za Ligi ya Mabingwa Ulaya, ikiwa imeshinda saba na kutoka sare nne. Ni mara moja tu katika historia ya klabu hiyo ambapo imekuwa na mfululizo mrefu zaidi bila kupoteza katika mashindano hayo ilipocheza mechi 13 kati ya Oktoba 2012 na Novemba 2013. Rekodi yake dhidi ya timu za England pia ni ishara nzuri kwa kikosi cha Luis Enrique.
PSG inaweza kuwa timu ya pili kucheza mechi 10 au zaidi mfululizo dhidi ya timu za England katika historia ya Kombe la Ulaya/Ligi ya Mabingwa Ulaya bila kupoteza. Kwa sasa haijapoteza mechi tisa, ikiwa imeshinda saba na kutoka sare mbili. Real Madrid ndiyo timu pekee iliyowahi kufanya hivyo awali, ilipocheza mechi 11 bila kupoteza kati ya mwaka 2011 na 2017.
MECHI ZINGINE
Mechi za leo, Jumatano, zitaanza kwa michezo miwili ya mapema, Feyenoord ikiikaribisha Como mjini Rotterdam, huku Liverpool ikisafiri kwenda Linz, Austria kukutana na LASK. Liverpool imeshinda mechi 25 kati ya 29 zilizopita katika hatua ya makundi au ligi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, hivyo itakuwa na imani ya kupata ushindi mwingine katika mchezo huu.
Isitoshe, hakuna timu ya Austria iliyowahi kuifunga ya England katika mashindano makubwa ya Ulaya tangu 1991, ambapo tangu wakati huo, timu za nchi hizo zimekutana mara 34 bila timu ya Austria kushinda, huku zikipoteza mechi 27 na kutoka sare sita.
Kutokana na hilo, Liverpool inapewa asilimia 70.7 ya ushindi, huku LASK ikiwa nazo 11.8. Ushindi mwingine wa ugenini unatabiriwa mjini Rotterdam, ambako Como inapewa asilimia 48.2 dhidi ya Feyenoord.
Mchezo mwingine utapigwa Roma, ambako mabingwa wa kihistoria, Real Madrid, wataifuata Roma, huku kikosi cha Jose Mourinho kikipewa asilimia 47.7 ya kushinda ilhali Kylian Mbappe anatarajiwa kucheza mechi yake ya 100 katika Ligi ya Mabingwa Ulaya. Akiwa na mabao 71, ni Lewandowski pekee aliyefunga mengi zaidi yake tangu aanze kushiriki mashindano hayo Septemba 2017, akiwa na mabao 76.
Nayo Borussia Dortmund itakabiliwa na mtihani mgumu itakapocheza ugenini dhidi ya Bodø/Glimt inayojulikana kwa kuwa ngumu kucheza nayo uwanja wake wa nyumbani. Tangu ilipoanza kushiriki mashindano hayo msimu uliopita imezishinda Inter Milan, Man City na Sporting CP kwenye Uwanja wa Aspmyra Stadion. Opta inaipa Bodo/Glimt asilimia 30.5 za udhindi dhidi ya 45.6 za Dortmund.
Aston Villa itakuwa mwenyeji wa Fenerbahce kwenye Uwanja wa Villa Park, ikiwa na lengo la kuendeleza rekodi yake ya kuvutia ya kushinda mechi 10 mfululizo za mashindano ya Ulaya nyumbani ikipewa asilimia 55.1. Ni mara mbili tu katika karne hii ambapo timu ya England imekuwa na mfululizo mrefu zaidi wa ushindi wa nyumbani katika mashindano makubwa ya Ulaya, Man City iliposhinda mechi 12 mfululizo kati ya 2022 na 2024, huku Man United ikifanya hivyo kati ya 2006 na 2008.
Kwa upande mwingine, unatabiwa ushindi wa nyumbani kwa Real Betis dhidi ya FC Porto, ikiwa na asilimia 45.6 ya nafasi ya kushinda. Huo utakuwa mchezo wa kwanza wa mashindano rasmi kati ya klabu hizo mbili. Wakati huohuo, Stuttgart ina nafasi kubwa ya kushinda dhidi ya Slovan Bratislava itakapocheza ugenini, ikiwa na asilimia 68.8.
Nayo AEK Athens itakutana na Shakhtar Donetsk katika mazingira yasiyo ya kawaida kwenye Uwanja wa Stamford Bridge, unaotumiwa na Chelsea na kwa mujibu wa Opta, Shakhtar Donetsk ina nafasi ndogo ya kuibuka na ushindi, lakini inaongoza kidogo dhidi ya AEK Athens kwa kushinda katika asilimia 36.9.